Kitaifa
Toto Afya Kadi bado ya moto

Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kubadili mfumo wa utoaji bima za afya kwa watoto, umeibua mjadala mkali mtandaoni, huku Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akilazimika kuingilia kati kutoa ufafanuzi.
Utaratibu wa sasa unataka kuwasajili watoto kupitia vifurushi vya bima au shule wanazosoma kama wategemezi.
Baadhi ya waliochangia mjadala huo jana wameishauri Serikali kuishirikisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika utaratibu huo. Pia kufungamanisha bima ya afya na mifuko ya hifadhi ya jamii, ili kuwapata wanafunzi wengi watakaojiunga na bima ya afya.
Mjadala huo uliibuka kwa kasi jana ikiwa ni miezi sita tangu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ulipotangaza kusitisha kifurushi cha usajili wa bima kwa watoto ‘Toto Afya kadi’ Machi 13, mwaka huu.
Kusitishwa kwa kifurushi hicho kulitokana na kile Serikali ilichoeleza kuwa, bima hiyo ni tishio kwa uhai wa NHIF kutokana na idadi ya waliojiunga kuwa wachache, lakini matumizi ya mfuko kwa kundi hilo ni makubwa.
Jana kupitia mtandao wa kijamii wa X, Waziri Ummy aliomba maoni ya wadau ili kuboresha bima ya afya kwa watoto.
Wakati Waziri akifanya hilo, hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii kwa mara kadhaa imeshuhudiwa kukitolewa taarifa bandia kwa umma zikieleza kwamba utaratibu wa awali wa Toto Afya kadi unarejeshwa, hatua iliyoilazimu NHIF kukanusha.
“Zipo sababu za msingi kwa nini NHIF wamebadilisha utaratibu wa kusajili watoto wanaojiunga na NHIF kwa hiari. Huwezi kuwa na bima inayokusanya Sh5 bilioni fedha inayolipwa kwa watoa huduma, yaani matumizi ni Sh40 bilioni!
“Tanzania, watoto ni takribani milioni 31. Watoto waliokatiwa Toto Afya Kadi ni kama laki mbili tu, hawajafika hata asilimia moja ya watoto wote nchini. Sasa leteni ushauri ni vipi NHIF wataweza kuvutia watoto wengi zaidi ambao hawana changamoto za kiafya kujiunga na bima ili pale watakapougua waweze kuchangiana,” aliandika Waziri Ummy.
Alisema Toto Afya kadi haijafutwa bali kilichobadilika ni utaratibu wa kuwasajili watoto; akisisitiza utaratibu wa sasa ni watoto wasajiliwe shuleni kwa gharama ya Sh50,400 ili waingie wengi wasio wagonjwa na hivyo kuchangia wachache watakaougua.
Namna ya kuongeza watoto
Katika andiko la waziri, mmoja wa wachangiaji aliishauri Serikali kuishirikisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili maelekezo yashuke kwa wazazi na watakaokuwa tayari waingize watoto kwenye utaratibu huo wa bima.
“NHIF wapite kutoa elimu kwenye shule, pia tuanzishe klabu za afya shuleni ambazo zitahamasisha bima ya afya. Ofisi ya Rais Tamisemi wasaidie kuhamasisha jambo hilo,” aliandika mchangiaji huyo.
Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alishauri bima ya afya ifungamanishwe na mfumo wa hifadhi ya jamii.
Zitto alishauri kuwapo mfumo wa hifadhi ya jamii ambao utapanuliwa kutoka kwenye kundi dogo la watu wazima milioni 1.8 hadi watu milioni 17.2 kwa sasa ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata bima ya afya.
“Tunataka mfumo unaomfanya mtu alipe bima kulingana na uwezo wake lakini apate huduma kulingana na mahitaji yake. Hali ya sasa katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa sehemu kubwa, umekuwa ukitegemea uwezo wa kifedha wa mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa,” aliandika Zitto.
Alisema kwa wananchi ambao ni masikini, wanaoishi chini ya mstari wa umasikini (Watanzania milioni nane), Serikali iwachangie kwa asilimia 100 kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii Sh30,000 kila mwezi.
Maoni hayo ni tofauti na mtazamo wa Dk Norman Jonas, aliyeshauri ili kundi kubwa lichangie kwenye bima ya afya, ni muhimu kuweka mfumo wa uchangiaji kidogo kidogo bila mtu kufahamu.
“Nikinunua kitu kiasi fulani kidogo kutoka kwenye bei ya kitu kinachangia bima yangu ya afya, kwa sasa watu wanaohitaji bima hulazimika kuchangia kwa mkupuo. Hii hii inaweza kuwa kikwazo kwa sababu ukiwa na kipato duni unakuwa na kipaumbele kingine kinachohitaji fedha kwa mkupuo,” alisema.
Uhitaji wa chanzo cha uhakika wa mapato kwenye bima ya afya ni muhimu, ndio maana Mfamasia Tumaini Makole, alishauri uhitaji wa kuwa na chanzo cha mapato kama changamoto ni uchache wa watoto waliojiunga kwenye bima ya afya.
“Wananchi wahamasishwe kulipia watoto wao. Kama changamoto ni gharama kwa sababu za kipato, utaratibu wa kulipia kidogo kidogo uwekwe na malipo yakikamilika ndipo mtoto aanze kupata huduma,” alisema.
Kuhusu usitishwaji wa Toto afya kadi, mdau wa afya Festo Ngadaya alisema kilichofanywa na NHIF ni kuondoa tatizo kwa kulifuta na sio kuisaidia.
Ngadaya alishauri ili kupata wananchi wengi wanaojiunga na huduma za bima ya afya NHIF wasikae ofisini bali wafuate wananchi kwenye makazi yao.
Naye Crensia Mashauri alishauri ili watoto wengi wawepo kwenye bima ya afya, Serikali ianzishe mfumo maalumu wa kuwaingiza kwenye bima watoto wote wanaozaliwa.
