Connect with us

Kimataifa

Sh71 bilioni zatumika kuunganisha mikongo ya Taifa ya Uganda na Tanzania

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh71 bilioni zimetumika kugharamia kuunganishwa kwa miundombinu ya mkongo wa Taifa wa Tanzania (NICTBB) na miundombinu ya mkongo wa Taifa wa Uganda (NBI) ikiwa ni katika kuongeza matumizi ya teknolojia na Tehama na  kuwaletea maendeleo  wananchi wa nchi hizo mbili.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Septemba 29, 2023  na Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga, katika hafla ya utilianaji saini wa mkataba huo uliofanyika jijini humo.

Ulanga amesema unganishaji wa mkongo huo kwa Tanzania utafanyika katika mpaka wa Mtukula mkoani Kagera na utakuwa mkataba wa miaka 15.

“Kuunganishwa kwa mkongo huu Uganda, kunaifanya iwe nchi ya tatu kwa Afrika Mashariki kuunganishwa na mkongo huo ikitanguliwa na nchi za Uganda na Burundi,”amesema Mhandisi Mugasa.

Mkurugenzi wa mkongo wa Taifa Uganda, Hatwib Mugasa amesema kuunganishwa kwa mkongo huo nchini mwao kutasaidia kupunguza gharama ya mawasiliano nchini mwao kwa zaidi ya asilimia 50.

Lakini kubwa kuchochea matumizi ya Tehama kwa wananchi na kujiletea maendeleo katika sekta ya kijamii na uchumi kwa jumla.

Waziri mwenye dhamana na mawasiliano nchini Uganda, Dk Chris Baryomunsi amesema uunganishaji wa mkongo huo nchini mwao ni mwanzo mzuri katika kuzinganisha nchi za Afrika na mikongo ya Taifa ambayo anaamini itachochea ukuaji wa uchumi na mawasiliano katika nchi hizo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema ni jambo la kushukuru Uganda kuichagua Tanzania kutumia mkongo wake.

“Kwa kuthamiwa huko ni matumaini yangu TTCL mtakwenda kutoa huduma iliyo bora  kama ambavyo mkataba unasema na sitapenda kusikia malalamiko ya kukatika mara kwa mara mawasiliano,”amesema Nape.

Pia Waziri Nape ameagiza endapo kutatokea changamoto zozote ni vyema zishughulikiwe kwa haraka.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi