Makala
Ndoa ya wanaharakati, upinzani yavunjika rasmi
* Mwabukusi awaponda upinzani, asema ni wabaya kuliko watawala
* Maria Sarungi, CHADEMA wararuana kwenye mitandao
* Jitihada za kuwapatanisha Mbowe na Lissu zakwama
Waandishi Wetu, Dar es Salaam
UPINZANI kumoto. Hayo ni maneno mawili yanayoweza kuelezea hali halisi kwenye vyama vya upinzani nchini, hususan CHADEMA ambacho kimejipambanua kama chama kikuu cha upinzani Tanzania bara.
CHADEMA tayari imemeguka vipande viwili. Kuna kundi la Mwenyekiti Freeman Mbowe na kundi la Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu.
Makundi haya mawili hasimu yameibuka kutokana na mgogoro wa madaraka na maslahi fedha ndani ya chama.
Kundi la Lissu linadai kuwa Mbowe na Katibu Mkuu John Mnyika wamekosa uwazi kuhusu mapato na matumizi ya chama, ikiwemo pesa za ruzuku, michango ya wanachama na misaada kutoka nje.
Kundi la Lissu pia linataka mwanasiasa huyo machachari, ambaye hutumia muda wake mwingi nje ya nchi alikoanzisha maisha mapya, awe mgombea Urais wa CHADEMA kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, licha ya kutofanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu wa 2020.
Kundi hilo la Lissu pia linapinga siasa za maridhiano za Mbowe na linataka kuanzisha siasa za uanaharakati za uhasama za maandamano bila ukomo ili kuleta machafuko ya kisiasa nchini waweze kupata misaada ya fedha kutoka nchi za Magharibi.
Kundi la Lissu linataka Mbowe aachie uenyekiti wa CHADEMA ampe Lissu, baada ya Mbowe kushikilia nafasi hiyo kwa karibu miaka 20.
Kwa upande mwingine, kundi la Mbowe linataka Mwenyekiti huyo agombee urais 2025, ikiwa ni miaka 20 tangu alipogombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 2005 dhidi ya Jakaya Kikwete wa CCM.
Kambi ya Mbowe inaamini kuwa sasa umaarufu wake umeongezeka zaidi na anaweza kuleta ushindani mkubwa kwa Rais Samia kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2025 kuliko Lissu, ambaye muda mwingi yuko nje ya nchi.
Mbowe, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 61, inaonekana kuwa uchaguzi mkuu wa 2025 ndiyo kiumri itakuwa nafasi yake ya mwisho kuweza kugombea urais. Lissu kwa sasa ana miaka 55, hivyo anaweza kusubiri hadi 2030 agombee tena urais akiwa na miaka 62.
Lakini Timu Lissu haitaku kusubiri, kwani wanaamini kuwa Lissu ndiyo anayestahili kugombea urais tena 2025.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA hivi karibuni walifanya kikao nyumbani kwa Mbowe, Machame Moshi, kwa lengo la kumpatanisha na Lissu, lakini mkutano huo haukuzaa matunda.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mbowe, Lissu, Godbless Lema, Ezekiah Wenje, Peter Msigwa na John Heche na wakaishia kupiga picha za kikao na kuzisambaza kwenye mitandao ya jamii.
“Hawa viongozi wetu wanachekeana tu hadharani na kusema hakuna mgogoro, lakini ukweli usiofichika ni kuwa CHADEMA imepasuka kwenye vipande viwili hasimu vya Timu Mbowe na Timu Lissu,” alisema mwanachama mmoja wa CHADEMA.
Wakati huo huo, ndoa ya CHADEMA na wanaharakati ya kupigania Katiba Mpya imevunjika rasmi baada ya pande hizo mbili kutofautiana hadharani.
Upande wa wanaharakati, ambao unamjumuisha Balozi Wilbrod Slaa, mwanasheria Boniface Mwabukusi na mwanaharakati Maria Sarungi, umetengana na CHADEMA baada ya ushirikiano uliodumu muda mfupi.
Kwa sasa CHADEMA inapigania Katiba Mpya kivyake na wanaharakati nao wanapigania kivyao kwenye mgogoro wa maslahi wa kila upande kutaka uongoze kampeni hiyo ili upate kuungwa mkono na wananchi na upate pesa za wafadhili.
Hivi karibuni, makada maarufu wa CHADEMA, akiwemo Martin Maranja Masese, wamekuwa wanarushiana maneno makali kwenye mitandao ya jamii na Maria Sarungi, huku kila upande ukigombania uhalali wa kuongoza harakati za kudai Katiba Mpya.
Naye Mwabukusi wiki hii ameushambulia upinzani nchini kuhusu mkakati wao wa kudai Katiba Mpya.
“Huku upinzani nako kuna machawa huku kwetu kwenye upinzani, hakuna mtu yuko tayari kumwambia kiongozi wake kwamba anayoyafanya hayako sawa, hatuna hata mgambo,” alisema Mwabukusi.
“Nakuhakikishia sisi wapinzani ni wabaya kuliko hawa walioko madarakani, tunaogopana kuambiana ukweli.”
Mwabukusi aliwakosoa upinzani kwa kushindwa kuonesha msimamo kwenye suala la Katiba Mpya na kuwataka wasusie uchaguzi bila katiba mpya.
“Nilishasema kuna biashara ya demokrasia inafanyika hapa nchini” Mwabukusi alisisitiza.