Connect with us

Kitaifa

Katakata ya umeme yapaisha bei za nondo, mabati

Dar es Salaam. Kukosekana kwa umeme wa uhakika kumetajwa kuwa moja ya sababu iliyochochea kushusha uzalishaji wa bidhaa za mabati na nondo kwa asilimia 40 katika kiwanda cha MM Intergrated Steel.

Hali hiyo ya upungufu wa umeme kwa ujumla, ilitajwa pia na wafanyabiashara kuwa sababu ya kuongezeka kwa viwango tofauti vya bei kulingana na aina ya bidhaa husika.

Hilo limeelezwa leo Januari 6 na Mkurugenzi wa MM Intergrated Steel, Ratisy Kamania wakati akitoa maelezo ya utendaji wa kiwanda hicho kwa Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Dk Ashantu Kijaji alipofanya ziara katika viwanda hivyo kusikiliza changamoto zao.

Mkurugenzi huyo amesema kukatika kwa umeme kati ya Oktoba hadi Desemba kulifanya viwanda hivyo kupoteza siku mbili hadi tatu bila kufanya uzalishaji hiyo ni kutokana na umeme mkubwa unaohitajika katika uzalishaji ambao ni ngumu kuupata katika vyanzo vingine kama jenereta.

Amesema kiwanda hicho kinahitaji megawati 10 ili kufanya uzalishaji wake kwa siku.

“Hali hii ilifanya uzalishaji kushuka kwa asilimia 40 na hii ilifanya jumla ya tani 15,000 kushindwa kuzalishwa kutokana na changamoto hiyo.

Tofauti na MMI Steel, kiwanda cha Mabati Bora wamesema pindi umeme unapokatika wanalazimika kuwasha jenereta ili kuendeleza na uzalishaji.

“Inaongeza gharama za uzalishaji, kama umeme haukuwapo siku nzima tunatumia zaidi ya lita 50 kwa sababu tunatakiwa kuwasha godauni tatu na ofisi, bei zinabaki palepale,” amesema Sonenga Majanjara ambaye ni Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko kutoka Mabati Bora.

Wakizungumzia upungufu wa umeme ulivyowagusa, Jackson Assenga, ambaye ni muuzaji wa vifaa vya ujenzi amesema ilichangia kupanda kwa bei za bati na nondo.

Akitoa mfano wa aina moja ya nondo za ndani ambazo hazikunjiki vizuri alisema tani moja ilitoka Sh1.8 milioni hadi Sh2 milioni.

“Kwenye mabati bando moja ilikuwa Sh390,000 hadi Sh400, 000 lakini sasa ni kati ya Sh430,000 hadi Sh450, 000,” amesema Assenga.

Maneno yake yanaungwa mkono na mmoja wa wafanyakazi kutoka FMJ Hardware ambaye hakutaka kutaja jina,  aliyesema bei za bati za Kiboko zilifikia Sh330, 000 kutoka Sh290,000.

“Hii ilianza Novemba katikati, ila huenda zikashuka kwa sababu baadhi ya mabati ya rangi yameanza kupungua kwa Sh10, 000,” amesema.

Hata hivyo, huenda suala la upungufu wa umeme ikafikia ukomo hivi karibuni baada ya kutarajiwa kuwashwa kwa mitambo miwili katika mradi wa maji wa kufua umeme wa Julius Nyerere.

Desemba 31, 2023 alipokuwa akilihutubia Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Februari mwaka huu mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme katika mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere utawashwa rasmi na mwingine utawashwa mwezi unaofuata.

Akizungumzia suala hilo akiwa katika kiwanda cha MMI, Dk Kijaji amewaomba wenye viwanda kuwa wavumilivu katika kipindi kilichobakia kabla ya kuwashwa kwa mitambo hiyo ili waweze kuendelea mbele.

“Kikubwa wanacholalamikia ni upatikanaji wa umeme, lakini wote mnatambua hatua iliyofikia katika bwawa la Mwalimu Nyerere, hadi Februari tumemsikia mkuu wa nchi amesema hatutakuwa na uhaba wa umeme katika viwanda vyetu,” amesema Dk Kijaji.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo Dk Kijaji amesema imelenga kusikiliza changamoto wanazopitia wamiliki wa viwanda.

“Pia tunapita ili tuwaambie Watanzania kuwa vipo viwanda vinavyotengeneza bidhaa zenye viwango visivyokuwa na mashaka ambavyo vinafikia viwango vya kimataifa (ISO) na Shirika la Viwanda Tanzania (TBS). Pia tuwaambie watu wa Afrika Mashariki na Afrika wakaribie kwani tuna bidhaa zenye ubora,” amesema Kijaji.

Amesema wanapokwenda kufanya maandalizi ya sheria ya fedha mwaka 2014, wataangalia namna ya kulinda viwanda vya ndani ili viendelee kutengeneza ajira kwa vijana hasa kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zisiagizwe nje.

Katika hilo pia amesema ipo haja ya kuanzishwa kwa kampeni maalumu itakayokuwa inahamasisha matumizi ya bidhaa zilizozalishwa nchini kwa ajili ya kuongeza soko.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi