Connect with us

Makala

Wanaume waongoza kushirikisha wenza mapato yao

Dar es Salaam. Wakati ushirikiano wa kiuchumi kwa wanandoa ukitajwa kuwa chanzo cha maendeleo ya familia, utafiti umeonyesha wanaume takribani watatu kati ya watano huwashirikisha wenza wao jinsi ya kutumia mapato yao ya fedha.

Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni inaeleza kuwa ni theluthi moja tu ya wanaume huamua wenyewe matumizi ya fedha zao.

Utafiti huo ulionyesha asilimia 58 ya wanaume huwashirikisha wake zao katika maamuzi ya kifedha kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

“Miongoni mwa wanaume waliooa wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ambao hupokea mapato ya fedha, asilimia 58 wanaripotiwa kwamba huamua pamoja na wake zao jinsi ya kutumia mapato yao.

“Ni theluthi moja tu sawa na asilimia 34 ya wanaume waliooa ndio huamua wenyewe jinsi ya kutumia mapato yao. Wanawake walioolewa wana uwezekano mdogo wa kuwashirikisha waume zao katika maamuzi kuhusu mapato,” inaeleza ripoti hiyo.

Imebainisha kuwa asilimia 53 ya wanawake hufanya maamuzi ya pamoja na waume zao kuhusu mapato yao, huku asilimia 40 wakisema ni fedha za mwanamume ndizo hufanyiwa maamuzi ya nini kifanyike.

Akizungumzia suala hilo, Solomon Ayubu alisema amekuwa akishirikiana na mkewe katika kufanya uamuzi wa kipato chake, uamuzi huo umemfanya aweze kufanya mambo mengi makubwa, hasa katika ujenzi wa uchumi imara wa familia yake.

Hata hivyo, wapo wanaume waliokiri kuwa wake zao wamekuwa chanzo cha wao kuficha kipato kutokana na matumizi mabaya, huku wengine wakitaja kuwa na kipato kidogo hivyo wanashindwa kuwa wawazi.

“Kipato changu ni kidogo kwa maana ya mshahara wangu. Siwezi kumjulisha mke wangu, hivyo nimekuwa nikifanya kazi mbalimbali kuongeza kipato, hii inanisaidia kubaki na heshima yangu, hata anapoambiwa na shoga zake waume zao wana mishahara mikubwa haimsumbui, japokuwa mimi simtajii,” alisema huku akicheka.

Kwa upande wake, Elizabeth George alisema; “Mimi ni mjane kwa sasa, lakini mume wangu akiwa hai alinishirikisha kwa kila kitu kuhusu kipato chake. Tulifanya maendeleo mengi na tukafanikiwa mpaka kujenga, kusomesha watoto na kujumuika katika masuala ya kifamilia bila kutetereka na alikuwa mume anayeijali familia yake.”

Mtaalamu wa saikolojia, Charles Nduku alisema kwa kuwa mama mara nyingi anakaa nyumbani, baba ndiye anaona awe mwamuzi na hivyo familia za namna hiyo ni mara chache kuwa na maendeleo.

“Mume kutokuwa muwazi kwenye uchumi wake kwa mwenza wake inaonyesha vitu vingi havipo sawa, mwanamume kuna vitu anavificha au anafanya, hataki fedha zake zijulikane na mara nyingi anazitumia visivyo, kwani lengo la msingi ni kujenga familia.

“Anafikiri mwenza wake akivijua italeta changamoto, lakini tafiti nyingi zinaonyesha wanawake wana matumizi mazuri ya kifedha ikilinganishwa na wanaume. Wale wanaoshirikisha wake zao wana mafanikio,” alisema Nduku.

Mtazamo wa kiuchumi

Wachumi wanaitafsiri ripoti hiyo kama ishara ya jamii kuondokana na fikra hasi na tamaduni zilizozoeleka ambapo mwanamke hakuwa anashiriki katika maamuzi ya kiuchumi, huku akishindwa kumiliki rasilimali muhimu miaka kadhaa nyuma.

Mtaalamu na mchumi mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora alisema asilimia 58 ni ndogo kwa macho, lakini ni kubwa na kwa Tanzania inakaribia kutufikisha usawa wa kijinsia 50 kwa 50.

Alifananisha ripoti hiyo na ile aliyowahi kuichapisha mwaka 2022 iliyoonyesha wanawake walioolewa wanafanya biashara vizuri zaidi kuliko wasioolewa.

“Nilipowauliza ikaonyesha kipato kikubwa kinapatikana kupitia waume zao, ule utafiti ulipendwa sana Korea ambako niliuelezea na ilikuwa ni tafiti nzuri kwa nchi yetu,” alisema.

Profesa Kamuzora alisema asilimia 58 kiuchumi ina maana pana kwani mwanamke anaposhiriki au kushirikishwa katika maamuzi ya kipato hukitumia chote katika familia yake, hawezi kukitapanya.

“Baba anaposhirikiana na mama uchumi unakua na ni chanzo cha kujenga familia iliyo bora, pia inaongeza hata uwezekano wa kufanya watoto waone umuhimu wa kuwa na familia, uchumi utakua na pia inachochea maadili ya Kitanzania,” alisema Profesa Kamuzora.

Mchumi mwingine, Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu Zanzibar (Suza) alisema ilimradi watu wameamua kuwa mke na mume na wana familia, wote wawili wanatakiwa kukaa pamoja na kujadili vitu vyote muhimu.

Alisema kuna umuhimu wa kuwa na demokrasia katika familia, kwani katika mila kuna mchanganyiko wa dini na utamaduni ambao unamleta kiongozi wa nyumba yeyote ambaye anatakiwa kushirikiana na msaidizi wake, hapo ndipo maendeleo yatakuja.

“Hii tafsiri yake katika familia zetu sasa tunaenda na utamaduni wa kisasa kwa maamuzi, ukiuliza sababu zinakuwa ni ufahamu na dunia inavyokwenda na masuala ya teknolojia, utandawazi na maendeleo ya kipato na uhusiano wa watu katika jamii ndiyo imebadilisha huo mfumo,” alisema.

Profesa Semboja alisema mke huangalia mume, familia, watoto, ndugu na jamaa, anaposhirikishwa kimaamuzi katika kipato cha mume, kutakuwa na maendeleo mazuri zaidi kwa kuweza kuwekeza.

“Nyumba nyingi nzuri zinazojengwa ni pale ambapo mwanamke yupo vizuri katika familia, ukiangalia sana dunia tunayokwenda mwanamke ni hazina nzuri, ile kumfikiria ni chombo cha starehe imepitwa na wakati. Sasa hivi wanawake wana uwezo mzuri na ndiyo maana benki kwa sasa zinawapa nafasi wanawake katika nafasi za uongozi wanafanya vizuri,” alisema Profesa Semboja.

Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya uchumi na biashara, Oscar Mkude alisema wanandoa kushirikishana ni jambo zuri, ijapokuwa kwa sasa ndoa nyingi zipo katika changamoto.

Alisema kwa ndoa zinazopitia changamoto ni ngumu wanandoa kushirikishana taarifa muhimu za kifedha.

“Kushirikishana ni ishara inayoonyesha ndoa iko vizuri, lakini ukiuliza wanaume watasema wanawake wengi hawawashirikishi kwa kuwa wanataka kuishi kwa kujilinganisha na wengine, na kama mwanamume ana kipato kidogo inakuwa changamoto kutekeleza matamanio ya mwenza wake.

“Wanaume wengi wanaona akimtajia kipato mke atamshusha hadhi, hivyo anabaki kimya, yeye ndiyo anajua taarifa zote, hivi ndivyo wanavyofanya wanaume, lakini anapojiamini na kipato chake kiwe kikubwa au kidogo anashirikisha mwenza,” alisema.

Anasema wanandoa wasioshirikishana masuala ya kifedha, kuna athari ya kutokuwa waaminifu na kushindwa kulea watoto.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi