Connect with us

Makala

Wimbi la iPhone feki linavyotikisa nchini

Wakati maendeleo ya teknolojia ya dijitali yakiendelea kushika kasi, simu zisizokuwa na ubora nchini imekuwa biashara ya kawaida.

Wakati mwingine zinageuka janga kwa namna tofauti, huku udhibiti wake ukiwa mgumu kutokana na mbinu zinazotumika katika uingizaji.
iPhone ni miongoni mwa simu zilizoathiriwa na soko hilo, vifaa hivyo ya kidijitali vinazalishwa na Kampuni ya Apple tangu mwaka 2004.

Kwa mujibu wa takwimu zilizoripotiwa na Mtandao wa Statista, Apple imekuwa katika nafasi tatu za juu kati ya kampuni 15 maarufu kwa mauzo ya simu sokoni kati ya mwaka 2009 hadi mwaka huu, licha ya changamoto za uzalishaji na usambazaji wa Iphone feki.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iliyoishia Oktoba mwaka jana, kulikuwa na simu janja hai milioni 17 pekee za 3G na 4G nchini. Hata hivyo, watumiaji wa huduma za intaneti kwa sasa wapo zaidi ya milioni 34, wengi wao wakiunganishwa na simu.

Licha ya kutopata takwimu za iPhone nchini, wakala wa huduma na bidhaa za kampuni hiyo, iStore Tanzania (APR) ni miongoni mwa waathirika wa simu feki tangu ilipoanza huduma zake nchini mwaka 2015 kwa mauzo ya iPhone 5. iStore Tanzania ni miongoni mwa vituo vya Kampuni ya Apple duniani.

Kujua athari ambayo chapa hiyo inapata kibiashara, Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Ofisa Masoko wa iStore Tanzania, Elias Karigo ambaye anasema simu feki ni changamoto kubwa.

“Hilo linaleta shida, kweli ni changamoto, kuna shida mbili. Kwanza mteja unaponunua iPhone kwa muuzaji ambaye hajathibitishwa ni sawa na kucheza kamari. iPhone inaweza kuja halisi sokoni au isiyokuwa halisi ikiwa imefungwa kwenye boksi pia. Kwa sababu mteja hana uzoefu ni rahisi kutapeliwa,” anasema Karigo.

“Baada ya muda, simu inaonekana mbovu na kutengeneza sifa mbaya kwamba iPhone ina shida lakini sio kweli, ni kwa sababu haukuipata halisi. Pili, ni changamoto kwa kampuni simu mbovu kuchafua chapa (brand) yake. Lakini wateja wameanza kuelimika kwa sasa kuhusu tofauti.”

Karigo anasema changamoto ni kwamba simu za Apple awali wengi walizipokea sokoni kama vifaa vya gharama kubwa, jambo ambalo sio kweli, isipokuwa inaendana na thamani halisi iliyonayo.

“Awali, watu wengi waliipokea sokoni kama simu yenye gharama kubwa kuimiliki. Lakini sio kweli, gharama inaendana na thamani halisi ya bidhaa. Baada ya kugundua hilo tukaamua kuanzisha mbinu za kurahisisha kuwafikia wateja wengi wanaotamani kumiliki simu hizi, ikiwamo njia ya kukopesha aliyeajiriwa tu,” anasema Karigo.

Anasema wakati mwingine ofisi yao inapokea simu za kubadilisha hata zile ambazo hazikutoka kwenye chaneli yao ili mradi kudhibiti soko kwa kumuonjesha mteja simu halisi ili asinunue simu feki tena.

“Tukifanya hivyo Apple wanatuadhibu, wanachukia kwa nini iPhone hazijatoka kwetu iStore Tanzania. Lakini sisi tunaamua kuwafanyia top up ili wasinunue tena mahali pengine,” anasema Karigo.

Kuhusu namna ambavyo mtu anaweza kuitambua simu feki, alisema iPhone zilizopo sokoni, zinatambuliwa kwenye seva ya Apple mahali popote duniani, ukifanya activation (ukisafisha simu), inatoa taarifa kwenye seva ya iPhone. Muuzaji anatakiwa akuhakikishie hilo.
Anasema ukinunua iPhone halisi ni vigumu kufanyiwa duplication ya IMEI namba (udukuzi wa namba za utambulisho wa simu), akifafanua kuwa udukuzi ni kwa simu zisizokuwa halisi.

Pia, anasema muuzaji wa iPhone anatakiwa amhakikishie mteja dhamana ya matengenezo bure kwa wataalamu wa mfumo wa iOS wenye vyeti vya ithibati kutoka Kampuni ya Apple.

“Huduma ya matengenezo bure hutolewa miaka miwili, hata kama kioo kitaharibiwa na mtoto nyumbani,” anasema.

Pia, anasema mteja ana haki ya kufanya top up (kubadili simu kwa kuongeza pesa kidogo), ikipata hitilafu kwa sababu zitarudishwa.

“Tatizo lolote la kuharibika kifaa zinafanyiwa top up na kurejeshwa kiwandani. Kuna huduma za kuhuisha mfumo huo, Apple huwa wanahuisha mfumo huo mara kwa mara kwa ajili ya kuimarisha usalama au kwendana na mahitaji mapya ya simu. Kwa hiyo tumekuwa tukieleza wateja wasicheze bahati nasibu katika bajeti zao, kununua simu hazina ubora ni hasara kiuchumi,” anasema.

Hata hivyo, Karigo anasema wao hawashindani na soko la simu feki kwa kuwa ubora wa simu na huduma zao zinawatofautisha na hizo simu nyingine, “huduma kama zetu huwezi kuzipata kwa muuzaji asiyetambuliwa na Apple.”

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi