Connect with us

Kitaifa

Sh337 bilioni kujenga, kukarabati miundombinu ya barabara Kagera

Mwanza. Serikali imepanga kutumia zaidi ya Sh337 bilioni kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Kagera.

Pamoja na kuhakikisha mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1,966.29 zinazohudumiwa na Wakala ya Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Kagera unapitika kwa kipindi chote cha mwaka, miradi hiyo pia inalenga kuimarisha uchumi wa mkoa huo kwa kurahisisha mawasiliano ya ndani na nje ya mkoa huo unaopakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kagera, Ntuli Mwaikokesya ametaja baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa fedha hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Nyakanazi-Kabingo yenye urefu wa kilomita 50 unaojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh47.9 bilioni.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wanaotembelea miradi ya miundombinu ya barabara inayotekelezwa na Serikali kupitia Tanroads, Ntuli amesema ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha mikoa ya Kagera na Kigoma tayari umekamilika kwa asilimia 100.

Ametaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa barabara ya Bugene-Kasulo-Kumunazi yenye urefu wa kilometa 128.5 na kipande cha barabara ya Bugene-Burigi Chato yenye urefu wa kilometa 60 inayojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh92.84 bilioni inayotarajiwa kukamilika Novemba 10, 2023. Kwa sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 27.7.

‘’Serikali pia tayari imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Bunazi-Kagera Sugar hadi njia panda ya Kitengule inayounganisha Wilaya za Karagwe na Misenyi yenye urefu wa kilometa 25 itakayogharimu zaidi ya Sh54 bilioni. Utekelezaji wa mradi huu utakamilika Septemba, 2025,’’ amesema Ntuli

Ujenzi wa barabara hiyo unganishi unalenga kurahisisha mawasiliano kati ya Wilaya za Karagwe na Misenyi baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa daraja la Kutengule lenye urefu wa mita 140, mradi unaogharimu zaidi ya Sh31.5 bilioni ambao tayari umekamilika kwa asilimia 99.

Kujengwa kwa daraja la Kitengule kumewaondolea wakazi wa wilaya hizo mbili adha ya kuzunguka umbali wa zaidi ya kilometa 28 kupitia daraja la Kyaka kwenda na kutoka njia panda ya Kitengule hadi Bunazi, makao makuu ya Wilaya ya Misenyi.

Ntuli amesema kutokana na umuhimu wa daraja la Kitengule kiwanda cha sukari cha kampuni ya Kagera Sugar, kampuni hiyo imechangia Sh5 bilioni kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja hilo huku Serikali ikitoa zaidi ya Sh26.5.

‘’Kabla ya kujengwa kwa daraja hili, usafirishaji kwenda na kutoka kiwanda cha sukari ulitegemea daraja la Kyaka, umbali wa kilometa 28 kutoka njia panda ya Kitengule Wilaya ya Karagwe yaliko mashamba ya miwa yenye ukubwa za zaidi ya hekta 16,000,’’ amesema Ntuli

Akizungumzia uimara na ubora wa daraja hilo linaloweza kuhamishika, Mandisi mshauri wa mradi huo, Mohamud Kitime amesema licha ya kuweza kudumu kwa zaidi ya miaka 50, daraja la Kitengule linaweza kupitisha shehena lenye uzito wa tani 100.

Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God, Enock Bonna amepongeza uamuzi wa kutekeleza mradi huo akisema umewaondolea wananchi adha ya kuzunguka umbali wa kilometa 28 kwenda na kutoka mjini Kayanga yaliko makao makuu ya Wilaya ya Karagwe kwenda mjini Bunazi ambako ni makao makuu ya Wilaya ya Misenyi.

‘’Hata sisi watumishi wa Mungu tumpata urahisi wa kueneza Injili kati ya wilaya hizi mbili za Karagwe na Misenyi,’’ amesema Mchungaji Bonna

Katika mikakati hiyo ya maboredho ya miundombinu, Serikali imetenga zaidi ya Sh153.5 bilioni kufanyia ukarabati barabara ya lami ya Lushahunga-Rusumo yenye urefu wa kilometa 92, mradi utakaokamilika Julai, 2025.

Kupitia agizo la Makamu wa Rais Dk Phillip Mpango, Tanroads pia inatekeleza mradi wa ukarabati na upanuzi wa barabara kuanzia mzunguko wa Rwamishenye hadi Bandari ya Bukoba itakayokuwa ya njia nne kutoka mbili za sasa.

Mkandarasi tayari yuko kazini kutekeleza mradi huu utakaogharimu zaidi ya Sh4.6 bilioni ambao unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2024.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi