Connect with us

Kitaifa

Samia apigia debe kilimo cha mbaazi na ufuta

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Kusini kuongeza ukubwa wa mashamba yao ya mbaazi kwani soko la zao hilo ni la uhakika na tayari Serikali imeingia mikataba ya soko la zao hilo.

Rais Samia alibainisha hayo jana wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Mtama mkoani Lindi, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani humo akitokea Mtwara, ambapo alipata nafasi ya kuweka jiwe la msingi katika miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.

Mikoa ya Lindi na Mtwara ni wazalishaji wa mazao ya korosho, mbaazi na ufuta na katika msimu wa mwaka huu, wameshuhudia bei ya mbaazi ikipanda hadi kufikia Sh2,200 kwa kilo ukilinganisha na huko nyuma ambapo bei ya zao hilo ilifikia Sh100 na katika baadhi ya maeneo kukosa soko kabisa.

Akizungumza na wananchi wa Mtama, Rais Samia alisema Serikali inahangaika kuhakikisha bei ya korosho nayo inapanda.

Hata hivyo, alisema ili bei ya korosho ipande, kuna mambo lazima yafanyike, ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani kwenye korosho wanayoivuna.

Rais Samia alisisitiza wakati wakulaima wanahangaika na changamoto hiyo, ana matumaini msimu wa mwakani, watauza korosho iliyoongezwa thamani na siyo malighafi, huku malighafi zikibaki hapa nchini kwa ajili ya kukamua mafuta, hali ambayo pia itatengeneza ajira ndani ya nchi.

“Ombi langu kwenu ni kuongeza mashamba, nimepita nimeona mashamba madogo madogo ya mbaazi, niwaombe sana ndugu zangu, ongezeni mashamba. Soko lipo na kwa sababu tumeanza na bei nzuri mwaka huu, In shaa Allah bei itaendelea kubakia hivyo na mwaka ujao.

“Tuna mkataba na soko la mbaazi, ongezeni uzalishaji wa mbaazi. Ongezeni uzalishaji wa ufuta, ufuta ni mali duniani, hauachi kuwa na soko na sisi tunafanya kazi ya kuwaunganisha wakulima na soko, tunakimbia wale makangomba wa katikati wanaochukua ufuta wenu kwa bei rahisi halafu wanawaacha na umasikini,” alisema Rais Samia.

Kauli ya Majaliwa

Awali, akiwa jimbo wa Ruangwa, Rais Samia alimpa nafasi Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo, kuzungumza na wananchi ambapo alisema bei ya mazao ya ufuta na mbaazi zimepanda na hasa mbaazi ambayo ilichukuliwa kama zao la chakula, sasa ni la biashara.

“Kwa mara ya kwanza tumeuza mbaazi kilo Sh2,200. Msisitizo wako wa kutafuta masoko umekuwa mkubwa. Mwakani sisi wakulima tutalima mbaazi nyingi, tuombe soko liendelee kubaki hapo hapo,” alisema Majaliwa huku akishangiliwa na wananchi.

Majaliwa aliongeza kwamba kwenye sekta ya madini, alisema baada ya vipimo, wamegundua kwamba Ruangwa kuna madini mengi, na sasa wachimbaji wameanza kuchimba madini ya graphite (kinywe).

“Sasa tumepata kampuni nne za uwekezaji kwenye sekta ya madini hapa Ruangwa…Kazi itakapoanza, wilaya hii itapaa kwa viwango vya juu,” alisisitiza Majaliwa.

Majaliwa alisema changamoto kubwa katika jimbo lake ni barabara zenye viwango vinavyokubalika, hata hivyo alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa barabara zimeanza kujengwa.

Nape na gesi

Akiwa Mtama, mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mwasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alimshukuru Rais Samia kwa kupeleka fedha kwenye jimbo lake kwa ajili ya kutekeleza miradi kwenye sekta za elimu, afya na ujenzi.

Nape alisema mbali na mazao ya mbaazi, ufuta na korosho, watu wa mikoa ya Mtwara na Lindi, waliweka matumaini yao kwenye gesi iliyogunduliwa hapa nchini kwamba itabadilisha maisha yao kiuchumi.

Alimshukuru Rais Samia kwa kurudisha mradi wa gesi ambao ulikuwa umeondolewa lakini sasa matumaini yao yamerejea baada ya Serikali kupeleka mradi wa gesi (LNG) mkoani Lindi utakaokuwa na thamani ya Sh70 trilioni.

“Tunakushuru sana Mheshimiwa Rais, umetuokoa sana watu wa kusini, ni matumaini yetu, Wizara ya Ardhi, washirikiane na Wizara ya Tamisemi na Serikali ya mkoa, tuitumie hii fursa ya gesi kuupanga mji wetu wa Lindi, uwe mji wa kisasa, wenye majengo ya kisasa,” alisema Nape.

Aliongeza kwamba tayari Wilaya ya Mtama imetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Gesi, kwani eneo hilo lipo katikati ya Lindi na Mtwara, hivyo itatoa fursa kwa wananchi wa mikoa hiyo miwili kunufaika na fursa hiyo.

Wananchi wampa zawadi

Rais Samia alipokuwa Ruangwa, wananchi wa Kijiji cha Nandagala walimpatia zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilo 25 za ufuta, mbuzi wawili majike na ng’ombe mmoja.
Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza kwamba zawadi hiyo ni shukrani kwake kwa kufika katika kijiji hicho ambacho alizaliwa.

“Wananchi hawa wanakupa kilo chache za ufuta, kilo 25 ambazo wakati mwingine zinafaa kutafuna na mkate, unapata lishe.

“Mbili, wanakupa mbuzi wawili majike ili ukitaka kufuga sisi tutawapeleka mpaka Kizimkazi, hakuna shida. Lakini tatu, wametoa ngombe mmoja ili tumpeleke kizimkazi na sisi tuko tayari kumpeleka Kizimkazi. Naomba uzipokee zawadi zetu hizo kwa niaba ya wananchi hawa,” alisema.

Akizungumza baada ya kupewa zawadi hizo, Rais Samia aliwashukuru wananchi wa Ruangwa kwa zawadi walizompa na kuahidi kwamba atarudi tena.

“Waziri Mkuu amesema ufuta nitapaka kwenye mkate lakini sisi Wazanzibari tuna kitu kinaitwa kashata. Kwa hiyo ufuta huu nakwenda kutengeneza kashata,.watoto wanazipenda sana,’’ alisema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi