Makala
Usahihi vipimo UTI Serikali yakuna kichwa
Dodoma/Dar. Wakati dunia ikiendelea kupambana na ugonjwa wa Maambukizi katika Njia ya Mkojo (UTI) kutokana takwimu zake kuzidi kuongezeka siku hadi siku, bado majibu ya vipimo vya ugonjwa huo Tanzania yanaendelea kuwa kitendawili kwa wananchi wengi.
Takwimu za dunia zilizotolewa na Jarida la ‘Front Public Health’ mwaka 2022 zinaonyesha vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vimeongezeka mara 2.4 ndani ya miaka 29.
“Mwaka 2019 jumla ya kesi milioni 404.61 za wagonjwa wa UTI ziliripotiwa huku vifo vikiwa 236,790 na watu waliopata athari ikiwemo ya ulemavu walikuwa 520,200,”inaeleza ripoti hiyo.
Hata hivyo, imani ya baadhi ya wananchi kuhusiana na vipimo vya UTI ipo chini huku wengi wakiamini huenda ni vya kufikirika.
“Mimi binafsi siamini kama kuna UTI, maana kila anayekwenda kupima anakutwa nayo na unashangaa unaweza usitumie dawa lakini ukapona,”anasema Halima Nyasa mkazi wa Tandale Uzuri jijini Dar es Salaam, ambaye mara kadhaa anadai anakutwa na UTI huku hazioni dalili.
Si Halima pekee ana wasiwasi na vipimo hivyo, Christopher Sostenes, mkazi wa Mwenge Lufungira jijini Dar es Salaam naye anasimulia kuwa zaidi ya mara nne kila anapopima anakutwa na maambukizi hayo ya njia ya mkojo lakini hupona bila kutumia dawa.
“Sasa hivi unajua kila mtu akienda hospitali kupima unaambiwa una UTI kiukwel mimi siamini sana kwasababu, niomepima mara nne nimekutwa na UTI lakini napona bila kutumia dawa, nahisi vipimo vyao vina shida,”anasema.
Katika kutatua changamoto hiyo ya vipimo vya UTI, Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za kuzindua mwongozo wa matumizi ya vipimo vya maabara ikiwemo vya ugonjwa huo.
Mwongozo huo utawasimamia watoa huduma wa maabara kutoa majibu sahihi na kuwaongoza wananchi jinsi gani watapata huduma na majibu sahihi ya ugonjwa huo na kuepuka udanganyifu kama inavyodhaniwa kwenye jamii.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi, Wizara ya Afya, Gerald Mrema alipokuwa akijibu swali la Mwananchi Digital kuhusu kuwepo na majibu ya uongo juu ya vipimo vya UTI kama njia ya kujipatia kipato kwenye sehemu za kutolea huduma za afya.
Si mara ya kwanza Mwananchi kuripoti…
Hii si mara ya kwanza kwa Mwananchi kuripoti tatizo hilo ambapo, Agosti 15, 2022 lilifanya uchunguzi kwa kupeleka maji kama kipimo cha mkojo kwenye hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam kisha majibu yake kuonyesha maji hayo yana UTI.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Serikali wa kipindi hicho (Agosti 15, 2022), Dk Aifello Sichwale, alisema uwezekano wa kipimo kutoa majibu kinyume na uhalisia, unasababisha na moja kati ya mambo matatu ambayo ni mashine husika, vitendanishi na weledi wa mtaalamu husika.
“Kwa upande wa mashine inaweza kufanya hivyo kama imetumika kwa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo, maana matengenezo yanapaswa kufanywa kutokana na namna mashine inavyotumika,” alisema.
Alisisitiza kuwa jukumu la ubora wa mashine, vitendanishi na taaluma za wataalamu, linapaswa kufuatiliwa na waganga wakuu wa wilaya ama mkoa ilipo hospitali au kituo cha afya husika.
Kwa mujibu wa Dk Sichwale, katika kila robo ya mwaka, mganga wa wilaya au mkoa anatakiwa awe ametembelea vituo vilivyopo katika eneo lake walau mara moja.
“Hawa ndiyo wenye mamlaka ya kuhakikisha hospitali au vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao vinafanya kazi kwa kufuata miongozo ya Wizara ya Afya,” anasema Dk Sichwale. Alisema jukumu hilo hawapaswi kulitekeleza katika hospitali za umma pekee, bali hata binafsi wanatakiwa kufanya hivyo.
Kwanini mwongozo ni muarobaini
Mrema anasema mwongozo huo wa matumizi ya vipimo vya maabara utasaidia kuondoa fununu za wizi na udanganyifu kwa sababu watoa huduma wote watapaswa kuufuata.
“Wizara ya Afya kupitia huduma za uchunguzi wa maabara imejizatiti na hivi karibuni itatoa huo muongozo sahihi na hizo fununu, dalili zote zitaondoka kwa sababu tayari kuna muongozo ambao umeandaliwa.
“Mwongozo huo utatumika kwa ajili ya wataalam wanaofanya vipimo na wananchi wajue nini cha kufuata kama mwongozo huo unavyosema,” amesema Mrema.
Awali akizungumza katika mafunzo hayo ya viongozi chipukizi wa maabara yaliyofanyika jana Novemba 29, 2023, Mrema amewataka kuwa ni miongoni mwa wafanya utafiti wa afya na sio kuwaachia Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pekee.
Mrema amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha huduma za maabara zinasimamiwa vyema na kuleta ufanisi ili wagonjwa waweze kupata huduma sahihi za maabara.
“Baada ya uwekezaji mkubwa uliofanyika na Serikali ya awamu ya sita, inahitajika utaalamu wa kusimamia vifaa, kwahiyo tunapoongeza huduma ni lazima kuongeza ufanisi wa usimamizi wa hizo huduma ili ziwe bora na ziwafikie watu wote kuanzia ngazi ya zahanati hadi Taifa,” amesema.
Kwa upande wake mtaalamu wa maabara Wizara ya Afya, Reuben Mkala amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuimarisha huduma za maabara kuanzia ngazi ya zahanati hadi Taifa.
Reuben amesema mafunzo hayo wanayoyapata pia yataondoa dhana ya kutoa majibu ambayo hayaaminiki katika jamii.
Naye mtaalam wa maabara, Philipo Petro amesema ili kuepuka majibu yenye udanganyifu wataalamu wanapaswa kuhakikisha ubora wa vitendanishi na vifaa vyao kila mara na kujikita kujifunza teknolojia mpya.