Makala
Nimeona dalili hizi 9 kuwa upinzani Tanzania unazama
Na Mwalimu Dkt. Gervas Makulilo, DSM
Kwa miaka zaidi ya 8 hivi sasa vyama vya upinzani Tanzania vimekuwa katika wakati mgumu kukua na kuelekea nia ya kila chama kutaka kushika dola. Hapa chini nachambua japo kwa ufupi mambo 9 ambayo nadhani yanasukuma vyama vya upinzani wodini kutafuta matibabu..
1. Kukosa ajenda kubwa na za kudumu. Kwa muda mrefu vyama hivi vimekuwa na ajenda na operesheni zisizodumu lakini pia zisizokuwa na mrejesho kwa umma. Operesheni kama Join The Chain ya CHADEMA au Shusha Tanga Pandisha Tanga ya ACT. Operesheni hizi nyingi huwa hazina miongozo ya malengo, matokeo na mrejesho kwa umma. Jambo hili limefanya vyama hivi vingi kuwa vya matukio ya kila siku.
2. Kukosa majawabu mbadala ya matatizo ya Watanzania. Hili ni la kisera. Mbali na kusema kwamba wanataka kushika dola kwa kuitoa CCM madarakani, vyama hivi havijatumia majukwaa ya kisiasa kama mikutano, mimbari za akademia, vyombo vya habari, mitandao na kadhalika kuelezea yapi hasa majawabu yao pale watakapowe madaraka na wananchi. Majawabu ya ajira, maji, nishati na kadhalika. Mfano nini hasa watafanya kuchochea ukuaji wa viwanda, kukuza kilimo, na kadhalika. Kukosekana kwa umahiri huu wa kisera kunajenga picha ya mtu asiye na majibu anayesema tu “nipe nafasi” lakini nini hasa atafanya na kwa namna gani na itachukua muda gani haelezi.
3. Migogoro ya wenyewe kwa wenyewe. Hii imekuwa kansa kubwa kwenye vyama hivi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992. Ni kweli baadhi ya migogoro ina mkono wa CCM lakini pia mingi inatokana na ukinzani wa kimaslahi na kiitikadi wa wenyewe kwa wenyewe kwenye vyama hivyo.
4. Ubadhirifu kwenye ruzuku. Taarifa ya CAG mara kwa mara imeonesha wizi au matumizi ya mabilioni ya shilingi katika vyama hivi. Mfano ni CHADEMA ambayo taarifa ya CAG ilionesha Mwenyekiti wake aliuzia chama hicho magari kwa bei juu bila kufuata kanuni za manunuzi. Wananchi wengi wana hofu iwapo wanaweza kumuamini kwa matrilioni yule asiyeaminika kwa mabilioni au mamilioni.
5. Ufinyu wa matawi na siasa za field. Sehemu kubwa ya vyama hivi vimekuwa haviongezi idadi ya matawi na wanachama na vimeingia katika propaganda ya kupika namba, kwamba tuna wanachama kiasi fulani. Idadi hizo hazioneshi matawi. Uhalisia huja kwenye uchaguzi. Propaganda ya namba hizi ni sawa na kusema una afya wakati una maradhi, mwisho kifo hukuumbua.
6. Kushindwa kubadili seke seke ya uchaguzi mkuu wa 2020 kuwa vuguvugu lenye matunda kwa katiba na uchaguzi mkuu 2025. Jambo hili linatokana na sababu hizo 5 za mwanzo hapo juu kwa pamoja. Siasa inahitaji muda, umoja wa wanaofanya siasa na mbinu kama za kivita. Changamoto 5 za mwanzo nilizotaja zimeunyima upinzani nafasi ya kutumia kilichotokea 2020 kuwaletea manufaa kwenye siasa.
7. Siasa biashara. Vyama hivi vingi vimekuwa biashara. Viongozi wake wanahongwa na wafanyabiashara na watawala kwa ajenda binafsi na vichwa na nafsi zao sasa zimekuwa kama bidhaa. Aina hii ya kufanya siasa haiwezi kukuleta chama cha ukombozi.
8. Mvutano wa taji la ushindi kati ya wanasiasa na wanaharakati. Katika siku za karibuni tumeshuhudia baadhi ya wanaharakati wakisema wanasiasa hawana nia ya kweli kuikomboa jamii. Tukumbuke kwamba unganiko la wanasiasa na wanaharakati ndiyo hasa chachu ya siasa kiasi kwamba mstari baina yao ni kama haupo. Kitendo cha makundi haya kushindana kinaleta picha kwamba kuna vita ya maslahi. Kinachora picha ya fisi wanaopigania mzoga na matokeo yake ni kudhoofisha imani ya umma kwa makundi haya.
9. Kununulika kwa wanasiasa. Hii tumeona sana kati ya mwaka 2016 hadi 2020. Tumeona wanasiasa na wanaharakati wakifungwa midomo kwa vyeo, mali na fedha. Picha hii inawapa wananchi uthibitisho kwamba watu hawa ni watu maslahi na wakipata nafasi ya kuwa sehemu ya keki ya utawala wanafunga midomo. Hii imeondoa imani kwa upinzani na wanaharakati. Mfano ni Profesa Palamagamba Kabudi, Dk Bashiru Ally, Humphrey Polepole, Shibuda, Mrema (marehemu) na wengineo.
Kuna mtu kaniuliza swali jana, je upinzani utaibuka tena chini ya Rais Samia?
Nimemjibu upinzani ni sifa ya binadamu lakini nimemjibu pia kwamba sioni upinzani ukivuna tija katika kipindi cha miaka mitano au zaidi ijayo ya Rais Samia. Kuruhusiwa kwa mikutano ya siasa kuna faida na hasara lakini tumeona hasara kwao zaidi. Hakuna ujenzi wa matawi mapya, kuna magomvi ya wao kwa wao, ajenda haziko za kudumu, hakuna majawabu, na kadhalika. Kwa ufupi mikutano imewavua tena nguo. Pengine serikali ya Rais Samia kuruhusu mikutano ilikuwa moja ya mbinu kubwa za mkakati wa kisiasa, sawa na kumpa mtu kamba ambayo japo anaweza kuamua kutumia kuchota maji kisimani lakini anaweza pia kujinyongea.
Kitachookoa upinzani ni kurudi na kujipanga upya aina ya siasa inazofanya lakini sio hilo likitokea na kufanikiwa walau kwa miaka kadhaa mbele.
Mpaka wakati mwingine .. Kwaheri kwa sasa.