Makala
Unyanyapaa tishio kwa wagonjwa wa akili

Dar es Salaam. Katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko la matukio ya watu kujiua, kuua wenza wao na vitendo vya ukatili, ambavyo huripotiwa kwenye vyanzo mbalimbali vya habari.
Kwa matukio yanayoripotiwa kwenye mitandao ya kijamii, katika eneo la maoni ya wasomaji, mengi hulaumu, kukebehi au kutania uamuzi uliochukuliwa na aliyeathirika.
Taarifa za wataalamu wa afya ya akili, zinasema maoni hayo hutokana na jamii kuwa na uelewa mdogo kuhusu magonjwa ya akili na unyanyapaa ulio kwa jamii. Wanahusisha matukio hayo na changamoto za afya ya akili bila kupata matibabu kwa muda mrefu.
Tunapoelekea maadhimisho ya siku ya afya ya akili duniani Oktoba 10, wataalamu hao wanapendekeza zifanyike jitihada za pamoja kuondoa unyanyapaa kwa jamii na kuongeza uelewa.
Uchunguzi uliofaywa na gazeti hili hivi karibuni kwenye mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dodoma kuhusu magonjwa ya akili, unaonyesha sababu za magonjwa ya akili ni matumizi ya pombe kupitiliza, matumizi ya dawa za kulevya, ugonjwa wa muda mrefu, msongo wa mawazo wa muda mrefu, kupoteza kazi, ukosefu wa ajira na madeni.
Daktari wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure, Mwanza, Meshack Samwel amesema mtu mwenye afya ya akili ni yule mwenye uwezo wa kupambana na changamoto zote za kila siku bila kujali ni za aina gani.
Amesema kushindwa kumudu utatuzi wa changamoto hizo, kukiambatana na kujitenga, mawazo ya kujiua, ni baadhi ya dalili za ugonjwa wa akili.
Unyanyapaa wa jamii kuita watu majina ya kufedhehesha kama chizi, kichaa au dishi limeyumba anasema kunachangia watu kuficha dalili za ugonjwa wa akili kwa kuhofia kuitwa majina hayo.
“Majina haya yanayoendana na maoni yenye kauli za kuudhi, kukebehi na kudhalilisha baada ya mtu kujidhuru, huogopesha watu kutafuta msaada na kuteseka kimya kimya. Hii husababisha ugonjwa kukomaa na madhara kuwa makubwa, ikiwamo kujiua au kuua,” amesema Dk Samwel.
Hospitali hiyo imejipanga kuondoa unyanyapaa na kuongeza uelewa kwa kuanzisha kliniki maalumu ya magonjwa ya afya ya akili mara tatu kwa wiki.
Pia imepata mtaalamu mmoja wa magonjwa ya akili hospitalini hapo, ambaye kwa miezi sita nyuma hakuwapo.
“Tulikuwa tunaelekeza wagonjwa kwenda Bugando, kwa sababu hatukuwa na mtaalamu wa magonjwa ya akili. Kliniki ilikuwa mara moja kwa wiki,” amesema.
Amesema huzitembelea shule, vyuo na nyumba za ibada kuelimisha watu namna ya kutunza afya ya akili.
Amesisitiza umuhimu wa kuboresha malezi kwa familia ili kuepuka vijana kuingia kwenye tabia hatarishi kama matumizi ya pombe na dawa za kulevya.
Dk Paul Lawala, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, alisema unyanyapaa husababisha watu kuwakimbia ndugu zao na kuiachia mzigo Serikali, wakiamini mgonjwa wa akili sehemu yake ya kuishi ni hospitali.
Dk Martin Andrea wa idara ya afya ya akili katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, alisema wagonjwa wengi au ndugu zao hawajui wanaumwa mpaka wafikwe na changamoto kubwa na kufikishwa hospitalini wakiwa wameumia, kuumiza na kufungwa kamba.
“Tunaifikia jamiii kupitia vyombo vya habari kuwaeleza umuhimu wa wagonjwa kufika hospitali mapema. Hii inaenda sambamba na kueleza umuhimu wa kumaliza unyanyapaa kwa wagojwa wa akili,” amesema.
Akizungumzia idadi ya wagonjwa waliofika kupata matibabu hospitalini hapo kwa mwaka 2021 hadi 2023, alisema jumla yao ni 2,361 na 1,071 walilazwa.
Dk Catherine Magwiza, mtaalamu bingwa wa magonjwa ya akili hospitali ya Bugando alisema gharama za matibabu hutofautiana kulingana na dawa anazopata kila mgonjwa.
“Gharama za matibabu kwa wagonjwa wa kuja na kuondoka ni ngumu kufahamu, ila kwa walio wengi ni kati ya Sh20,000 na Sh30,000 kwa kila mgonjwa kwa mfumo wa kuchangia gharama za matibabu. Hii hujumuisha gharama za kumuona daktari na kuandikiwa dawa za mwezi mmoja,” amesema.
Amesema kwa wagonjwa wanaolazwa wasio na bima gharama ni kati ya Sh150,000. Mwaka jana jumla ya wagonjwa 548 walilazwa hospitalini hapo na wagonjwa 341 walitibiwa na kurudi nyumbani.
Kwa mwaka huu hadi Machi, wagonjwa wa kulazwa walikuwa 147 na jumla ya wagonjwa 1,193 walipata huduma za matibabu ya kuonwa na kuondoka.
