Connect with us

Kitaifa

Madaktari watoa mapendekezo kitita kipya NHIF

Dar es Salaam. Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimesema kimewasilisha hoja na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuufanya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuwa stahimilivu, wakati wakisubiri maoni ya kamati huru itakayoundwa na Waziri wa Afya.

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa jana Januari 5, 2024 katika kikao cha pande hizo mbili kwa lengo la kujadili ada ya usajili na ushauri wa daktari katika kitita kipya kwa manufaa ya pande zote.

Kikao hicho ni matokeo ya NHIF kufanya mapitio ya kitita cha mafao kwa mwaka 2023, Desemba 18 yaliyoibua sintofahamu baada ya madaktari bobezi kuyalalamikia wakidai kutoshirikishwa, huku wamiliki wa hospitali binafsi wakidai kwamba hawakuafikiana.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Januari 6, 2023 Rais wa MAT, Dk Deus Ndlanha amesema kikao hicho kilikwenda vizuri na wao kupata nafasi ya kuwasilisha hoja walizonazo.

“Baada ya kukaa vikao vyetu vya kichama na kukutana na wadau tofauti, tuna hoja ambazo tulikuja nazo,  tulipata nafasi ya kuziwasilisha  kwa uongozi wa NHIF ni jinsi gani kwa kufanya hivyo, kutakuwa na  manufaa kwa watoa huduma na wamiliki wa vituo,” amesema.

Dk Ndilanha amesema kuna maeneo ambayo waliambiwa kwamba Waziri ataunda kamati ambayo itayapitia, hivyo wana imani kamati itakuwa huru na itapata nafasi ya kuwasikiliza.

Amesema wanaamini pia kamati itapata maoni ya wadau na kuona ni namna gani wanakuja na maboresho yenye faida kwa pande zote, lakini kuna yale ambayo yapo ndani ya NHIF wenyewe.

“Wamechukua maoni na hoja ambazo zitawasaidia, MAT hatukuangalia upande wetu tulijaribu kuangalia na mfuko kwa ujumla kwa namna gani kuna mambo wakifanya yanaweza yakausaidia mfuko ukawa stahimilivu na lile tishio la kwamba unaelemewa litaisha,’’ amesema.

Dk Ndilanha amesema kuna maeneo wamekubaliana watashirikiana na kuna maeneo wamechukua maoni na watakwenda kuyafanyia kazi.

Amesema wanasubiri kamati iliyoundwa na Waziri na wanaamini itasaidia.

, “Kuna maeneo tumependekeza kuwa sisi kama wasemaji wakuu wa madaktari tupate nafasi ya kushirikiana ili tuwe na uelewa wa pamoja halafu ndiyo tunaenda kwenye jamii,” ameeleza.

Kuhusu gharama iwapo walikuwa na mapendekezo, Dk Ndilanha amesema NHIF walikuwa na hoja zao na wao pia ambazo zote zitapelekwa kwa kamati teule na uamuzi utatoka huko.

“Tunaamini itaangalia mapendekezo na uhalisia katika soko na itakuja na majibu baada ya kuangalia pande zote kiwango kipi ni stahiki na haitaelemea upande wowote, watakachokipata watakileta kama kilivyo kwa manufaa ya nchi,” amesema Dk Ndlanha.

Ofisa Uhusiano wa NHIF, Grace Michael amesema walikutana na MAT kama ambavyo wanafanya kwa  makundi mengine kwa ajili ya kujadiliana kuhusu kitita hicho.

Amesema madaktari wamekiri kwamba wao hawawezi kuacha kutibu wanachama wa NHIF na hawapo tayari kuona mfuko ukifa kwa sbabau ndiyo nguzo pekee ambayo imeshikilia vituo vya afya binafsi nchini.

“NHIF imekuwa sehemu ya kukuza hivi vituo na ndiyo maana vinajiendesha, vinajiendeleza, vinajiboresha na kupanua huduma zake na wananchi kwa ujumla mbali na wanachama wanapata huduma hivyo wao wapo tayari, wanachosubiri ni majibu ya kamati,” amesema Grace.

Januari 4, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alikutana na kufanya mazungumzo na Umoja wa  Wamiliki wa Vituo vya Afya Binafsi (APHFTA), ambapo alisitisha bei mpya za kitita cha matibabu zilizowekwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), huku akitangaza kuunda kamati huru itakayofanya mapitio ya maboresho yaliyofanyika.

Kusitishwa huko kwa bei ambazo zilipangwa kuanza kutumika Januari Mosi, kunafuatia tishio la hospitali binafsi kusitisha huduma za matibabu kwa wenye kadi za NHIF na hivyo kulazimu mazungumzo na waziri.

Baada ya majadiliano ya kina kwa pande zote mbili, Waziri alisema angeunda kamati huru itakayofanya mapitio ya bei za kitita cha huduma za afya cha NHIF.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi