Kitaifa
Majaliwa: Tupinge ukatili, watoto wasikimbie familia
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka jamii kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto kwa kuwa vinasababisha watoto wengi kukimbia familia zao na kukosa makao maalumu.
Majaliwa amesema hayo leo Ijumaa, Januari 5, 2024, wakati wa hafla ya chakula cha mchana na watoto wanaolelewa katika makao ya kulelea watoto ya SWACCO yaliyoko Manispaa Songea, mkoani Ruvuma.
“Jamii kwa ujumla kila mmoja ashiriki katika kulinda haki na ustawi wa watoto wetu. Hii ni nguvu kazi ya Taifa letu, hivyo ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu letu sote. Mamlaka zinazohusika ziendelee kusimamia, kufuatilia na kuratibu vyema huduma za makao ya watoto zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali,” amesema Majaliwa.
Pia ameutaka uongozi wa mkoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kuwatembelea wadau wanaoshirikiana na Serikali kutoa huduma kwa wenye uhitaji.
Amesema hiyo itasaidia kutambua changamoto walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuwapa uelewa wa mipango na mikakati ya Serikali kuhusu huduma za ustawi wa jamii.
Kadhalika, ameitaka wizara inayohusika na masuala ya ustawi wa jamii iendelee kushirikiana na wadau kuongeza kasi ya utoaji elimu ya malezi chanya kwa wazazi au walezi na jamii kwa ujumla, ili kuwa na nguvu kazi yenye tija kwa Taifa.
“Nawashukuru wadau na wafadhili kwa kusimamia makao haya ili kuhakikisha watoto wetu wanapata huduma stahiki za malezi na mahitaji muhimu,” amesema Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuhakikishe kuwa watoto wote wenye ulemavu wanapewa fursa ya kupata huduma za jamii ikiwemo elimu na waache tabia za kuwaficha ndani badala yake washirikishe mamlaka ikiwemo viongozi wa mitaa, vijiji, kata na wilaya ili kupata msaada.