Kitaifa
Mita za zamani za luku mwisho Oktoba 25
Dar es Salaam. Umetazama mita yako ya luku kama inaanzia na namba 04 au 05?
Shirika la Umeme nchini(Tanesco) litafunga mita hizo takribani 30,000 zenye utambulisho wa namba hizo Oktoba 25, mwaka huu, ikiwa ni siku 18 kuanzia leo endapo mteja hautabadilisha.
Mita hizo za teknolojia ya matumizi ya ‘lipia umeme kadiri utumiavyo’, zinamilikiwa na wakandarasi wawili: Conlog (namba 04) na CBI-Electric (namba 05).
Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 7, 2023 kaimu meneja wa mawasiliano na masoko Tanesco, Irene Marobe amesema mita hizo hazitaweza kuakisi mabadiliko mapya ya kimfumo yatakayofanyika mwaka ujao chini ya Shirika la kusimamia Viwango vya Kimataifa vya Mita za Luku (STSA).
Kwa mujibu wa Tanesco, inatoa huduma za umeme kupitia aina 15 ya mita hizo zenye wateja zaidi ya milioni 4.4 nchi nzima tangu mwaka 1996 ambazo zilianza kubadilishwa Septemba mwaka huu lakini mita hizo 30,000 ndio zilikuwa zimebakia na hazikufikiwa kutokana na changamoto mbalimbali.
“Miaka ya nyumba hakukuwa na mfumo wa kuhifadhi data kidigitali, kwa hiyo hakutukuwa tumewahifikia kwa sababu wengine walibadili umiliki wa nyumba, kupoteza kadi, kuhama makazi au kupangisha watu tofauti,”alisema
“Kwa hiyo tunaamini muda huu unatosha, kila mteja mwenye mita hizo ajitokeze ili tumbadilishie mita hizo zilizokuwa zimebakia, wasipojitokeza tutazifunga wasipate huduma ili isadie kuwapata kwa urahisi, tunafanya hivyo ili kuwasaidia wasikose huduma mabadiliko yatakpofanyika mwakani.”
STSA imejulisha wakandarasi wote wa mita zinazotumia mfumo wake wa lipa kadri utumiavyo kwamba, mwaka 2024 itahuisha mfumo wa utambulisho wa namba za mita hizo ili kuimarisha usalama wake hivyo namba hizo 04 na 05 zimepitwa na wakati na hazitaweza kupokea mabadiliko hayo.
Wakati teknolojia hii inaanza mwaka 1996, Tanzania ilikuwa miongoni mwa mataifa ya awali kutumia Luku ikitanguliwa na Afrika Kusini. Kabla ya mfumo huo, Tanzania ilitumia mfumo wa mita za makadirio (Conventional Meters) kwa malipo ya bili kila mwezi.
Kutokana na mageuzi ya mfumo huo, Irene amesema baadhi ya mafanikio ni pamoja na utambuzi wa wateja wake milioni 4.4 nchi nzima pamoja na mauzo yaliyofanyika.
Shirika hilo kwa sasa limefikia mali zenye thamani ya Sh20trilioni huku likiingiza mapato ya Sh2.3trilioni kupitia watumishi 12,000 magari 1,600, ofisi kila wilaya.