Kitaifa
Nusu kaputi, ‘Pethidine’ zatumika kunogeshea shisha
Dar es Salaam. Kama wewe ni mpenzi wa shisha anza kujitafakari, kwani wafanyabiashara wa kiburudisho hicho wamegundulika kutumia dawa za tiba shufaa ‘Pethidine’ pamoja na zile zenye asili ya kulevya kukinogesha.
Hayo yamebainika katika operesheni iliyofanyika katika mikoa 13 nchini na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), iliyogundua uwepo wa dawa zenye madhara ya kulevya aina ya ‘Pethidine’ kwenye maeneo mbalimbali zikiuzwa kwa siri.
Matokeo ya oparesheni hiyo maalumu yaliyotolewa leo Jumatano, Desemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam yametokana na kukamata dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya Serikali, dawa zisizo na usajili na dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa wataalamu, dawa hizo husababisha uraibu kwa mtumiaji lakini pia zina athari kwa kujenga usugu mwilini, hivyo muhusika kushindwa kutibika kwa dawa hizo iwapo ataumwa au atahitaji kufanyiwa upasuaji.
“Madhara yanayoweza kujitokeza, anayetumia nusu kaputi atahitaji kiasi kikubwa zaidi cha dawa akihitaji kufanyiwa upasuaji. Hii ni sawa na mtumiaji wa pombe kupita kiasi kwa muda mrefu, akiuguwa na tiba yake kuhitaji dawa za usingizi ili zifanye vizuri atawekewa nyingi au zisifanye kazi vizuri,” amesema Mfamasia na mkufunzi wa shule ya famasia kutoka Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Mnyemba.
Mnyemba amesema matumizi ya dawa hizo kwenye viburudisho mbalimbali ikiwemo shisha au kuchanganya kwenye vinywaji hutengeneza uraibu.
“Anapotengeneza uraibu au utegemezi wa dawa kwenye damu yake ile dawa inakuwepo muda mwingi, hivyo kama atahitaji upasuaji itawalazimu wataalamu watumie dawa nyingi kupita kiasi ili kuweza kumlaza,” amesema.
Akisalia kwenye nusu kaputi, Mnyemba amesema mtu anapoitumia kwa muda mrefu hawezi kuacha na dozi anayotumia leo, kesho haitamtosha.
“Asipotumia anajisikia vibaya hata kama anaumwa na akapewa hizo dawa kama atazidisha anaingia kwenye uraibu, lakini atapata madhara kiafya kwa maana akitumia hulala na zinamkolea zaidi akiwa usingizini hivyo madhara yake ni pamoja na kifo cha ghafla,” amesema.
Akiizungumzia Pethidine, amesema ni dawa ya kuondoa maumivu makali ambayo hutumika kama tiba shufaa kwa wagonjwa waliopata ajali mbaya, wenye saratani au waliofanyiwa upasuaji.
“Ni dawa maumivu makali ambayo inaleta mtu kujisikia raha na ina uraibu ikitumika sivyo ndiyo maana zinadhibitiwa, madhara yake hutengeneza uraibu kama dawa za kulevya asipotumia anapata maumivu makali, atatapika hawezi kuishi bila kuzitumia, pia zinaathari kiuchumi na kupoteza nguvu kazi,” amesema Mnyemba.
Akilizungumzia hilo, mkazi wa jijini hapa Juma Ally (26) amekiri kuwahi kutumia dawa hizo.
“Kinondoni zinapatikana lakini zinauzwa kwa siri sana, mtaani wanatumia kama starehe lakini mateja wanazitumia zaidi, niliwahi kupewa na daktari nikazitumia lakini kuna wakati nilitamani nipate kila siku nikajizuia nikaacha,”amesema Ally.
Akisoma matokeo ya oparesheni hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo ametaja dawa za nusu kaputi zilizokutwa kwenye maduka ya dawa ambazo haziruhusiwi kutumika wala kuuzwa nje ya hospitali. “Mtandao wote umebainika na wahusika wamefahamika na wanachukuliwa hatua.
Fimbo amesema dawa tiba zenye asili ya kulevya zimechepushwa kutoka katika mnyororo wa ugavi na kuuzwa katika maduka ya dawa, ambapo mara nyingi zimekuwa zikitumika kwenye shisha na mbadala wa dawa za kulevya.
Kamishna ukaguzi na sayansi jinai kutoka Mamlaka ya Dawa za Kulevya, Domician Dominic amesema wanafanya kazi kwa karibu kufuatilia dawa tiba zenye asili ya kulevya zisichepushwe na kutumika kama dawa za kulevya.
“Lakini bado wapo watu wachache wanakiuka na kuchochea, zinatumika kiholela zinachanganywa kwenye vinywaji, shisha au na dawa zingine za kulevya,” amesema.
Dominician amesema kazi ya kupambana na uuzwaji holela wa dawa za binadamu zenye asili ya kulevya ni kubwa na ina changamoto nyingi kwenye udhibiti.
“Kazi siyo ndogo ni kubwa, natoa wito kwa kushirikiana na mamlaka zote za Serikali hakuna eneo tutaliacha lipumue, kupita tiba zenye asili ya kulevya, dawa za viwandani na uchepushwaji wa kemikali tashirifu zinazotumika kutengenezea dawa hizi,” amesema Dominician.
Kwa upande wa Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Daniel Nyambabe amesema katika operesheni hiyo wamefungua majalada, 13 yapo kwenye upepelezi chini ya ofisi ya Mkuu wa Mashtaka.
Katika operesheni hiyo jumla ya majengo 777 yalikaguliwa na kati yake 283 ni famasi, 23 maduka ya vifaatiba, 9 maghala ya dawa, maghala mawili ya vifaa tiba, 105 maduka ya dawa za mifugo, 272 maduka ya dawa muhimu za binadamu na vituo 30 vya kutolea huduma za afya, maabara 32 na kiwanda kimoja.