Kitaifa
Hizi hapa kada zinazopendwa zaidi na wanafunzi wa kike Chuo Kikuu
Dar es Salaam. Bila shaka katika kipindi hiki wahitimu wa kidato cha sita na stashahada ambao wana mpango wa kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza watakuwa wanatafuta kada sahihi za kusoma katika elimu yao ya juu, Mwananchi Digital imekuandalia kada tano ambazo zinasomwa zaidi na wanafunzi wa kike Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti ya ‘Vitalstats 2022’ inayotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inaonyesha kuwa kada inayoongoza kusomwa na wanafunzi wa kike Vyuo Vikuu nchini ni Ukutubi na uhifadhi makumbusho.
“Uwiano wa wanafunzi wa kiume na kike katika katika masomo ya ukutubi na uhifadhi makumbusho ni 0.64,”imeonyesha ripoti hiyo ambayo maana yake kuwa katika kila wanafunzi watano wanaosoma kada hiyo watatu ni wa kike.
Kada nyingine inayosomwa sana na wanawake ni Sayansi ya Sanaa ambapo uwino wake kati ya wanafunzi wa kiume na kike ni 1. Hii inaamaisha kuwa idadi ya wanafunzi wa jinsia zote inalingana, ambapo wakike walikuwa 13,366 huku wakiume wakiwa 13,693.
Pia, ripoti hiyo inaonyesha kada nyingine inayoongozwa kusomwa na wanawake ni biashara ambapo uwiano kati ya wanafunzi wa kiume na kike ni 1.06, sawa na kulingana kwa idadi ya wanafunzi kijinsia. Wanafunzi wa kike wanaosoma biashara ni 23,483 na wakiume ni 24,914.
Mbali na kada hizo, pia idadi ya wanawake inaonekana kuwa kubwa katika kada za sheria na elimu ambapo wanaume wamezidi idadi ya wanawake kwa achano dogo.
Kwa upande wa masomo ya sheria, wanafunzi wa kike walioandikishwa ni 9,464 huku wa kiume wakiwa 10,082 na masomo ya elimu wanawake ni 27,443 na wanume ni 30,578.
Wakati kada za elimu na sheria zikiwa na achano dogo kati ya wanafunzi wa jinsia hizo mbili hali ni tofauti katika kada ya uhandisi ambapo achano ni kubwa zaidi huku wanaume wakiwa vinara kwa wingi, ambapo katika kila wanafunzi wanne wa kada hiyo watatu ni wanaume.