Kitaifa
Chalamila aibuka na operesheni panyarodi waibuka upya
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameanzisha operesheni ya kimyakimya ya kukabiliana na vikundi vya kihalifu vijulikanavyo kwa jina la panyarodi.
Akizungumza jana wakati wa kusikiliza kero za wananchi katika Kata ya Chanika, Chalamia alisema operesheni hiyo itafanyika kwa baadhi ya maeneo, hususani Chanika na Zingiziwa.
“Tumefanya utafiti wenye taarifa za kutosha maeneo yenye vijana wengi wa panyarodi, vijana wengi wadokozi wanatoka Zingiziwa na Chanika.
“Ngoja niendelee kusisitiza, hapa kuna wazazi naomba niwaeleze ukweli, kiwango cha uvumilivu wetu kimetosha. Naweza kumvumilia anayemtukana mkuu wa mkoa, lakini kitendo cha kushika panga kuingia kwenye nyumba ya mtu na kumkata, jambo hilo linaweza kukurudia kama ulivyofanya,” alisema aliyeambatana na Kamati ya Ulinzi ya mkoa huo.
Vikundi vya panyarodi vinavyohusisha vijana wadogo wanaotumia mapanga, visu na nondo, vimepata umaarufu miaka ya hivi karibuni, kwa kufanya matukio ya uporaji wa mali, kujeruhi na wakati mwingine kuua watu.
Matukio ya vikundi hivyo kuvamia makazi ya watu vimekuwa vikijirudia kwa nyakati tofauti, licha ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuanzisha misako ya mara kwa mara.
Akisisitiza kuhusu, operesheni hiyo, Chalamila alisema hawezi kuvumilia baadhi ya watu kujiita ‘jeshi la kujitegemea’ na kuendesha uhalifu.
Aliwaomba wazazi kuendesha mapambano dhidi ya wahalifu hao.
“Tumegundua ukimchekea nyani utavuna mabua, tumegundua ukionyesha upole na utulivu wanatufanya wajinga na inaonyesha kila nikirejerea ya haki ya binadamu ni lile tendo alilolifanya, kama biblia inasema aliyeua kwa upanga atauliwa kwa upanga, mimi nasema aliyeua kwa upanga atajijua baadaye,” alisema.
Alisimulia tukio la uhalifu lililokabiliwa na wananchi na kusababisha mauaji ya mmoja wa wahalifu ambaye hakumtaja jina katika eneo la Vingunguti, akisema walibaini mtu huyo ametokea Chanika.
Alisema baada ya kuuawa, wenzake walitoka maeneo ya Chanika kwenda kuleta fujo kwenye eneo hilo wakihoji kwa nini mwenzao ambaye ni mwandamizi kauawa, lakini wananchi waliwakabili.
Alisema kupitia operesheni hiyo wamedhamiria pia kuijenga Dar es Salaam salama ikiwa ni pamoja na kubomoa na kuteketeza ngome za madanguro yote.
“Leo, (jana) Dar es Salaam katika nchi nzima inaongoza kwa uwekezaji mkubwa wa madanguro, watoto wetu wanakwenda si kwa sababu wana shida, ndiyo maana nimeanzisha operesheni ya kuyabomoa na atakayepiga kelele nitampeleka mahakamani,” alisema.
Alisema Serikali haiwezi kuvumilia na kuilea miradi haramu, hivyo ameenda kubomoa mwenyewe na mwenye uhuru ampeleke mahakamani kwa jina lake ili apambane naye.
“Wazazi mkiona madanguro mnacheka na hatuwezi kujenga taifa ambalo uwekezaji mkubwa ni madanguro, lazima tupige kelele,” alisema,
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Gogo, Hamad Keto alisema vikundi vya panyarodi vina mtandao mkubwa ndani ya mkoa na vimekuwa vikibadilishana taarifa.
“Operesheni hiyo ya kimyakimya inaweza kusaidia kwa kuwa kuna baadhi ya vijiwe vinafahamika na inatakiwa ifanyike mchana na usiku,” alisema.
Wavamia Chamazi
Wakati huohuo, katika eneo la Chamazi, Mbande jijini Dar es Salaam limeibuka kundi la uhalifu linalotumia pikipiki kwa kuzingurumisha eneo wanakofanya uhalifu wa kuvunja na kuiba.
Tukio hilo la limetokea usiku wa kuamkia Jumamosi eneo la Kiponza, Kata ya Chamazi, vijana waliokuwa na pikipiki tatu walikata makufuli katika dula la vinywaji liitwalo Kigo Pub na kuchukua mauzo ya siku hiyo, runinga, mashine ya michezo ya kubahatisha (dubwi) na redio ya sub-woofer.
Shuhuda wa tukio hilo, Linah Mathias alisema kundi hilo lilivamia muda wa saa 8 usiku na kuanza kuungurumisha pikipiki, zingine zikienda na kurudi huku wenzao wakivunja na kupakia mizigo.
“Kama si kupiga yowe huenda wangebeba kila kitu kwa sababu, walikuwa ni kundi kubwa la vijana waliokuwa na silaha,” alisema Linah.
Shuhuda wa tukio hilo, Goodlove Musa alisema alilazimika kumsindikiza mke wake anayefanya kazi Mbezi ili awahi kwenye majukumu yake.
Alisema akiwa anarudi kutoka kituo basi cha Mbande, aliamua kuchukua pikipiki, hata hivyo walikutana na kundi hilo njiani likiwa na silaha mkononi ambazo ni mapanga, visu na bisibisi ndefu.
“Baada ya kunusurika na kundi hilo, niliamua kuwajulisha majirani ili wachukue tahadhari iwapo wanawahi kuamka kwenda kazini,” alisema.
Alisema muda wa saa kumi na moja vijana wawili waliokuwa na silaha na wakitumia bodaboda, walimvamia jirani anayefahamika kama Mama Hadija na kumnyang’anya pochi yake na simu.
Jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke hakupatikana kuzungumzia matukio hayo, baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.