Kitaifa
Serikali kupitia upya sera, mifumo ya biashara kuvutia uwekezaji

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kujikita na kutekeleza sera yake ya kuvutia uwekezaji nchini sasa inajipanga kutekeleza mfumo wa udhibiti utakaosimamia biashara nchini.
Hayo yamezungumzwa jana Jumatano Septemba 13, 2023 Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji katika kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL), Obinna Anyalebechi.
Waziri Kijaji amesema Serikali iko tayari kufanya mazungumzo na sekta binafsi kama njia ya kutatua changamoto zinazokabili wafanyabiashara huku wakitengeneza mfumo wa kuendelea kuvutia uwekezaji.
“Sekta binafsi ni mdau muhimu katika ujenzi wa taifa. Tunathamini jukumu la sekta hii katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi, mchango wake katika kutengeneza ajira, ukusanyaji wa mapato na misaada kwa jamii,” amesema Dk Kijaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL ameipongeza Serikali kwa kuongeza uhamasishaji katika uwekezaji na biashara nchini.
Obinna amesema SBL imewekeza zaidi ya Sh165 bilioni katika miaka mitatu iliyopita kwa lengo la kuongeza uzalishaji, jambo ambalo limeleta ajira mpya na kuongeza fursa kwa wazalishajiwa ndani kwa kampuni hiyo.
“Upanuzi huu umesababisha kuongezeka kwa uzalishaji na kwa hiyo kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa Serikali kutoka kwa biashara yetu wakati unaimarisha uwezo wa kampuni kufadhili programu za kusaidia jamii zaidi,”amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Programu za kusaidia jamii za SBL kulingana na Obinna, zinajumuisha utunzaji wa maji, upandaji wa miti, na mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana, wanawake, na makundi yanayotengwa.
Hata hivyo, kampuni hiyo pia inaendesha programu ya kilimo inayosaidia zaidi ya wakulima wa ndani 400 wanaolima shayiri, mahindi, mtama na nafaka nyingine ambazo kampuni inanunua na kutumia kama malighafi kwa uzalishaji wa bia.
