Connect with us

Makala

Zingatia mambo haya ufanikiwe 2024

Kwa mujibu wa tovuti ya insideout master, umri 0-12 ni kundi tegemezi, (13-20) ni maandalizi ya kujitegemea, (21-35) kujitegemea na kuwekeza katika ndoto, (35-56) ni kupindi cha kutegemewa na wengine na miaka (57 – 65) ni kusaidia wengine. Miaka 66 na kuendelea ni kipindi cha kufurahia maisha.

Hata hivyo, licha ya mpangilio wa maisha kuwa hivyo, wakati mwingine huwa vigumu kufanikisha ndoto katika umri husika kutokana na mazingira yanayomzunguka mhusika.

Mathalan, mchambuzi wa masuala ya kijamii, Abdul Fatah Lyeme anasema uzoefu unaonyesha umri 21-35 unaathiriwa na utayari wa kufanya uamuzi sahihi na kutenda kwa wakati.

“Kwa mfano, mkandarasi anakamilisha mradi lakini Serikali inachelewesha kulipa, kwa hiyo mipango yake yote inaathiriwa na mazingira hayo, hii inamrudisha nyuma kimaendeleo. Lakini kuna sababu za kujitakia kwa wale wasioheshimu dhamana wanayopewa, ambao wengi ni vijana,” anasema Lyeme.

Mbali na hilo, tatizo jingine, ni kutoheshimu thamani ya muda katika matumizi ya kila sekunde, kama anavyoeleza Sheikh Khamisi Mataka, mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata.

“Sekunde ndiyo inazaa dakika, saa, siku, mwezi na mwaka, kwa hiyo ni muhimu kila sekunde ujiulize umeingiza maarifa gani mapya yatakayoongeza thamani katika maisha ya kila siku, au umezalishaji nini na umesaidiaje wengine. Je, umetumiaje muda wa kupumzisha mwili na akili?” anahoji.

“Hiyo ndio inakuwa dira ya mwaka katika kujipima kila baada ya siku, mwezi na baadaye mwisho wa mwaka. Unafanya tathmini ya kuchambua mahali ulipokwama, unaangalia udhaifu wako, fursa ulizonazo, ushawishi na changamoto za kimazingira, kama tutazingatia njia hizo itasaidia sana kupunguza makosa.

“Ni muhimu kujua ulipanga kufanya nini, umefanikiwa kwa kiwango gani na umeshindwa wapi. Je, ulichofanikiwa ni kwa matarajio au ni bahati tu, uliposhindwa ni sababu gani zimechangia ukashindwa, ni muhimu sana kufanya uchambuzi huo na kupanga kama kuna watu unahitaji kuwaona 2024 ukutane nao,” alisema.

“Hakuna mtu anapenda kuishi maisha ya kimaskini, ni muhimu kujipanga ili mwaka 2024 pia uwe mwaka wa kutegemewa. Usiposaidia ndugu au watu wako wa karibu shida, hazitapungua kwako,” anasema Sheikh huyo.

Kuhusu muda, mwanasheria na waziri mkuu wa kwanza wa Singapore 1959/1990, Lee Kuan Yew anasema vijana wengine wanajisahau katika muda wa kuanza maisha kwa ajili ya kupata watoto na badala yake wamejikita kutafuta elimu zaidi.

Yew aliyejichukulia umaarufu kupitia ushauri wake kwa mwanafunzi wa kike wa shahada ya uzamivu, anasema kadiri unavyochelewa kuoa au kuolewa ndivyo unavyotengeneza mazingira magumu ya kuhudumia watoto utakaowapata kwenye maisha ya ndoa wakati ukiwa na nguvu za kufanya kazi.

Marafiki wema

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Reuben Andrew anataja jambo jingine la kuwa makini nalo ni aina ya marafiki. Anasema kuna uhusiano mkubwa kati ya mafanikio na aina ya marafiki ulionao.

Andrew anasema ameshuhudia baadhi ya watu wakibadilika kupitia marafiki.

“Ukizungukwa na marafiki waliooa na wewe lazima utajikuta umeoa tu, ukiwa na marafiki wanamiliki magari utashawishika ununue pia bila hata kukwambia, nimejijengea utamaduni wa kuwa na marafiki wanaonizidi kipato au wenye mawazo ya kunipa changamoto, imenisaidia,” alisema.

Uthubutu

Jambo la nne la kutazama linaelezwa na Michael Mahumbi, mkurugenzi wa Taasisi inayoendesha elimu ya kujitambua kwa wanafunzi (MTS), aliyetilia mkazo umuhimu wa kuthubutu.

“Watu wengi wanaelewa mbinu nyingi za mafanikio, lakini hawathubutu kujaribu na kuweka nia. Ni muda wa kuchukua hatua 2024.”

Nidhamu binafsi

Uthubutu unakwenda sanjari na jambo la tano ambalo ni nidhamu binafsi, suala ambalo Mahumbi anaona linakosekana.

“Vijana wengi wakimaliza masomo huanza kulalamikia Serikali au shetani, hawataki kupitia kipindi cha maumivu wakati wa utafutaji. Kwa hiyo kuna haja ya vijana wetu kufundishwa kuwa na malengo makubwa,” anasema Mahumbi.

“Kuna vijana wengi hawafahamu kwamba kesho inategemea maamuzi ya leo. Changamoto ni kwamba wengi hawajafundishwa kuipenda kesho, wengi hawako tayari kulala njaa leo ili kulinda utu wao, bora auze mwili ili apate chakula leo lakini hajui madhara ya kesho yake.”

Mahumbi alisema kwa mwaka 2024 ni muhimu vijana waepuke utamaduni wa kuishi ndoto za watu wengine, wafikirie ndoto kubwa zinazoleta matokeo chanya.

“Unapenda kuimba, kwa hiyo ni sahihi unaposhinda studio lakini unataka udaktari halafu unashinda studio, basi umekosea mahali.”

Wakati vijana wengi wakionekana hawajajipanga au kupangilia malengo yao, Advera Mufuruki, mhitimu wa Shahada ya Jioinfomatikia inayohusisha Sayansi ya Dunia (GIS) na uchambuzi wa taarifa za kijiografia Chuo Kikuu Ardhi, anasema baada ya kumaliza masomo yake mwaka huu anakusudia kuanza kutafuta kazi.

“Nitafanya maombi ya kazi katika ofisi kadhaa, nikipata mojawapo nianze kazi wakati huo nikitafuta ufadhili wa kusoma shahada ya uzamili kwa ajili ya kuongeza maarifa na ujuzi,” anasema.

Mipango ya Advera inalandana na ya vijana wengi walioko shuleni na vyuoni. Ni kupata kazi.

Hata hivyo, suala hilo kwa sasa limekuwa gumu, wahitimu wakiwa wengi na fursa za ajira zikipungua.

Hali hiyo inajitokeza hivyo, wakati ripoti ya Jukwaa la Wachumi duniani 2023 likiorodhesha fursa ya ajira zinazokua kwa kasi, ambazo vijana wanaweza kuziangazia kuanzia mwaka unaokuja.

Ajira nane zinazokua kwa kasi ni uzalishaji data, elimu na teknolojia ya ukuzaji wa nguvukazi, usalama wa kimtandao na teknolojia ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Fursa nyingine zinazotajwa ni huduma za mifumo ya kompyuta, majukwaa ya kidijitali na uzalishaji wa programu tumizi, huduma saidizi za intaneti na vifaa unganishi pamoja na biashara ya kimtandao.

Ripoti hiyo imetumia kampuni 803 zilizoajiri watu zaidi ya milioni 11 katika mabara duniani.

Katika mfumo wa ajira milioni 673 zilizoonyeshwa katika kanzidata za ripoti hiyo, waliohojiwa wanatarajia ukuaji wa nafasi za kazi milioni 69. Hata hivyo, ripoti hiyo inabainisha pia kupungua kwa nafasi za kazi milioni 83 ndani ya miaka mitano ijayo.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi