Kitaifa
TMB yaanika sababu ya bei nyama kupaa
Dar es Salaam. Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Kanda ya Mashariki imesema kupanda kwa bei ya nyama jijini Dar es Salaam kumetokana na uhaba wa ng’ombe.
Imesema wafugaji wamepunguza kuuza ng’ombe katika msimu wa mavuno.
Agosti, mwaka huu kilo ya nyama kwa jumla ilikuwa Sh 6,500 na rejareja ilikuwa Sh 7,500 lakini kuanzia Septemba mosi, mwaka huu bei ya jumla imekuwa Sh8,500 na rejareja imekuwa Sh10,000.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMB Agosti 25 ng’ombe wa kilo 200 alikuwa anauzwa Sh1.75 milioni, wa kilo 100 alikuwa Sh 810,000 na wa kilo 80 alikuwa Sh450,000.
Hadi kufikia Desemba 22,2023 bei ya ng’ombe mmoja katika mnada wa Pugu ilikuwa Sh2.49 milioni kwa ng’ombe wa kilo 200, huku wa kilo 100 akiuzwa kwa Sh1.295milioni na kilo 80 akiuzwa Sh 650,000.
Akizungumza na Mwananchi jana Ofisa Masoko wa Bodi ya nyama (TMB), Nicholai Chiweka alisema mara nyingi nyama inapanda kutokana na upatikanaji wa mifugo katika soko la minada.
Alisema wanaofuga mikoani ni wakulima ambao wanawezesha upatikanaji wa mifugo hivyo wapo ambao hawafugi katika hali ya biashara bali kwa malengo binafsi.
“Wafugaji wanaofuga kwa malengo binafsi wao wakiuza wanalenga kwa ajili ya kupata fedha za labda matibabu, kununua chakula na kulipa ada za watoto, hivyo kupanda kwa gharama inamaanisha watu hao wameshikilia mifugo yao,” alisema.
Alisema mvua inaponyesha mara kwa mara mifugo hupata chakula cha kutosha hivyo hawahangaiki kuwatafutia chakula wala kuiuza.
“Neema ya mvua ikiwapo wafugaji wanakuwa na chakula cha kutosha hivyo hawatumii ng’ombe kama sehemu ya kupatia kipato kwa sasa, wafugaji wanaweka akiba kwa ajili ya matumizi ya baadae.”
Alisema wananchi wanatakiwa kuangalia kipindi cha Januari kinakuwa na mabadiliko ya gharama za nyama kwa sababu ni kipindi ambacho wakulima wanakuwa kwenye maandalizi ya mashamba.
Chiweka alisema biashara ya mifugo ni soko huria hawana mamlaka ya kupanga bei ya mifugo hivyo nguvu ya soko ndiyo itakayoongeza au kupunguza gharama za mifugo na nyama sokoni.
Gabriel Ngoka, muuza nyama soko la Mabibo alisema upandaji wa nyama kwa kipindi cha miezi minne inatokana na uwepo wa vyakula vya kutosha katika mikoa wanayoagiza mifugo hiyo, kwa hiyo wafugaji wengi hawauzi mifugo hiyo kwa kuwa tayari wanakuwa na utoshelevu wa mahitaji yao.
“Wengi wao wanauza ng’ombe kwa kuangalia mahitaji kama kipindi hiki wameshavuna wanavyakula vya kutosha ndani, hivyo shida zao wanamaliza kwa kuuza mazao waliyonayo hawategemei mifugo tena,” alisema Ngoka.
Naye Joel Meshacky, muuza ng’ombe machinjio ya Vingunguti alisema kwenye mikoa wanayonunua ng’ombe, kipindi hiki malisho yamepungua.
Alisema hali hiyo inachangia kuingizwa mnadani ng’ombe wasio na ubora hali inayowafanya wauzaji wa nyama wengi kutowanunua na wanunuzi nao wanaacha kuwauza kuogopa hasara.
Meshacky alisema kutokana na uchache huo, wahitaji wanakuwa wengi kwa hiyo wanajikuta ng’ombe wa kilo 100 aliyenunuliwa kwa Sh500,000 kipindi cha malisho mengi, hivi sasa anauzwa kwa Sh1 milioni
“Hesabu hizo zinasababisha kupanda kwa gharama ya nyama. Huwa tunaangalia, ili nilinde mtaji wangu na kupata faida kidogo sana, inanibidi niuze kilo moja kwa Sh8,500 hadi Sh10,000 na mauzo ya makongoro, miguu na utumbo napata pesa ya kula,” alisema Meshacky.
Lakini pia alisema kingine kilichochangia bei hiyo kupaa ni ongezeko la mahitaji hasa kipindi hiki cha sikukuu.
Meshacky alisema wauzaji nao hutumia kipindi hiki kupandisha bei kiholela lakni baada ya msimu kupita, bei hurejea katika hali ya kawaida.
“Siku hizi za sikukuu nyama hupanda kwa sababu inamshawishi mtu ambaye si mlaji wa kula, siku hiyo naye aitafute kwa ajili ya familia yake,” alisema.
Alisema upandaji wa gharama za mifugo katika minada unaweza kupungua endapo wafugaji wakiamua kutumia ushauri wa Serikali kuwa na mashamba ya majani.
Hasnath Salum, mamalishe wa Vingunguti alisema amepunguza ukubwa na idadi ya vipande vya nyama anayouzia wateja wake kutoka viwili vikubwa vya awali na sasa anaweka kipande kimoja na mboga za majani na maharage kwa sahani ya wali anayoiuza Sh1,500.
Anna Stanslaus, muuza supu Mabibo alisema bei ya nyama inawasumbua ambapo awali alikuwa ananunua kilo moja kwa Sh8,000 sasa ananunua Sh 11,000.