Makala
Ripoti maalumu: Kwa nini wamachinga mfupa mgumu?
Dar es Salaam. Kuanzia saa 11 alfajiri ni jambo la kawaida katika mitaa ya Kariakoo, Manzese, Mwenge, Kimara Mwisho na Mbezi Mwisho jijini hapa, kukutana na wamachinga wakiuza bidhaa kando mwa barabara au kuzunguka nazo mtaani.
Jambo hili huwa kero kwa watumiaji wa barabara, hata wafanyabiashara wenye maduka ambao mara kadhaa hulalamika wamachinga huziba maeneo yao ya biashara. Ni nini kiini cha tatizo hili, kwa nini linaonekana kuwa mfupa mgumu kwa Serikali na mamlaka husika kulimaliza?
Raphael Kipisa, mmachinga eneo la Mwenge Mataa jijini Dar es Salaam kwa miaka 17, anasema sababu ya kufanya biashara kwa mtindo huo ni kile alichodai kuwa wateja wengi ni wavivu wa kufuata bidhaa dukani.
“Natokea Tandale, kila siku asubuhi huwa naenda soko la Karume kununua nguo. Huanza kuzitembeza mtaani kutafuta wateja maana watu wengi wanaonekana kuwa wavivu wa kufuata mahitaji yao sokoni,” anasema na kuongeza:
“Ikifika jioni bidhaa zangu nazipanga hapa chini (Mwenge sokoni) sababu Watanzania wengi hawapendi kupata shida ya kutafuta vitu ndani ya soko,”amesema.
Halima Nakapanya, mchuuzi wa soda na juisi katika stendi ya daladala Karume, Dar es Salaam anasema hufanya biashara hapo kutokana na wingi wa wateja.
“Hapa unajua ni kituoni, wateja lazima wapitie. Wakiona soda au maji hununua kwa sababu ni rahisi kwao,” amesema.
Ripoti za utafiti
Kauli za wachuuzi hawa zinaendana na majibu ya utafiti uliofanywa na wahandisi wa michoro ya ujenzi kutoka Sweden kwa ushirikiano na Chuo Kikuu Ardhi (Aru) mwaka 2013 ulioitwa ‘Vendors garole and more.’
“Tatizo la uwapo wa wamachinga wengi wanaofanya biashara katika maeneo ambayo si rasmi jijini Dar es Salaam linatokana na fikra zao, kuamini eneo lenye watu wengi ndipo biashara inafanyika kwa urahisi,” inasema sehemu ya utafiti huo na kuongeza:
“Ili tatizo la wamachinga kuzagaa maeneo yasiyo rasmi liishe wanatakiwa watafutiwe eneo la kutosha ambalo lina miundombinu sahihi na rahisi kufikika,”amesema.
Sara Boustedt na Nethalie Mair, walipendekeza hilo katika majibu ya utafiti huo uliochunguza soko la Kariakoo na Machinga Complex.
Utafiti mwingine uliofanywa na Constantine George wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) mwaka 2022 ulioitwa ‘Urasimishaji wa biashara za wamachinga Dar es Salaam’ ulibaini tatizo hilo kusababishwa na kiwango kidogo cha ushirikishwaji kwa wamachinga katika maamuzi ya Serikali.
“Sababu ya urasimishaji maeneo ya wamachinga kushindwa kufanikiwa ni pamoja na kiwango kidogo cha ushirikishwaji, jumuiya za wafanyabiashara zisizokuwa na meno na kushindwa kutekeleza sheria,” imesema sehemu ya utafiti huo.
Mtazamo wa wamachinga
Majibu ya utafiti wa George yanaungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Wamachinga Tanzania (Shiuma), Steven Lusinde ambaye amesema ushirikishwaji wa viongozi wa Serikali katika masuala yanayowahusu wamachinga ni mdogo.
Lusinde amesema, “Tatizo ni tafsiri ya maelekezo ya Rais, huku chini hawawezi kutafsiri hilo. Vema wahusika wakae na wakubaliane wanachokitaka, hataki purukushani lakini huku wanatafsiri kwamba watutafutie maeneo na si tukae chini pamoja tujadiliane.
“Tunakaa na viongozi kama ‘bosheni’ lakini mwisho wa siku tunapangiwa tu nenda kule, ndiyo maana unaziona hizo purukushani,” amesema.
Akijibu kuhusu hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, amesema huo ni uzembe wa viongozi wa maeneo husika kwa kuwa utaratibu unawataka kukaa na makundi hayo kujadili.
“Jukumu la Serikali katika ngazi ya mkoa ni kutatua matatizo ya watu wa eneo hilo, wakuu wa maeneo husika wana vikao vyao katika Serikali za mitaa kama kuna changamoto katika mkoa wowote, viongozi wanawajibika kwa sababu walitakiwa kukaa na watu wao kupanga,” amesema.
Lusinde amesema suala lingine linalokwamisha urasimishaji wa wamachinga ni ujenzi na upangaji wa masoko usiozingatia mahitaji yao.
“Viongozi hawataki kusikia wahitaji wanachokihitaji, wamachinga mtaji wetu tunatafuta fedha ya siku moja, ndiyo maana tunahitaji mzunguko wa watu, hivyo Serikali ijenge masoko kwenye mizunguko ya watu,” amesema.
Akizungumzia ujenzi wa masoko, Waziri Mchengerwa amesema Desemba 10, 2023 watasaini mkataba na washauri elekezi watakaoishauri Serikali maeneo ya kujenga masoko hayo, ili yawe na tija kwa wafanyabiashara wa ngazi zote.
“Katika masoko mengine, programu ya uboreshaji tunayokwenda kuizindua Desemba 10 itatusaidia kupata suluhu ya changamoto hiyo,” amesema.
Waziri Mchengerwa amesema, “Lengo letu ni kupata masoko bora yatakayowanufaisha wafanyabiashara wakubwa, wakati na wadogo, pia itaenda kutatua kero ya wamachinga ya muda mrefu.
Kuhusu urasimishaji wamachinga katika masoko makubwa hususani Kariakoo, Mchengerwa amesema, “Kupitia ukarabati wa Soko Kuu la Kariakoo kila mmachinga atapata nafasi ya kuuza ndani, hawa wafanyabiashara wote waliokuwa nje tutahakikisha wanapata vizimba pale Kariakoo.
Hata hivyo, George katika utafiti wake kuhusu suluhu ya urasimishaji wa wamachinga ameshauri, “Mfumo rafiki wa ufanyaji biashara wa wamachinga na kuwa na utozaji mzuri na halali wa ulipishwaji faini kwa wanaokiuka sheria.
Je, wanatokea wapi?
Mwandishi alipiga kambi maeneo ambayo wamachinga wanafanya biashara jijini Dar es Salaam. Katika hali ya kushangaza sura za watoto wadogo zimejaa, huku wakichakarika kusaka wateja.
Napata shauku ya kumfuata mmoja, ambaye ananieleza anaitwa Joseph Julius (si jina halisi) mwenye miaka 11. Ni mkazi wa Kigoma aliyekuja Dar es Salaam kwa lengo kutafuta kazi.
“Nimekuja mwaka jana (2022), braza (kaka) ndiye kanileta kutoka Kigoma, hapa tunauza mifuko na matunda. Kule niliacha shule nikaamua nije huku,” amesimulia.
Simulizi ya Julius inanifanya nidadisi zaidi kwa kumuuliza mtoto mwingine anayejitambulisha kwa jina la Hamduni (si jina halisi), aliye eneo jirani na stendi ya daladala Karume. Anasema anatokea Geita na lengo lake la kuja Dar es Salaam ni kutafuta maisha.
“Nilitoroka nyumbani Chato (Mkoa wa Geita) nikaamua nije huku nifanye biashara kwa sababu kuna wenzetu walikuja sasa hivi wana biashara zao,” anasema kijana huyo ambaye umri wake ni miaka 17 kwa makadirio.
Kauli za watoto hao waliojitosa katika umachinga eneo la Kariakoo zinaakisi vitu viwili: Kwanza, uhamiaji wa watu kutoka vijijini kuja mijini kutafuta ajira. Pili, tatizo la watoto kuacha shule kukimbilia mijini kutafuta ajira.
Watoto hao wananipa shauku ya kuangalia takwimu za uachaji shule katika mikoa wanayotoka ambazo zinaakisi wanachokisema, kwani mikoa hiyo ni vinara wanafunzi wa shule za msingi kuacha shule.
“Mkoa wa Geita unaongoza kwa watoto kuacha shule ya msingi, ambapo watoto 21,596 waliacha shule mwaka 2022, huku Mkoa wa Kigoma ukishika nafasi ya nane ambapo wanafunzi 10,355 waliacha shule mwaka huo,”inabainisha ripoti ya BEST inayotolewa na Wizara ya Tamisemi.
Mwanaisha Kondo, mtaalamu wa maendeleo ya jamii anasema watu kuhamia mijini kunatokana na fikra zao kuwa huenda mjini kuna maisha mazuri. Anasema suala hilo linachangiwa na sera za maendeleo zinazowaacha nyuma watu wa vijijini.
“Kuna utafiti uliwahi kufanywa na Athumani Liviga kuhusu tatizo hilo, unaitwa ‘Kuhama kwa vijana vijijini sababu ya umasikini.’ Aliwahoji wamachinga, utafiti ulibaini kuongezeka kwao maeneo ya mijini kunasababishwa na sera za Serikali kutoakisi maendeleo ya vijijini na kuwafanya wabaki huko,” anasema.
Hoja ya Mwanaisha inaungwa mkono na takwimu za Taasisi ya Utafiti ya Repoa kupitia ripoti yake inayoitwa ‘Mabadiliko ya Miji Tanzania’ ya mwaka 2022 inayoonyesha uhamiaji wa watu mijini kila mwaka nchini unaongezeka kwa kiwango cha asilimia 5.2.
“Kiwango hicho kinatokana na wengi kuamini mjini kuna ajira za kutosha. Hadi mwaka 2030 takribani watu milioni 35.5 watakuwa wamehamia mijini, huku mwaka 2050 makadirio yanaonyesha watu milioni 76.5 watakuwa wapo mijini,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Matokeo ya utafiti wa Repoa pia yalionyesha watu wenye kipato cha chini, wasio na elimu na wanawake ndio wanaongoza kuhamia Dar es Salaam kutafuta ajira.
Mbali na utafiti wa Repoa, ripoti ya ‘Tanzania in figures 2022’ inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha eneo linalokimbiliwa na wengi (mijini) kiwango cha ukosefu wa ajira ni kikubwa zaidi.
“Kiwango cha ukosefu wa ajira jijini Dar es Salaam ni asilimia 20.5, miji mingine ni asilimia 9.9, huku vijijini hali ikiwa chini zaidi ambayo ni asilimia 7.2,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Takwimu hizo zinamaanisha katika kila watu watano wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, mmoja hana ajira, huku katika kila wakazi 10 wa miji mingine mmoja hana ajira.
Hata hivyo, katika sekta binafsi, wamachinga wakiwamo idadi ya ajira zinazotengenezwa zinazidi kuongezeka kutoka 275,905 mwaka 2021 hadi ajira 286,665 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 3.9.
Ili kudhibiti wimbi la nguvu kazi kubwa kuhamia mjini, Mwanaisha ameshauri kuwekeza katika elimu ya amali na vitendo kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla.
“Ili wananchi wajione salama kuendelea kubakia vijijini na kuzalisha mali, lazima mfumo wetu wa elimu uwape ujuzi hasa ule adimu ambao wanaweza kujiajiri wenyewe kule waliko,” amesema.
Utoro shuleni
Alichoshuhudia mwandishi kuhusu watoto kuacha shule ili kufanya biashara ndogondogo na kutafuta ajira, kinaelezwa katika takwimu za uachaji shule kwa wanafunzi ambao umeongezeka takribani mara mbili zaidi mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2017.
Ripoti ya Best 2022 inayotolewa na Wizara ya Tamisemi inaeleza: “Jumla ya wanafunzi 329,918 waliacha shule nchini mwaka 2022, kati yao wavulana ni asilimia 55.2 na wasichana ni asilimia 44.8. Mwaka 2017 walioacha shule walikuwa 131,842 sawa na ongezeko la asilimia 150.”
Ripoti hiyo pia imesema walioacha shule ya msingi walikuwa 193,605 mwaka 2022 wakiongezeka kutoka 66,142 mwaka 2017. Kwa upande wa sekondari walikuwa 136,313 mwaka 2022 wakiongezeka kutoka 65,700 mwaka 2017.
Kimbilio la wengi
“Juzi hapa wamefanya mtihani watoto wa darasa la saba, walioshindwa kufaulu wanaenda wapi? Kwa hiyo lazima Serikali ituangalie wamachinga kwa sababu ni mbadala wa ajira kwa wengi,” amesema. Lusinde anayekiri wengi wanaoshindwa kuendelea na masomo na hata wahitimu kimbilio lao ni kujiajiri kupitia umachinga.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Neec), Profesa Aurelia Kamuzora amesema ili kupunguza ukosefu wa ajira wamachinga wakiboreshewa mazingira na sera watakuwa kimbilio la kundi hilo.
“Huko ndiko tunakohimiza vijana waende kufanya biashara wajiajiri kupunguza ukosefu wa ajira. Inatakiwa tujiulize kwa namna gani hawa wanakuwa na mazingira mazuri ili waongeze tija katika uchumi,” amesema.
Teknolojia suluhisho
Ili kuondoa msongamano wa wamachinga barabarani, Profesa Kamuzora ameshauri teknolojia itumike kukutana na wateja wao na wanunuzi wafanye hivyo kupitia mtandao na si kufuata bidhaa sokoni.
“Kuwe na sera itakayomuondoa mmachinga kwa hiari, ikiwamo ununuzi wa kieletroniki. Tuache kutumia nguvu kuwapanga,” amesema Profesa Kamuzora, mchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Neec.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Tehama Tanzania, Dk Kundwe Mwasaga amesema wataanza kutoa elimu ya matumizi ya mifumo hiyo ili kurahisisha biashara.
“Serikali tuna programu ya mapinduzi ya kidijitali, tunaangalia skills (ujuzi). Wamachinga wanatakiwa wapewe elimu ya matumizi ya mitandao na mifumo, pia kuhakikisha inakuwa salama kwa ajili ya matumizi yao kibiashara,” amesema na Kuongeza:
“Tunawahamasisha vijana waliopo katika teknolojia kutumia ubunifu kutengeneza mifumo itakayowasaidia wamachinga kutatua changamoto zao,”amesema.
Vitambulisho viboreshwe
Faudhia Bakari, mfanyabiashara pembezoni mwa barabara eneo la Manzese Darajani, jijini Dar es Salaam, amependekeza mfumo wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo uboreshwe.
“Vitambulisho vilikuwa suluhu endapo wangetuonyesha sehemu nzuri yenye watu wengi ya kufanyia biashara. Ila sasa utaratibu ni mbaya kila sehemu tunakimbizwa,” amesema.
Machi 2018 mfumo wa utoaji vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wasio kwenye sekta rasmi, wakiwamo wamachinga ulianza lengo likiwa kuwatambua. Walikuwa wakilipia Sh20,000 kwa mwaka.
Kitambulisho cha mjasiriamali mdogo kilikuwa kikitolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi kwa ajili ya matumizi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Makamu Mwenyekiti wa Shiuma, Lusinde ameshauri wamachinga washirikishwe katika utungwaji sheria ndogondogo za halmashauri na majiji.
“Sheria zinazotumika ni zile za halmashauri ambazo mara nyingi si rafiki kwetu… ni zile zile ambazo ni toka, ondoka. Hakuna inayotupa nafasi ya cha kufanya endapo umetendewa vibaya, ushirikishwaji haupo katika utungaji sheria, ili tulimalize hili kwa pamoja tushirikishwe,” amesema.
Matamko ya kisiasa
Kutokana na mkwamo wa urasimishaji maeneo ya kufanyia biashara wamachinga, wadau wa sekta hiyo wanadai jambo hilo linakuwa gumu kufika tamati kutokana na kauli za kisiasa zinazotolewa kwa nyakati tofauti.
“Inatakiwa tuwe na sera zinazoakisi suala la kitaifa na si mtu mmojammoja. Kila anayekuja madarakani anakuja na mambo yake ndiyo maana tunajikuta tunabaki hapahapa,” anasema Lusinde.
Kauli hiyo inashabihiana na majibu ya utafiti wa George wa mwaka 2022 unaoeleza: “Tatizo la urasimishaji biashara za wamachinga linachagizwa na wanasiasa wanaotumia suala hilo kama mtaji kisiasa.
Hili linajidhihirisha katika awamu mbili tofauti za utawala, awamu ya tano na ya sita ambazo zimekuwa na njia tofauti za kushughulikia suala hilo.
Oktoba 24, 2021 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua kongamano la tano la Neec aliwaagiza wakuu wa mikoa kuzisimamia halmashauri ili zitenge maeneo ya wamachinga kufanya kazi ambayo yana mwingiliano wa watu.
“Tumeagiza halmashauri kuhakikisha wanatenga maeneo mazuri ya biashara kwa wamachinga ambayo yanafikika na wateja kwa urahisi,” aliagiza.
Agizo hilo halikuwa mara ya kwanza kutolewa na viongozi wa juu, liliwahi kutolewa na Rais John Magufuli na hata Rais aliye madarakani sasa, Samia Suluhu Hassan.
Mwandishi alifika maeneo maalumu yaliyotengwa na halmashauri kwa ajili ya wamachinga, ambayo kwa kiasi kikubwa yamebaki tupu kutokana na wamachinga kutotaka kuyatumia.
Miongoni mwa hayo ni Machinga Complex. Othman Liemba, mfanyabiashara eneo la Karume amesema wengi hawalitumii kutokana na kuwa mbali na msongamano wa watu.
“Limekaa sehemu mbaya, pale hakuna watu pia ukienda kutaka kizimba unapata vya juu ambavyo kupata wateja ni ngumu,” anasema.
Mwaka 2016, Rais Magufuli alitoa agizo wamachinga wasisumbuliwe hadi watakapowekewa mazingira mazuri ya biashara.
“Naomba niagize wamachinga wasisumbuliwe mpaka watakapotengenezewa utaratibu na maeneo ya kufanyia biashara zao,” aliwahi kunukuliwa akiagiza hayati Magufuli.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla Novemba 23, 2021 kupitia kampeni ya pendezesha, safisha Dar es Salaam alisema asilimia 90 ya wamachinga wamewapanga katika maeneo rasmi ya biashara.
“Dar es Salaam tumefanikiwa kwa asilimia 90 kuwaondoa wamachinga kwenye maeneo wasiyotakiwa, viongozi wao ndio waliosaidia kufanikisha hili,” amesema Makalla.
Hata hivyo, wamachinga wamerejea katika maeneo yasiyoruhusiwa, huku wakikimbizwa mara kwa mara na mgambo wa jiji.