Connect with us

Kitaifa

Watanzania wawili watajwa wenye ushawishi zaidi Afrika 2023

London. Jarida la New African lenye makao makuu yake jijini London nchini Uingereza limeorodhesha Waafrika 100 wenye ushawishi mkubwa kwa mwaka 2023, wakiwamo Watanzania wawili – Marie Mbullu na Elizabeth Mrema.

Mrema ni naibu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), aliyeteuliwa Desemba 27, 2022 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kushika wadhifa huo uliokuwa chini ya Mtanzania mwingine, Joyce Msuya.

Msuya aliteuliwa kuwa katibu mkuu msaidizi wa masuala ya kibinadamu na naibu mratibu wa misaada ya dharura katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu (OCHA).

Pia, Jarida la New African limemtaja Mtanzania mwingine Marie Mbullu, mwanafunzi anayeishi nchini Marekani ambaye  hujihusisha na simulizi za Afrika kwenye mtandao maarufu wa TikTok.

Rais wa Kenya, William Ruto naye ametajwa na jarida hilo kuwa miongini mwa Waafrika 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi kwa mwaka 2023.

Nchi za Senegal, Afrika Kusini, Kenya, Misri, Ghana na Nigeria zimetajwa kutawala kwenye orodha hiyo.

“Orodha hiyo ina makundi tofauti ya wanaume na wanawake, ambao wameonyesha ubora, uvumbuzi, uongozi, uthabiti na maono katika nyanja mbalimbali.

“Wanajumuisha wanasiasa, wafanyabiashara, wenye viwanda, wanamazingira, wabunifu, wanasayansi, waelimishaji, wanamichezo.”

Elizabeth Maruma Mrema aliyezaliwa Januari 5, 1957, kabla ya kwenda kufanya kazi Umoja wa Mataifa mwaka 1994, alifanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akiwa mshauri na wakili mwandamizi.

Wakati akiwa wizarani, aliwahi pia kuwa mhadhiri wa masuala ya sheria ya kimataifa ya umma na diplomasia ya mikutano katika Kituo cha Ushirikiano wa Masuala ya nje na Diplomasia cha Tanzania.

Mrema ana shahada ya uzamili ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dalhousie, Halifax, Canada, stashahada ya uzamili ya uhusiano wa kimataifa na diplomasia kutoka Kituo cha Uhusiano wa Nje na Diplomasia cha Dar es Salaam na shahada ya kwanza ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Marie Mbullu

Marie Mbullu mwenye umri wa miaka 20 ni mwanafunzi Mtanzania anayeishi nchini Marekani na hutumia TikTok kushiriki maudhui yanayohusu  masuala mbalimbali ya Afrika.

Ni Mtanzania mwenye shauku kuhusu utamaduni wa Kiafrika, masoko na kuzalisha maudhui yenye kuelimisha na anamiliki chaneli ya mtandaoni ya Habari Njema inayojadili masuala ya kijamii yanayohusu Afrika kwa lugha ya Kiswahili.

Wanasiasa

Orodha ya wanasiasa wenye ushawishi mkubwa zaidi na nchi zao kwenye mabano ni Rais William Ruto (Kenya), Ibrahima Cheikh Diong  (Senegal), Dk Sidi Ould Tah (Mauritania), Tidjane Thiam (Côte D’Ivoire), Ngozi Okonjo-Iweala (Nigeria).

Wengine ni Rais wa Nigeria Bola Tinubu, Mamady Doumbouya (Guinea), Nadia Fettah Alaoui (Morocco), Tsitsi Masiyiwa (Zimbabwe), Ousmane Sonko (Senegal) na Akinwumi Adesina(Nigeria).

Wafanyabiashara

Orodha ya wafanyabiasha wenye ushawishi ni  Didier Acouete (Togo), Bahija Jallal (Morocco), André De Ruyter (Afrika Kusini), Profesa Benedict Okey Oramah (Nigeria), Riham ElGizy (Misri),  Samaila Zubairu(Nigeria), Simon Tiemtoré (Burkina Faso), Ham Serunjogi (Uganda), Karim Beguir (Tunisia), Ralph Mupita (Zimbabwe).

Wafanyabiashara wengine ni Aliko Dangote (Nigeria), Mohamed Kande (Côte D’Ivoire), Ibrahim Sagna (Senegal), Shola Akinlade (Nigeria), Serge Ekué (Benin), Jules Ngankam(Cameroon), Hassanein Hiridjee (Madagascar).

Wengine ni  Sim Tshabalala (Afrika Kusini), Bernard Koné Dossongui (Côte D’Ivoire), Coura Sène (Senegal), Pascal Agboyibor (Togo), Olugbenga Agboola (Nigeria) na James Mwangi (Kenya).

Wasomi na wanasayansi

Orodha ya wasomi na wanasayansi ni Moungi Bawendi (Tunisia), Nemat Talaat Shafik (Misri), Timnit Gebru (Eritrea), Ismahane Elouafi (Morocco), Chao Tayiana Maina (Kenya) na Anna Adeola Makanju (Nigeria).

Wabunifu

Orodha ya wabunifu imehusisha Ali Said Alamin Mandhry (Kenya), Teju Cole (Nigeria), DJ Snake (Algeria), Nana Darkoa Sekyiamah (Ghana), Omoyemi Akerele (Nigeria), David Diop (Senegal), Aïda Muluneh (Ethiopia), Tems (Nigeria), Pierre Thiam (Senegal), Serge Attukwei Clottey (Ghana).

Wengine ni Bassem Youssef (Misri), Editi Effiong (Nigeria), Burna Boy (Nigeria), Tyla Laura Seethal (Afrika Kusini),  Alice Diop (Senegal), Kaouther Ben Hania (Tunisia), Gims (DRC), Thebe Magugu (Afrika Kusini), Danai Gurira (Zimbabwe),  Mulenga Kapwepwe (Zambia), Ncuti Gatwa (Rwanda), Pretty Yende (Afrika Kusini).

Wengine ni Black Coffee (Afrika Kusini), Mariam Issoufou Kamara (Niger),  Wanuri Kahiu (Kenya), Malenga Mulendema (Zambia), Abel Tesfaye (Ethiopia), Victor Ekpuk (Nigeria), Jadesola Osiberu (Nigeria), Julie Mehretu (Ethiopia) na Lesley Lokko (Ghana).

Wanamazingira

Orodha ya wanamazingira ni Rashid Sumaila (Nigeria/Ghana), Irungu Mwangi (Kenya),  Elizabeth Maruma Mrema (Tanzania), Dk Musonda Mumba (Zambia), Ephraim Mwepya Shitima (Zambia) na Wanjira Mathai (Zambia)

Wanahabari

Orodha ya wanahabari ni  Fabrice Sawegnon (Côte D’Ivoire), Wode Maya (Ghana), Edward Enninful (Ghana), Charity Ekezie (Nigeria), Uncle Mo (Uganda), Nicolas Pompigne-Mognard (Gabon), Alan Kasujja (Uganda), Khaby Lame (Senegal), Chioma Nnadi (Nigeria) na  Anton Harber (Afrika Kusini).

Wanamichezo

Orodha ya wanamichezo ni Yassine Bounou (Morocco), Francis Ngannou (Cameroon), Kelvin Kiptum (Kenya), Patrice Motsepe (Afrika Kusini),  Victor Osmihen (Nigeria), Faith Kipyegon (Kenya), Biniam Girmay (Eritrea) na The Springboks (Afrika Kusini).

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi