Connect with us

Kitaifa

Wajawazito sasa kula vidonge vya ‘Folic Acid’ kwenye ugali

Arusha. Katika kukabiliana na tatizo la udumavu nchini, Serikali inatarajia kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa mashine maalum za kuchanganya virutubishi kwenye vyakula.

Kwasasa mashine ya aina hiyo imetengenezwa nchini kwa kutumia vifaa vilivyoletwa na shirika la ‘GAIN’ ambapo ilizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Arusha,

Mashine hiyo inachanganya virutubishi vya Vitamini B, Folic Acid, sambamba na madini ya chuma na Zinki kwenye mahindi wakati wa kusaga.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa mashine zilizonunuliwa na shirika la ‘GAIN’ la kutokomeza utapiamlo nchini, Mkurugenzi Idara ya Sera na Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Paul Sangawe alisema kuwa Serikali sasa itaweza kukabiliana na udumavu kwa kuchanganya virutubishi hivyo kwenye chakula kikuu kwa wengi ambacho ni mahindi.

“Serikali ilikuwa inapitia changamoto kubwa ya udumavu na utapiamlo kutokana na kukosekana kwa mashine hii, ambayo hivi virutubishi ilikuwa lazima mtu avipate kwa vidonge au vyakula vingine sasa watakula kwenye ugali wakiwemo hata wale wanawake wajawazito ambao huwa wanavikwepa wanapopewa kwenye vituo vya afya na kusababisha matatizo makubwa kwa watoto walio tumboni,”amesema.

Amesema kuwa Serikali inatarajia kutenga bajeti za kununua mashine hizo zinazotengenezwa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) na kuzisambaza nchini ili kuhakikisha wajasiriamali wanaosaga mahindi wanazitumia katika kuchanganya virutubishi hivyo kwenye unga.

Akizungumzia mradi wa usambazaji mashine hizo, mkuu wa kitengo cha program kutoka shirika la Gain la nchini Uswiss linalojishughulisha na utokomezaji wa utapiamlo nchini, Dk Winifrida Mahila alisema kuwa waliona tatizo la udumavu nchini na wakaamua kununua mashine hizo nje ya nchi kuleta nchini.

“Ilikuwa ni gharama sana kununua nje kwani iligharimu zaidi ya milioni 5 kwa moja, hivyo tulipoona dhamira ya serikali kutaka zitengenezwe hapa nchini tulisaidia vifaa vya kutengenezea na wataalamu wamefanikiwa na sasa inapatikana kwa gharama ya milioni 1.5,”amesema.

Alisema kwa kuanzia wamenunu mashine 50 na wanasambaza katika mikoa mitano ya manyara, kagera, Kilimanjaro, Mbeya na Tanga ambazo zina wazalishaji wadogo na kulisha kundi kubwa la wananchi.

Awali akizindua mashine hiyo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa aliwataka wadau wa chakula na lishe nchini kuhakikisha virutubisho vinavyotumika katika mashine hizo vinazalishwa nchini ili kuondokana na utegemezi wa kuviagiza kutoka nje ya nchi mara kwa mara.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi