Makala
Ripoti: Nusu ya wanawake wana viriba tumbo
Dar es Salaam. Imekuwa jambo la kawaida kukutana na makundi ya wanawake wa rika mbalimbali pembezoni mwa barabara wakifanya mazoezi. Wapo wanaokwenda kwenye klabu za mazoezi, lengo likiwa ni kujiweka fiti na kulinda afya ya mwili dhidi ya maradhi hasa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa tishio kubwa kwa sasa.
Hata hivyo, kwenye makundi hayo wapo ambao kwa kuwaangalia utabaini wamefikwa na jambo na sasa wanapambana ili kuepukana nalo. Kubwa ni uzito na miili mikubwa iliyopitiliza maarufu kama viriba tumbo. Takwimu zinaonyesha zaidi ya nusu ya wanawake kwenye maeneo mbalimbali nchini, huku Dar es Salaam, Kusini Unguja na Mbeya yakitajwa vinara kuwa na wanawake wenye uzito uliopitiliza au kiriba tumbo. Ripoti mpya imeonyesha.
Dar es Salaam imeendelea kushikilia rekodi yake ya miaka mitano iliyopita, huku Mkoa wa Kilimanjaro ukifanikiwa kung’atuka katika rekodi hiyo.
Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria Malaria (TDHS) wa mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonyesha Kusini Unguja na Dar es Salaam, ndio zinaongoza kwa wanaume wenye uzito uliopitiliza wakiwa ni watatu katika kila kumi.
Ripoti imebaini kuwa wanawake hunenepa zaidi umri unavyozidi kuongezeka ikionyesha karibu nusu ya wanawake wenye miaka 40 hadi 49 ni wanene wakati ni robo pekee wenye miaka 20 hadi 29 ndio wanene.
Pia imebainika wanawake wa miaka 20 hadi 29 wenye uzito kupita kiasi au unene, wengi ni wenye elimu na kipato kikubwa kwenye kaya wanazoishi, ikilinganishwa na wenye elimu ndongo na kipato kidogo.
Asilimia ya wanawake walio na uzito mkubwa au wanene ni kubwa zaidi Zanzibar kwa asilimia 46 kuliko Tanzania Bara asilimia 36 na zaidi mijini (50) kuliko vijijini (28).
Idadi ya wanawake walio na uzito mkubwa au wanene ni kubwa zaidi katika jiji la Dar es Salaam kwa asilimia 54, Kusini Unguja (54) na Mbeya (53) na chini kabisa ni Rukwa na Mara zenye asilimia 18.
Uwiano wa wanawake waliokonda ni wengi Kaskazini Unguja kwa asilimia 14 na chini kabisa ni Iringa kwa asilimia moja.
“Miongoni mwa wanawake vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 19, asilimia ya walio na uzito kupita kiasi au wanene ni kubwa zaidi mijini kwa zaidi ya mara mbili kuliko vijijini ambapo ni asilimia 9 pekee ndio wanene,” imeeleza ripoti hiyo.
Wanaume
Ripoti hiyo pia imeonyesha kuongezeka kwa uzito kupita kiasi na unene uliokithiri miongoni mwa wanaume wenye umri wa miaka 20-49 ambao pia huongezeka kadri umri unavyoongezeka, elimu na utajiri wa kaya.
Asilimia ya wanaume walio na uzito uliopitiliza au wanene ni kubwa maradufu mijini kwa asilimia 26 kuliko vijijini.
Kimkoa asilimia ya wanaume wenye uzito mkubwa au wanene ni kubwa zaidi Kusini Unguja kwa asilimia 32, Dar es Salaam (30) na Mbeya (28) na chini kabisa ni Shinyanga (6), Simiyu (7), Tabora (10) na Geita asilimia 10.
Asilimia ya wanaume vijana wenye umri kati ya miaka 15-19 ambao ni wazito au wanene ni kubwa zaidi Zanzibar kwa asilimia 10 kuliko Tanzania Bara (3).
Sababu yatajwa
Janga la unene kupita kiasi katika maeneo ya mijini, limetajwa kutishia mfumo wa afya, ambapo hatua kali na za kimkakati za kukabiliana na tishio hilo zinatakiwa kuchukuliwa, wataalamu wa afya wameshauri.
Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo alisema jiji la Dar er Salaam lina watu wengi wenye uzito uliokithiri kutokana na mtindo wa maisha wa walio wengi.
Dk Pedro ambaye amewahi kufanya tafiti nyingi, alisema wakazi wa jiji la Dar es Salaam hawazingatii mlo kamili, hula vyakula vilivyopikwa kwenye mafuta mengi, vilivyosindikwa na bila kuzingatia wakati sahihi wa kula.
“Mwaka 2020 JKCI tumewahi kufanya utafiti ambao ulionyesha asilimia 67.2 ya wakazi wa Dar es Salaam wana uzito kupita kiasi, huku idadi kubwa ya watu hao ikionekana ni wanywaji wa pombe wa mara kwa mara,” alisema na kuongeza;
“Tuliangalia aina ya ulaji wa watu, ufanyaji wa mazoezi, unywaji wa maji na uvutaji wa sigara.”
Alisema kwenye suala la ulaji, waligundua watu wanaotumia vyakula nje ya nyumbani hasa wakinunua migahawani, walionekana kuwa na uzito mkubwa ikilinganishwa na wale wanaobeba vyakula kutokea nyumbani.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa inayowafanya wengi wawe na uzito kupitiliza ni kutokuwa na nidhamu ya muda wa kula na wanakula vyakula ambavyo si vizuri kiafya.
Pia Dk Pedro alisema waliangalia mwenendo wa ulaji wa mbogamboga na matunda kwa siku kulingana na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambapo walibaini wale waliokuwa na ulaji mdogo kuliko inavyopaswa walikuwa kwenye hatari zaidi ya kupata uzito uliokithiri.
“Hali hii inachangia shinikizo la juu la damu, wanywaji wa pombe na watu wasiozingatia unywaji wa maji, tabia bwete na kutoushughulisha mwili wala nusu saa kwa siku tano kwa wiki ndiyo wanaoathirika zaidi na uzito uliopitiliza.”
Mwenyekiti wa chama cha wagonjwa wa kisukari na Mwenyekiti wa muungano wa vyama vya magonjwa yasiyoambukiza, Profesa Andrew Swai alisema watu wengi wamekuwa wakitumia zaidi vyakula vya haraka vinavyoongeza mafuta na sukari kwa wingi mwilini.
Alisema kwa kawaida binadamu anatakiwa kula vijiko vitano vya sukari kwa siku, lakini baadhi ya vyakula vina sukari iliyozidi mfano soda yenye ujazo wa mil 350 ina sukari vijiko 10, hali inayochangia sukari hiyo kugeuzwa mafuta na hivyo mtu kuwa na uzito kupita kiasi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge alionya kuwa sababu kubwa ya wanawake kuwa na uzito mkubwa ni kutopangilia mlo sahihi kwa maana ya kula mlo kamili.
Alisema kwa kawaida kila binadamu anatakiwa kuwa na uwiano sawa kati urefu na uzito wa mwili yaani BMI, “Kawaida inatakiwa kuwa 18 mpaka 29.5 ikiwa kuanzia 30 kwenda juu ana uzito uliopitiliza, kuna sababu nyingi sana zinasababisha mtu kuwa na uzito uliopitiliza pamoja na nyama zembe za mgongoni chanzo ni kutofuatilia mlo kamili.”
Alisema kitu cha msingi cha kuzingatia ni kuepuka vyakula vyenye mafuta na sukari kwa wingi ambavyo wanawake wengi wamekuwa wakivipenda zaidi.
“Mji kama Dar es Salaam unakua kwa kasi na watu hawapati ratiba ya kula vizuri, wanapenda kula vyakula vya mafuta na sukari kwa wingi na wanatumia pombe kupitiliza, vyakula vya kusindika ambavyo ndivyo vilivyozoeleka.
“Ukiangalia vyakula karibu vyote ni vya kusindika kuna kuku wa kisasa, soseji anakula ilia pate ladha mdomoni na havina maana mwilini na vyakula vingi vinawekwa katika mafriji kwa muda mrefu na hivyo vinapoteza ubora,” alisema.
Nini kifanyike
Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Fatma Mwasora alisema ili kukabiliana na uzito uliokithiri na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni muimu kupunguza vyakula vya mafuta na wanga.
“Ale mbogamboga kwa wingi, asile ugali, wali, mkate kwa wingi, wasiruke milo mtu ahakikishe anakula milo mitatu kwa siku na ahakikishe anafanya mazoezi hata kama hapati muda ofisini anaweza kunyanyuka na kutembea kidogo,” alisema.
Kulingana na takwimu za WHO, watu milioni 41 sawa na asilimia 71 hupoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo watu milioni 15 hufariki dunia wakiwa na umri kati ya 30 na 69.
Kwa hapa nchini, asilimia 27 ya vifo vinavyotokea husababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza WHO.
Baadhi ya wanawake Mkoa wa Mbeya wameeleza sababu za kuwa na miili minene na uzito uliopitiliza kuwa ni kutokana na wingi wa vyakula ambavyo vinalimwa na kuuzwa kwa gharama nafuu.
Neema Mulungu, mkazi wa Mabatini Jijini hapa, alisema miili hiyo imekuwa haizuiliki huku akibainisha urahisi wa utafutaji wa fedha kwa wanawake na gharama za mahitaji kuwa chini pia inachangia.
“Kwa mfano ukienda sokoni na Sh5,000 utarudi na matunda kama parachichi, ndizi mbivu na mbichi maziwa ya mgando na chenji juu, kwani hivyo vyakula baadhi yetu tunavipenda,” alisema.
Kwa mujibu wa daktari wa huduma za dharura katika Hospitali ya Kanda ya rufaa Mbeya, Aveline Laizer wanawake wa mkoa huo wamekua na utaratibu wa kula vyakula vyenye wanga kwa kiasi kikubwa, hali inayosababisha wengi kuwa na uzito uliopitiliza.
Dk Laizer alisema hali ya hewa inachangia watu wa eneo hilo kula sana na hivyo wengi wamejikuta wakijenga utamaduni huo.
“Unapokula wanga mwingi unaongeza uzito, kwani utazalisha sukari lakini pia hawafanyi mazoezi, wengi wana miili mikubwa ulaji wa watu wa Mbeya atakula chakula kingi, parachichi, maziwa mgando na si kwa kiasi kinachotakiwa ni kingi,” alisema Dk Laizer.
Wanawake wengi wamekuwa wakijaribu njia mbalimbali za kuhakikisha wanapunguza uzito uliokithiri kwa kufanya mazoezi, kutumia njia mbalimbali za kupunguza mwili ikiwemo kufanya ditoksi, kupunguza kiasi cha chakula ‘diet’ na wengine mikanda ya kubana wakiamini itaondoa vitambi.
“Tunapambana sana wanawake, licha ya mazoezi wengi wanakunywa dawa za kuondoa mafuta, kufanya huduma mbalimbali za massage za tumbo, lakini ukiacha unarudi palepale, maana wengine sisi tunashinda tumekaa hatufanyi mazoezi,” alisema Coletha Lyimo, mfanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Asilimia kubwa ya Wazanzibari wanapenda kula wali, samaki, pweza na vyakula vingi vyenye asilia ya ngano kama maandazi na mikate.
Mkazi wa Unguja, Hadija Khamis Mzee alisema “Ukiangalia asilia ya kwetu huku kuna ulaji mkubwa uziozingatia lishe bora za afya, vyakula vingi vinavyoliwa pia mafuta nayo yanaweza kuchangia kuwa na uzito mkubwa kupitiliza,” alisema.
Hinja Abdulla, alisema “Kuna watu wanakula lakini hawafanyi mazoezi, mbaya zaidi wengine hata kufanya kazi hawafanyi unakuta wapo kwenye mabaraza wakicheza bao kutwa nzima,”