Connect with us

Kimataifa

Uganda kuwanyang’anya magari mawaziri, katibu wakuu

Uganda. Wakati Uganda ikijiandaa kwa mikutano ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa (NAM) na G77+China, Serikali nchini humo imepanga kuchukua magari kutoka kwa maofisa wake ikiwemo mawaziri na makatibu wakuu kuanzia Jumatatu ya Desemba 18, 2023.

Mkutano wa 19 wa NAM utafanyika kuanzia Januari 15 hadi 20, 2024 na G77+China kuanzia Januari 21 hadi 23, 2024 ambayo itakayofanyikia Speke Resort Munyonyo.

Katibu wa kudumu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni, Vincent Bagiire amesema leo, Desemba 15, 2023 kuwa mpango huo wa kuyachukua magari ya vigogo wa Serikali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi na maofisa huenda yakaathiri shughuli zao pamoja na sikukuu za mwisho wa mwaka.

Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Monitor, kiongozi huyo amesema kwa miaka mingi viongozi hao wamekuwa wakitumia sikukuu za mwisho wa mwaka kurejea vijijini kwao wakiwa na magari hayo ambayo sasa watapaswa kuwarejesha na hakueleza baada ya hapo watatumia usafiri gani.

Taarifa ya Bagiire imebainisha magari yanayotumiwa na vigogo hao yataegeshwa katika viwanja vya Uhuru Kololo kwa ajili ya ukaguzi na matengenezo.

Amesema yatarejeshwa kwa maofisa wenye haki baada ya mikutano hiyo kumalizika na kuongeza kuwa kwenye mikutano hiyo miwili nchi itahitaji angalau magari 1,200 kusafirisha wajumbe.

“Magari tunayolenga kuyatumia ni yale ya mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi na maofisa wote wenye haki,” amesema Bagiire akiwa kwenye hafla ambayo Serikali ya China imekabidhi magari 70 kwenye Shirika la Michezo la Uganda kwa ajili ya matumizi wakati wa mikutano hiyo.

Wajumbe kutoka mataifa 120 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa NAM, huku nchi 134 zikitarajiwa kwenye mkutano wa pili.

“Pamoja na magari 70 kutoka China, Serikali imenunua magari 30 ya aina hiyo ambayo yatawasili nchini kabla ya mwisho wa mwezi,” amesema.

“Kuhusu maandalizi, nchi ipo tayari kuandaa mikutano yote miwili katika usafiri, tuna magari mengine ambayo yako katika wizara na idara. Magari haya yote kama nilivyosema yatarejeshwa kutumika kwa siku 10 zaidi ambazo mikutano hiyo itafanyika,” amesema.

Vuguvugu lisilofungamana na upande wowote, lililoanzishwa mwaka 1961 katika kilele cha Vita Baridi kati ya nchi za kambi ya Magharibi na Mashariki, lina wanachama wa nchi 120; 53 kutoka Afrika, 39 kutoka Asia, 26 kutoka Amerika ya Kusini na Caribbean na wawili kutoka Ulaya.

Huu ni moja ya mikutano mikubwa zaidi ya kimataifa ambayo Uganda inaandaa baada ya Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola mwaka 2007.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi