Connect with us

Kitaifa

Samia aishawishi Denmark isifunge ubalozi wake Tanzania

Denmark yatangaza kufuta uamuzi wa kufunga ubalozi wake Tanzania mwaka 2024

Uamuzi huo ni matokeo ya Rais Samia kuimarisha diplomasia ya Tanzania

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali ya Denmark imetangaza kufuta uamuzi wake wa kufunga ubalozi wake nchini Tanzania, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kurejesha mahusiano mazuri kati ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa.

Denmark ilitangaza mwaka 2021 kuwa itafunga ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 2024 kuendana na mwelekeo mpya wa sera yake ya mambo ya nje.

Uamuzi huo wa Denmark wa kufunga ubalozi wake nchini ulikuja wakati uhusiano wa Serikali ya wakati huo ya Tanzania ya Awamu ya 5 na mataifa ya nje pamoja na mashirika ya kimataifa ukiwa umeyumba.

Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia amefanya kazi kubwa kuimarisha uhusiano wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa, ikiwemo kurejesha mahusiano mazuri ya kihistoria kati ya Tanzania na Denmark yaliyodumu kwa miaka 60.

“Leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Løkke Rasmussen, ametangaza kuwa Denmark itabakisha ubalozi wake nchini Tanzania,” Ubalozi wa Denmark jijini Dar es Salaam ulisema kwenye taarifa yake leo.

Ukiacha mahusiano ya kidiplomasia, Denmark ni mmoja wa washirika wakuu wa maendeleo wa Tanzania, chanzo kikubwa cha uwekezaji na watalii.

Wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wanasema kuwa uamuzi wa Denmark kubakisha ubalozi wake nchini ni matokeo ya ushawishi mkubwa wa diplomasia aliokua nao Samia.

Rais Samia ameweka jitihada kubwa kwenye masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa na kuifanya Tanzania ing’are duniani kwenye miaka mitatu kasoro ya uongozi wake.

Rais amevutia viongozi wengi wakubwa duniani, ikiwemo Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, kufanya ziara nchini Tanzania.

Samia pia amealikwa kwenye ziara za kitaifa kwenye nchi nyingi na kuhudhuria mikutano mikubwa ya kimataifa ambayo ameitumia kwa ufanisi kusukuma ajenda ya Diplomasia ya Uchumi.

Hivi karibuni, Rais Samia ameongoza kampeni ya kimataifa kuhakikisha kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, anachaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na hivyo kuleta heshima kubwa kwa Tanzania.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi