Connect with us

Kitaifa

Kizungumkuti nauli mpya za daladala

Dar es Salaaam. Kutokuwepo kwa tiketi mpya, chati ya nauli mpya na kutobadilishwa kwa maelezo ubavuni mwa daladala, kumeibua malalamiko kutoka kwa abiria, ikiwa ni siku ya pili ya utozwaji wa nauli mpya.

Ongezeko la nauli lilitangazwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Novemba 27, 2023 baada ya kupokea maombi kutoka kwa wasafirishaji ya kufanya hivyo kwa kile walichoeleza kupanda kwa gharama za uendeshaji, ikiwemo mafuta na bei za vipuri vinavyouzwa kwa dola.

Kwa mujibu wa Latra, daladala za masafa yasiyozidi kilomita 10 nauli itapanda kutoka Sh500 hadi Sh600, ruti ya kilomita 11 hadi 15 nauli itaongezeka kutoka Sh550 hadi Sh700 na ruti ya kilomita 16 hadi 20 nauli itaongezeka kutoka Sh600 hadi Sh800.

Maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam jana kulikuwa na malalamiko ya abiria, huku baadhi wakikataa kulipa nauli hizo kwa kile walichodai hakuna tangazo lolote kwenye daladala linaloonyesha kuna ongezeko la nauli.

Mmoja wa abiria kwenye magari yanayofanya safari kati ya Makumbusho-Mbezi, alisikika akisema, “Mimi nauli kwenda Mbezi najua ni Sh500, hiyo Sh650 umesema wewe, silipi nakwambia.”

Abiria mwingine aliyepanda gari za Gongolambo-Simu 2000 aliyejitambulisha kwa jina moja la Agripina, alisema hakuamini kama nauli imepanda mpaka pale alipoona imeandikwa kwenye ubavu, japo alieleza magari mengine bado hawajafanya hivyo.

Naye Maneno Sufiani, alisema hawana shida ya kulipa nauli, lakini daladala nyingi bado zinatumia risiti za bei ya zamani na hapo ndipo mikwaruzano na makondakta inapoanzia.

Kwa upande wake, kondakta wa daladala zinazofanya safari kati ya Mbezi -Mbagala, Joshua Lema alisema abiria zaidi ya saba wamelipa nauli mbele ya askari wa usalama barabarani kwa kuwa kila wakiwaambia kuwa nauli zimepanda hawakuamini, hivyo kulipeleka gari kwa askari hao.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dara es Salaam (Darcoboa), Kifaya Lema alisema wamepokea mabadiliko hayo ya nauli kwa mikono miwili, japokuwa alikiri hata baadhi ya makondakta hawakuwa na taarifa.

Kwa mujibu wa katibu huyo, kuandika bei za nauli Veta ni Sh25,000 lakini wakiandika kwa watu wa mtaani ni Sh2,500 mpaka Sh3,000.

Akizungumzia malalamiko ya kutokuwepo kwa chati za nauli mpya, Mkurugenzi wa Latra, Johansen Kahatano alisema kati ya jana jioni au leo chati za nauli zitakuwa tayari zimewekwa kwenye mabasi.

Pia amewataka wamiliki wa daladala kuandika nauli mpya ubavuni kabla ya Desemba 15.

Wakati Latra ikitoa maelezo hayo, Mwananchi imeshuhudia baadhi ya watu wakitumia fursa kwa kuchapisha chati hizo, hasa kwa daladala ambazo kila moja huuza Sh500.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi