Connect with us

Kitaifa

Panya wa SUA wapata majukumu bandarini

Bagamoyo. Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), imesema miongoni mwa njia wanazozitumia kudhibiti ujangili na utoroshwaji wa bidhaa zinazotokana na wanyapori ni kukagua mizigo bandarini kwa kutumia panya wenye mafunzo maalumu kutoka Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA).

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Wanyamapori daraja la kwanza wa Tawa, Tryphon Kanon, alipokuwa akitoa mada kwenye semina ya wahariri iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari wa Mazingira Tanzania (Jet), kupitia wa mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (Usaid).

Kanon amesema kukabiliana na ujangili na usafirishaji wa pembe za ndovu na bidhaa nyingine zinazotokana na wanyamapori kunahitaji teknolojia ya kisasa, ndiyo maana kila kukicha wanabuni mbinu mbalimbali za ukaguzi na udhibiti.

“Tunatumia panya waliopewa mafunzo maalumu kukagua mizigo katika bandari zetu, hili tunalifanya kwa kushirikiana na wenzetu wa SUA. Kimsingi, hatuna njia bora ya kufanya ukaguzi kwa kuwa wahalifu wana mbinu nyingi za kufanya uhalifu,” amesema.

Kanoni amesema kutokana na udhibiti unaofanywa na Serikali, wahalifu wamebuni mbinu ya kusaga meno hayo na kusafirisha unga, huku wengine wakitengeneza vito vya aina mbalimbali na kuvisafirisha kwenda nje ya nchi.

Hata hivyo, amesema hatua za kudhibiti ujangili zilizochukuliwa na Serikali kuanzia mwaka 2013 hadi 2022 zimesaidia kupunguza idadi ya tembo wanaouawa kila mwaka kutoka 50 hadi 0.

Amesema mwaka 2016 kulikuwa na kesi za ujangili 3,289 lakini mwaka 2023 zimeshuka hadi 1,213 na kati ya hizo 577 zimeshamalizika.
“Mapambano ya ujangili na uhifadhi yanahusisha jamii, kama haina utayari katika jambo hili hali huwa ngumu kwa kuwa askari wetu hawawezi kuwa katika kila eneo na kila wakati. Tunahitaji jamii itambue ni sehemu ya ulinzi,” amesema.

Meneja ufuatiliaji mradi wa Tuhifadhi Maliasili, John Noronha alisema utoaji wa elimu na upangaji wa matumizi ya ardhi utasaidia kupunguza migogoro ya mipaka inayotokea mara kwa mara.

Amesema wananchi wanapopata elimu ya matumizi sahihi ya maeneo hawatajenga au kufanya shughuli kwenye mapito ya wanyama (shoroba) hivyo hawataathirika na wanyama hao.

“Tutenge na kupanga matumizi ya ardhi, baada ya hapo tuanze kuwapa elimu wananchi wetu juu ya umuhimu wa kuhifadhi maliasili zetu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.

Mwenyekiti wa Jet, Dk Ellen Otaru alisema waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kuhifadhi, kulinda na kutunza maliasili.

“Vyombo vya habari vinaifikia jamii kubwa kwa muda mrefu, vinaaminika hivyo tumeona njia bora ya kufikisha elimu kwa umma ni kuwaelimisha wahariri ili waifikishe elimu hiyo kwa jamii,” amesema.

Mkurugenzi wa Jet, alisema wahariri wakitoa fursa zaidi kwa habari, makala na vipindi vinavyoelimisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira Tanzania itapiga hatua zaidi katika uhifadhi, utunzaji na ulinzi wa mazingira.

Mhariri wa Clouds, Joyce Shebe alisema ni muhimu wanahabari kujengewa uwezo wa mara kwa mara ili kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta husika.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi