Kitaifa
Mwigulu aipiga ‘stop’ TRA kufunga maduka
Kyela. Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema kitendo cha maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), kuwafungia maduka wafanyabishara wadogo ni changamoto inayochochea kuwepo kwa uingizwaji holela wa bidhaa za magendo nchini.
Nchemba amesema hayo jana Jumatatu Oktoba 2, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Njisi, Kasumulu katika mpaka wa Tanzania na Malawi, kwenye ziara aliyoambatana na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa.
Hatua hiyo ya Nchemba imekuja kufuatia malalamiko ya wafanyabishara kufungiwa maduka kutokana na kushindwa kulipia leseni zao kwa wakati.
“Naagiza TRA kuanzia sasa, acheni kuwasumbua wafanyabishara wadogo kwa kufunga maduka yao, kwani ni sehe,mu ya maisha yao, na pia wanasomesha watoto, sasa wekeni mifumo mazuri ya ukusanyaji wa kodi,” amesema na kuongeza;
“Serikali imekuwa ikikusanya mapato kwa lengo la kusaidia kuboresha sekta binafsi, sasa endapo mkitumia mfumo wa ukusanyaji mapato kwa kufunga maduka, hamtafikia malengo.”
Nchemba amesema umefika wakati wa TRA kujenga uhusiano mazuri na wafanyabishara ikiwepo kutoa elimu au kuweka mfumo mzuri wa kulipia leseni hizo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi amesema ujio wao katika Wilaya za Kyela na Rungwe, ni kufanya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu hususan barabara ya Ibanda mpaka Kajunjumele yenye urefu wa kilometa 22 inayonganisha bandari ya Kiwira na Itungi
“Miradi hiyo itakapo kamilika itakuwa chachu ya kufungua fursa za kiuchumi hususan mwingiliano wa kibiashara baina ya Tanzania na Malawi,” amesema.
Mfanyabiashara Ester Jordan, amesema kitendo cha Waziri wa Fedha kupiga marufuku TRA kuwafungia maduka, kutawafanya kulipa kwa wakati pindi wanapokuwa na uchumi mzuri.
“Sio kwamba hatupendi kulipa kodi, hii ni nchi ambayo inajiendesha kwa kodi za watanzania, tunaomba tu uwekwe mfumo mzuri ili tusikinzane na Serikali,” amesema.
Mawaziri hao wako mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ya kukagua miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Rungwe na Kyela sambamba na mradi wa barabara njia nne kutoka Nsalaga Uyole mpaka Ifisi.