Connect with us

Kitaifa

Matumaini mapya upungufu umeme ukizidi kupungua

Dar es Salaam. Huenda makali ya kukatika kwa umeme yakazidi kupungua, baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kufanikiwa kupunguza upungufu wa umeme kutoka megawati zaidi ya 400 zilizokuwapo Septemba hadi 290 hivi sasa.

Hali hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu wamiliki wa viwanda kufanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na kumuelezea namna uzalishaji bidhaa unavyoshuka kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika.

Akizungumza jana, Mkurugenzi wa miradi wa Tanesco, Dismas Lyamuya alimwelezea Chalamila jitihada zinazofanyika ili kukabiliana na changamoto iliyopo alipotembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I na II.

Alisema wakati mgawo ukianza, megawati takribani 400 zilikuwa zimepungua, lakini sasa zimeshuka hadi megawati 290, ikiwa ni uthibitisho wa maboresho yanayofanyika kwa kutengeneza mashine zilizokuwa zimeharibika

“Tuna imani hizi mvua pia zinazoendelea kunyesha, zikinyesha zaidi maeneo ambayo kuna mitambo yetu, hali ya umeme itaboreka zaidi, ila sisi tunajikita kuhakikisha tunatekeleza wito tuliopewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunamaliza tatizo hili,” alisema Lyamuya.

Septemba, mwaka huu Rais Samia alipomuapisha bosi mpya wa Tanesco, Gissima Nyamo-Hanga alimueleza baada ya miezi sita hataki kusikia kelele za kukatika kwa umeme. Hivyo, alimtaka kusimamia mchakato wa ukarabati wa mitambo unaoendelea hivi sasa, akisema ndilo jukumu lake la kwanza ndani ya shirika hilo.

Tangu wakati huo, matengenezo mbalimbali yamekuwa yakifanyika kwa mujibu wake, huku akiwatoa hofu wananchi kuwa wanaposikia kuzimwa kwa mashine kwa ajili ya matengenezo, hakutaongeza tatizo kwa sababu wanafanya kazi huku wakihakikisha umeme unaendelea kuwapo na shughuli za maendeleo zinafanyika.

Kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha, Lyamuya alisema wanaamini zitasaidia kupunguza tatizo la mgawo wa umeme ikiwa zitanyesha katika maeneo yenye mitambo ya kuzalisha.

Hilo linaendana na uhalisia ulioelezwa siku chache nyuma, ikiwemo kushuka kwa kina cha maji katika baadhi ya mabwawa kuwa kulichangia kushuka kwa uzalishaji.

Mradi wa upanuzi wa Kinyerezi I wenye megawati 185 ulibuniwa ili kuongeza uwezo na upanuzi wa kituo hicho chenye uwezo wa kufua umeme MW 150. Baada ya kukamilika kwa kituo hicho kutafanya jumla ya uwezo wa kituo cha Kinyerezi I kuwa na uzalishaji wa Megawati 335.

Awali, Chalamila alisema moja ya changamoto iliyotajwa na wamiliki wa viwanda ni kukosekana kwa umeme wa uhakika.

“Kwa mfano wenye viwanda vya saruji walisema uchanganyaji wao wa malighafi ili kupata bidhaa unapoanza hakutakiwi kutokea tatizo lolote la umeme na endapo itatokea ni hasara kwao, kwani inaweza kuganda,” alisema Chalamila. Kutokana na suala hilo, aliwataka wananchi kutunza mazingira yanayowazunguka, ikiwemo miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri baadhi ya huduma kama upatikanaji wa umeme.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi