Kitaifa
Petroli, dizeli zashuka bei, mafuta ya taa yakipaa Dar
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za nishati ya mafuta mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ambazo zinaanza kutumika leo Novemba 1, 2023; huku kwa mkoa wa Dar es Salaam, petrol na dizeli zikionekana kushuka, wakati mafuta ya taa yakipanda.
Kwa mujibu wa Ewura, kwa Dar es Salaam, Petroli itauzwa Sh3,274, dizeli ni Sh3,374 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 3,423; be hizi ni kwa kipimo cha lita moja (bei za rejareja).
Kutokana na tangazo hilo la bei hizo mpya, inaonyeshakuwa petrol imeshuka kwa Sh7 kwa lita wakati dizeli imeshuka kwa Sh74 kwa lita, huku mafuta ya taa yakipanda kwa Sh480 kwa lita, tofauti na bei kikomo zilizotangazwa mwezi uliopita kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa upande wa Tanga, petroli itauzwa kwa Sh3,274 kutoka Sh3,327, huku dizeli ikiwa imepanda kutoka Sh3,494 hadi Sh3,510; na mafuta ya taa yatauzwa Sh3,469 tofauti na ilivyokuwa mwezi uliopita ambapo yaliuzwa Sh2,989.
Taarifa ya Ewura imeendelea kueleza kuwa kwa Mkoa Mtwara, petroli itauzwa Sh3, 347, huku dizeli ikuzwa Sh3, 546; hata hivyo bei za mafuta ya taa zinaonekana kupanda kutoka Sh3, 016 had Sh3, 495.
“…mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Oktoba 2023 yanatokana na kupungua kwa bei za mafuta katika soko la dunia kwa wastani wa asilimia 5.68 na gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 13 kwa petroli,” inaeleza taarifa hiyo na kuongeza;
“…asilimia 25 kwa dizeli na uamuzi wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani (OPEC+) kupunguza uzalishaji na vikwazo vya kiuchumi ambavyo nchi ya Urusi imewekewa.”