Kitaifa
Chalamila: Hakuna aliyepoteza maisha ajali ya moto Kariakoo
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kufuatia tukio la moto eneo la Big Bon Kariakoo hakuna mtu aliyepoteza maisha.
Akizungumza baada ya kuwasili katika eneo la tukio, leo Oktoba 1, 2023 Chalamila amesema moto ulianza kwenye jengo moja na baadae kusambaa kwenye baadhi ya majengo.
Lakini, amesema vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wamiliki wamesaidiana kuokoa baadhi ya mali.
“Hasara itakuwepo kwa wenye mali na kwa majengo, lakini taarifa zaidi tutaendelea kufahamishwa kadri jitihada za kuzima moto zinavyoendelea,” amesema Chalamila.
Kulingana na Chalamila, baadhi ya njia kati ya jengo na jengo zimezibwa na kusababisha watu kushindwa kupita, akitaka zifunguliwe ili zitumike wakati wa majanga.
“Baadhi ya vichochoro tumebaini vitengenezwa na mbao na vimekuwa kichocheo cha moto, nilipongeze Jeshi la zimamoto kwa umahiri wao lakini kwa vyombo vingine vya ulinzi na usalama,” amesema.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Mrakibu Mwandamizi Elisa Mugisha amesema moto umetokea kwenye maduka ya Big Bon lakini hadi sasa chanzo chake hakijafahamika.
Amesema kwa kiasi kikubwa moto umedhibitiwa lakini kuna changamoto ya kuungana kwa majengo hivyo kusababisha moto kusambaa kwa kasi.
“Tulipata taarifa saa moja hadi kufika eneo la tukio tulitumia dakika mbili kwa kuwa ofisi yetu iko jirani, kutokana na changamoto ya ufinyu wa njia za kupita moto ulisambaa kwa kasi,” amesema Mugisha.
Kamanda Mugisha amesema wamelazimika kuomba magari ya kubeba maji maarufu kama maboza ili kurahisisha shughuli ya uzimaji.
“Pamoja na kuwa na stesheni kwa ajili ya tahadhari ya moto, kwa leo maji yalikuwa hayana presha hivyo ikatulazimu kwenda kuchukua maji eneo letu ambalo pia sio mbali na hapa,” amesema.
Amebainisha baada ya shughuli ya kuzima moto huo, watafanya uchunguzi ili kubaini chanzo na kuchukua tahadhari ya matukio kama hayo kujirudia.