Kitaifa
Vigogo matumbo joto utekelezaji ripoti ya CAG
Dar/mikoani. Kuna kila dalili kwamba maazimio ya Bunge kuhusu utekelezaji wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yataondoka na ‘vichwa’ vya mawaziri, makatibu wakuu, watendaji wa taasisi na wakurugenzi wa halmashauri (DED).
Hii ni Bunge kupitisha maazimio ya likitaka wote waliotajwa wao wenyewe au taasisi zao, kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma wajitafakari wenyewe au la washughulikiwe.
Juzi, Bunge lilipitisha azimio hilo ikiwa ni mapendekezo kutoka Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Kupitishwa kwa maazimio hayo, kunatokana na mjadala mkali wa siku tatu kutoka kwa wabunge baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hizo zikionyesha namna ripoti ya CAG, ilivyobaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.
Katika kile ambacho wabunge walionyesha kukerwa na ‘madudu’ hayo ya mara kwa mara yanayoibuliwa na CAG, wabunge 168 walijiandikisha hadi kufikia juzi, wakitaka upelekwe bungeni muswada wa adhabu ya kifo kwa mafisadi.
Ni kutokana na moto huo wa wabunge, wengine wakitaka mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wengine waliotajwa katika ripoti ya CAG inayoishia Juni 30 mwaka 2022 wajipime kabla ya mamlaka ya uteuzi kuchukua hatua, ndipo uwezekano wa ‘kulia vichwa’ unapokuja.
“Mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wote walioguswa na taarifa ya CAG na ya kamati, wajitafakari kabla ya mamlaka ya uteuzi haijachukua hatua dhidi yao,” alisema Jashet Hasunga, makamu mwenyekiti wa PAC akisoma maazimio ya kamati hiyo.
Azimio hilo lilipendekezwa na Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka aliyetaka liongezwe kwenye maazimio ya PAC na likaridhiwa na Bunge na kupitishwa kuwa azimio rasmi la Bunge baada ya Spika Tulia Ackson kulihoji Bunge.
Katika hilo, Mwenyekiti wa LAAC, Halima Mdee akizungumza na gazeti hili jana, alisema kazi ya Bunge imekamilika na kinachosubiriwa ni hatua stahiki zichukuliwe kwa wahusika wote waliotajwa.
“Kwa sababu kuna ambao wakati madudu yanatokea walikuwa halmashauri fulani au wizara fulani na sasa wako kwingine, kuwabaini ni kurudi nyuma na kuangalia wakati yakitendeka alikuwepo nani na hatua zichukuliwe dhidi yake,” alisema Mdee.
Baada ya kuwahoji wabunge kwa nyakati tofauti wakati wa kupitisha maagizo hayo, Spika alizishukuru kamati hizo tatu kwa kazi kubwa.
“Mmekuja na mapendekezo mengi ambayo sasa ni maazimio na maazimio yanayopitishwa na Bunge, ni maelekezo ya Bunge kwa Serikali,” alisema
Pia, Spika Tulia alisema Serikali itatakiwa kuwasilisha bungeni taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo katika mkutano wa Bunge, Februari mwakani.
Maazimio hayo ya Bunge hayapishaji maagizo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Aprili mosi mwaka huu, kupitia kamati kuu, kilipoeleza kusikitishwa na baadhi ya maeneo yenye ubadhirifu na kuagiza hatua stahiki zichukuliwe.
“Kamati kuu imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika wote waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi,” alisema Sophia Mjema, aliyekuwa katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wakati huo.
Pamoja na hayo, wengine wanajiuliza iwapo moto huo wa wabunge na azimio hilo la Bunge litamsukuma Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua za kuwawajibisha wahusika kama alivyofanya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete mwaka 2012.
Moto uliowaka bungeni wakati huo kutokana na ripoti ya CAG iliyoibua upotevu mkubwa wa fedha za umma wakati huo, mawaziri walishikwa koo na wabunge wakitakiwa kujiuzulu.
Baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo, wenyeviti wa kamati za hesabu za mashirika ya umma, Serikali za mitaa nao waliwaliwasilisha ripoti na maazimio ya kamati hizo ilikuwa ni kutaka kuwajibishwa kwa mawaziri hao.
Kutokana na hilo, Mei 2012, ripoti hiyo ya CAG ilisababisha mtikisiko mkubwa kwa kuwang’oa mawaziri sita na manaibu wawili ambao ni Athumani Mfutakamba wa Uchukuzi na Dk Lucy Nkya wa Afya.
Mawaziri waliong’olewa ni Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na William Ngeleja wa Nishati na Madini.
Hali kama hiyo iliyojitokeza 2012, ndio ambayo wabunge kwa siku tatu walichangia taarifa hizo za PAC, PIC na LAAC za mwaka 2022 wanataka itokee kwa mawaziri na watendaji serikalini, waliohusika na ubadhirifu huo.
Waliochangia ripoti za kamati hizo za Bunge wanatamani historia hiyo ijirudie kutokana na hali tete iliyopo mtaani kwa baadhi ya wananchi wanaona kama Bunge limekosa meno ya kuisimamia na kuishauri Serikali ili iwashughulikie wanaofanya ubadhirifu.
Pamoja na majibu ya mawaziri kupangua hoja na wengine kukubaliana kuna tatizo, bado fukuto la kutaka waliotajwa katika ripoti hiyo ya CAG wawajibishwe haliko tu kwa wabunge, bali hata kwa wananchi.
Rais Samia mwenyewe wakati akipokea ripoti ya CAG Ikulu Jijini Dar es Salaam, Machi 29, mwaka huu, alionyesha kukerwa na usokozi wa fedha za umma serikalini, akisema atakabana na makatibu wakuu na watendaji wasio na uzalendo.
Jukumu kwa Rais Samia
Spika la Bunge la Wananchi la Chadema, Suzan Lyimo alisema ingawa asilimia kubwa ya wabunge wa sasa wametokana na CCM, anaamini Rais Samia atafanya uamuzi wa kuwachukulia hatua wote waliohusika.
Mojawapo ya kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali, lakini miaka ya nyuma wakati wapinzani wakiwa bungeni kuna baadhi ya mawaziri walijiuzulu kwa tuhuma mbalimbali, na anaamini hata sasa waliotajwa katika ripoti watajiuzulu bila kutenguliwa.
“Shida iliyopo Tanzania uwajibikaji haupo, watendaji hawana utaratibu wa kujiuzulu hadi mamlaka ya uteuzi ichukue uamuzi, lakini natamani Rais Samia aangalie haya mambo na achukue hatua kwa mujibu wa sheria kwa wahusika,” alisema Lyimo aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu kwa zaidi ya miaka 10.
Lyimo ambaye ni spika wa Bunge la Wananchi la Chadema, alisema Bunge limeshamaliza kazi yake, jukumu analo Rais Samia kufanya uamuzi wa hatua zaidi kuhusu watendaji waliotajwa katika ripoti ya CAG.
Hata hivyo, alisema bunge hilo la wananchi litatoka na taarifa kwa umma hivi karibuni baada ya kufanya uchambuzi wa kina na kutoa mapendekezo kwa Serikali.
Kauli ya Lyimo inaungwa mkono na Mhadhiri wa Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kakobe aliyesema Bunge limeshatimiza wajibu wake, kazi iliyobaki ni Serikali kuchukua hatua kwa waliohusika.
Dk Kakobe alisema endapo Serikali itachukua hatua, vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma vitapungua, lakini isipofanya hivyo vitaendelea.
“Kama Bunge limefanya haya, kazi iliyobaki ni kwa Serikali ambayo inafahamu nani na nani wanahusika kwa kiasi gani kupitia vyombo vyake. Inawezekana mawaziri wakawajibika kisiasa, ingawa wao si watendaji wakuu wa wizara wala hawasaini fedha zitoke bali wanasimamia sera.
Jinamizi kama hilo lilijirudia mwishoni mwa mwaka 2014, matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili (Otu), iliyoanzishwa na Serikali nayo ilizua mtikisiko mwingine uliowang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa operesheni hiyo.
Balozi Khamisi Kagasheki wa Maliasili na Utalii ndiye pekee alipata ujasiri na kusimama ndani ya Bunge kabla ya Rais Kikwete kuridhia kujiuzulu kwa mawaziri wengine wanne na kutangaza kujizulu wadhifa wake huo.
Walichokisema wabunge
Akizungumza jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest alisema ni vizuri kwa mawaziri ambao wizara zao zimeguswa kutoa nafasi kwa Rais kusuka upya baraza.
Kuhusu utamaduni wa viongozi kuwajibika kunapotokea mambo hayaendi sawa, Anatropia alisema hakuna utamaduni huo kwa sababu Watanzania wamefanya siasa kuwa ajira badala ya huduma.
Mbunge wa Ndanda (CCM), Cecil Mwambe alisema viongozi ambao wameshindwa kuchukua uamuzi wanatakiwa kujitafakari kwa sababu wameshindwa kumsaidia Rais kwa kuchukua hatua kwa wale wanaobainika kufanya ubadhilifu.