Connect with us

Kitaifa

Serikali yatoa neno wanafunzi 226 kufeli ‘Samia Scholarship’

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiweka wazi sababu za kuendelea kukunjua makucha ili kukomesha wizi wa mitihani ya Taifa, pia imeweka bayana kuwa inakwenda kufanya tafiti mbili ikiwemo kuhusu wanafunzi zaidi ya 226 kudondoka ufadhili wa masomo wa Samia, maarufu kama Samia Scholarship).

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Novemba 30, 2023 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alipokuwa  akifungua maonyesho ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) yanayofanyika jijini hapa yanayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Profesa Mkenda amesema Serikali ilitoa ufadhili wa Samia Scholarship kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi, lakini baadhi walipofika chuo hawakufanya vizuri kwa kiwango kilichotarajiwa, jambo lililofanya watolewe na kurudishwa katika utaratibu wa wanafunzi wanaopewa mikopo.

“Hawa wote tunakwenda kuangalia wametoka shule gani, tunaaza kufanya utafiti, wewe si ndio ulikuwa mwanafunzi bora, huenda mazingira ya chuo yanaogopesha ni tofauti sana haya tunayoyajua. Kama hujafanya utafiti hauna haki ya kuzungumza, tutajaribu kufanya tathimini kujua waliwezaje kuwa bora lakini walipofika vyuo hawakufanya vizuri,”amesema.

Hili linakwenda kufanyika wakati ambapo wanafunzi zaidi ya 226 kati ya 640 ambao walinufaika na ufadhili huo katika awamu ya kwanza 2022/2023, wameondolewa katika ufadhili huo kutokana na kutofikia  kigezo cha GPA ya 3.8.

Mdondoko wa wanafunzi

Wakati asilimia 26.8 ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2017 wakishindwa kufikia mtihani wa darasa la saba mwaka 2023, Serikali imesema inakwenda kutafuta kiini cha mdondoko huo.

“Tumeangalia takwimu ya waliojisajili darasa la kwanza halafu wakafanya mtihani darasa la saba mwaka huu, tumepoteza wanafunzi katikati, ile idadi hairidhishi, tumeanza kuwatafuta na kuangalia nini kimetokea na kufanya tafiti, mikoa gani yenye tatizo na kwa nini,”amesema Waziri Mkenda.

Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za elimumsingi   (Best) ya mwaka 2017, wanafunzi milioni 1.8 waliandikishwa darasa la kwanza mwaka 2017 lakini Necta ilieleza kuwa waliofanya mtihani wa kumailiza elimu ya msingi walikuwa milioni 1.3.

Amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona walioandikishwa wanashindwa kumaliza elimu yao ya msingi na wanalo jukumu kama wizara  kumueleza Rais Samia Suluhu Hassan nini wanafanya kukabiliana na suala hilo.

Amesema ili kudhibiti mdondoko unaotokana na mimba shuleni,  wanafanya kampeni kubwa ya kuhamasisha watoto kujilinda ili wawe salama,  licha ya kuwapo kwa nafasi nyingine waliyopewa ya kurudi shule baada ya kujifungua.

Necta na udanganyifu

Aidha, akizungumza katika ufunguzi huo, Profesa Mkenda amesema Necta imekuwa chujio muhimu katika kusaidia kujua mwanafunzi anayepaswa kuendelea katika ngazi inayofuata baada ya kufanya mtihani wa taifa, hivyo ni vyema kuwapo kwa mazingira sawa ya upimaji.

Kauli hii inakuja ikiwa ni siku chache tangu Necta kuzifungia shule ya msingi Thwibhoki na Graiyaki kuwa vituo vya mitihani wa darasa la saba, kutokana kuthibitika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika Septemba 5 na 6 mwaka huu.

“Mmefanya kazi kubwa sana (Necta), katika jamii ambayo wanaamini kuiba mtihani ni fahari, lakini kwa miaka yote 50 tunajivunia nyie, ukiona wahandisi wanajenga majengo mazuri, madaktari hospitali basi ni tunda la Baraza la mitihani,”amesema Profesa Mkenda.

Amesema wanapiga vita na kulaani wizi wa mitihani kwa sababu unaweza kumpatia mtu nafasi kwa kuamini ana uwezo kumbe alipita kwa njia za wizi.

“Amepita kwa kuiba mitihani, wasifu na cheti chake kinakuwa kizuri unampa kazi kwa kuamini anaweza na anastahili kumbe siyo. Nalipongeza baraza la mitihani kwani walijua usipoziba ufa utajenga ukuta,” ameeleza.

Kwa upande wake,Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed amesema wanakusudia kuwa na upimaji unaolenga kubaini uwezo wa wanafunzi katika kufikiri na kutenda kwa pamoja ili watahiniwa wanaomaliza wawe wamejengwa kikamilifu.

“Baraza litaendelea kuboresha utahini katika ngazi zote za elimu ili upimaji unafanyika uendane na mabadiliko ya sera unaolenga kuwa na upimaji wa umahiri,” amesema Dk Mohamed.

Kuhusiana na  hilo, Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Hashim Komba amesema watakwenda kushirikiana na Necta  kudhibiti wizi wa mitihani, ili kupata watu waliopimwa katika vigezo vinavyotakiwa.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi