Connect with us

Makala

Wanafunzi hawa wapo wapi?

Dar es Salaam. Wanafunzi 148,229 waliopangiwa shule kwa ajili ya kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2022 hawajulikani walipo na hawatafanya mitihani ya upimaji wa kidato cha pili inayotarajiwa kuanza Oktoba 30 hadi Novemba 9, mwaka huu.

Hiyo ni baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kupitia Katibu Mtendaji wake, Dk Said Mohamed kutangaza wanafunzi 759,573 kutoka shule za sekondari 5,546 Tanzania Bara ndio watakaokaa darasani kwa ajili ya mitihani yao ya upimaji kidato cha pili.

Idadi hiyo ni pungufu ya asilimia 16.32 ikilinganishwa na wanafunzi 907,802 waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2022 na Serikali baada ya kufaulu mitihani yao ya darasa la saba, iliyofanyika mwaka 2021.

Dk Mohammed alisema watakaokaa katika mitihani hiyo ni wavulana 353,807 na wasichana 405,766.

Ukilinganisha na waliofaulu mtihani mwaka 2021 wavulana walikuwa 439,835 na wasichana walikuwa 467,967.

Hiyo ikiwa na maana ndani ya kipindi cha miaka miwili ya masomo wavulana 86,028 wameachwa njiani ambayo ni sawa na asilimia 58.03 ya wanafunzi wote ambao hawajulikani wanafanya nini baada ya kukacha masomo hayo ya sekondari.

Kwa upande wa wasichana, 62,201 hawajulikani walipo ambayo ni sawa na asilimia 41.96.

“Nafikiri mbali na elimu bila ada ipo haja ya wazazi kuelimishwa juu ya umuhimu wa kupeleka watoto shule, baadhi ya maeneo hasa wilaya za pembezoni wazazi wanaona elimu haina maana na hii inaweza kuwa sababu ya watoto wengi kutoendelea na shule,” alisema Alistidia Kamugisha, mdau wa elimu.

 Kamugisha alisema ni vyema wazazi wakatambua ipo tofauti ya mtoto aliyesoma na kukosa kazi na mtoto ambaye hajakwenda shule kabisa, ili wawe mstari wa mbele kuwahamasisha kwenda shule.

“Ili kukomesha hili ni vyema kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, ikiwamo uanzishaji wa sheria ndogondogo zinazoweza kuwabana wazazi na jamii kwa jumla na kuwalazimisha kupeleka watoto shule,” alisema Kamugisha.

Wakati yeye akisema hayo, Faraja Kristomus kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema zipo sababu mbalimbali zinazochangia mdondoko wa wanafunzi hao, mojawapo ni lugha ya kujifunzia na hali za kiuchumi za familia.

Katika lugha za kujifunzia alisema inaweza kuwa sababu ya watoto wengi kukosa motisha ya kuendelea na shule, hasa baada ya kukutana na lugha ya Kiingereza ikiwa wametoka kujifunza kwa Kiswahili kwa miaka yao saba ya elimu ya msingi.

Katika hili, Naibu katibu mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Charles Msonde alisema kutokana na kutambua changamoto ya wanafunzi kushindwa kumudu lugha, Serikali ilizindua mkakati wa kuboresha elimu mwaka 2022, lengo likiwa kuwaandaa wanafunzi ili waweze kumudu lugha ya kujifunzia.

Mkakati huo uliozinduliwa Agosti mwaka uliopita, ulitenga muda wa kuanzia Januari hadi Mei kuwa maalumu kwa wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza kujifunza Kiingereza ili waweze kumudu stadi za kuandika, kusikiliza, kusoma na kuwasiliana.

“Tathmini tuliyoifanya ndani ya miezi mitatu watoto wa kidato cha kwanza wameonyesha umahiri wa lugha na sasa wanakaribiana na wale wa kidato cha pili,” alisema Dk Msonde alipozungumza na Mwananchi.

Kristomus aliendelea kwa kueleza kuwa sababu za mdondoko huo pia zinaweza kutofautiana kati ya eneo na eneo, hususan kwa jamii kama za ufugaji, kilimo na uchumi wa wazazi ambao unawafanya washindwe kumudu mahitaji muhimu.

“Jamii kama ya wafugaji watoto watajikita katika kufuga au kulima. Na uchumi wa familia unapokuwa duni watoto wanaona badala ya kuendelea na shule ni vyema watafute vibarua vya kujiingizia kipato,” alisema Kristomus.

Akizungumzia mikakati ya Serikali katika kukabiliana na mdondoko wa wanafunzi, Dk Msonde alisema njia nyingine ni kuanza kutoa chakula shuleni ili kuwafanya watoto wawe na ari ya kuendelea kubaki shuleni badala ya kuondolewa na njaa.

“Pia tunaboresha mazingira ya utoaji elimu, kujenga shule karibu na makazi ili wanafunzi wasitembee umbali mrefu na kupunguza msongamano darasani, kwani mazingira mazuri ndiyo yanamfanya mtoto kukaa shuleni,” alisema Dk Msonde.

 alisema Dk Msonde.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi