Kitaifa
Ubunifu DIT: Sh100 inakupa saa mbili za kuperuzi mtandaoni
Dar es Salaam. Wanafunzi wa Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) wamebuni vifaa na mfumo wa kutoa unafuu wa matumizi ya intaneti pamoja na kuzuia upotevu wa maji.
Ubunifu huo unalenga kuisaidia jamii kupunguza matumizi mabaya na kuzuia upotevu wa maji kutokana na kuharibika miundombinu.
Pia mfumo huo utawezesha matumizi kidogo ya fedha kwa ajili ya huduma ya intaneti.
Maelezo ya matumizi ya vifaa na mifumo hiyo yametolewa jana Desemba 6, 2023 katika maonyesho ya teknolojia chuoni hapo yanayolenga ubunifu wenye kutatua changamoto katika maisha ya kila siku ya wananchi.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili wa masuala ya elektroniki na mawasiliano ya anga, Joshua Gilbert amesema kwa kushirikiana na wenzake wamebuni mashine yenye mfumo wa kurahisisha upatikanaji wa intaneti kwa bei nafuu, itakayomwezesha mtumiaji kupakua nyaraka kwa urahisi kwa kutumia kiwango kidogo cha fedha.
“Mashine hii tunaunganisha intaneti kwa gharama nafuu inayoanzia Sh100 ambayo inatoa saa mbili za kuperuzi. Imekuwa kivutio cha wengi katika eneo la chuo,” amesema Gilbert.
Amesema baada ya maonyesho, mpango uliopo ni kwa uongozi wa chuo kuangalia iwapo mfumo huo unaweza kutumika katika maeneo mengine nje ya chuo hicho.
Gilbert amesema mfumo huo una uwezo wa kutumika kwenye simu na kompyuta. Amesema uunganishaji wake unatumia muda mchache kuanzia sekunde 50 hadi dakika moja.
Amesema msukumo wa kubuni mfumo huo ni kutokana na changamoto ya bei kubwa ya bando ya intaneti kwa wanafunzi, huku fedha za mikopo wanazopata hazitoshelezi matumizi ya intaneti.
“Tulikaa na wenzangu baada ya kugundua kuwa tunatumia pesa nyingi kupakua nyaraka kwa ajili ya kazi za masomo ndipo tulipoamua kubuni mfumo huu unaoitwa bongonet,” amesema.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa masomo ya masuala ya mitambo, Othman Daz ametengeneza mfumo wa matumizi ya majisafi anaoamini utasaidia wakazi zaidi ya wawili kwenye nyumba za kupanga wanaotumia mita moja ya maji.
“Ili kuondoa kelele za watu kwenye nyumba zenye wapangaji wengi, mfumo huu unawafaa kwani utasaidia kila mmoja kufahamu matumizi yake ya maji kama ilivyo kwenye mfumo wa Luku kwa wale wanaotumia kila mmoja mita yake,” amesema Daz.
Amesema mfumo huo unatumia simu na una uwezo wa kutoa taarifa za uharibifu wa bomba kwa kutumwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwenye simu ya mhusika, hivyo kumwezesha kufanya ukarabati.
Amesema makadirio ya gharama ya kufungiwa mfumo yatategemea na mahitaji ya mteja.
Akizungumza wakati wa maonyesho hayo, Profesa Ezekiel Amri, Naibu Mkuu wa Taasisi ya Utafiti, Taaluma na Ushauri wa Kitaalamu wa DIT, amesema ubunifu unaofanywa na wanafunzi umekuwa chachu kwa kampuni na taasisi mbalimbali kushiriki katika utoaji wa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri, wakiwa na ubunifu wa kipekee.
“Tumekuwa tukihamasisha wanafunzi ili kuwa bora na kupata cheti, ni muhimu kufanya ubunifu utakaoshawishi taasisi kutoa tuzo na hata kumpa mwanafunzi fursa ya kuendelea kufanya kazi chuoni hapa,” amesema.
Profesa Peter Msofe, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amewataka wanafunzi kuruhusu fikra zao kufanya kazi zaidi ya ubunifu ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kufanya maisha kuwa rahisi katika kutafuta kipato.
“Kumetengenezwa mifumo ya gesi asilia si kwa bahati mbaya, bali kusaidia kubakiza pato la Taifa ndani na si kupeleka nje. Nimesikia kumebuniwa bajaj za umeme, hii itasaidia kuchangia fedha kwa Shirika la Umeme la Tanzania (Tanesco),” amesema Profesa Msofe.
Amesema, “Msiubanie ubunifu wenu, uleteni hadharani ili tuuchambue na kuutumia katika matumizi yenye kuleta manufaa kwa jamii zetu.”
Asha Zakaria, mkazi wa Mbagala aliyefika eneo hilo kwa ajili ya tuzo za wanafunzi bora amesema kuna haja ya Serikali kutumia vitu vinavyobuniwa na wanafunzi na kuviendeleza ili kupunguza gharama za kununua kutoka nje ya nchi.
“Kumekuwa na malalamiko kwa wananchi kila leo kuhusu matumizi mabaya ya fedha za Serikali kwa kununua mitambo ikiwamo ya maji ili kufanyiwa ukarabati wa mabomba,” amesema.
Amesema endapo ubunifu wa kuzuia upotevu wa maji ukizingatiwa, utasaidia wananchi na Serikali kufahamu sehemu yenye tatizo kwa kutumiwa ujumbe tofauti na utaratibu unaotumika sasa wa kupiga simu na kutumia muda mrefu kufika eneo la tukio.