Connect with us

Kitaifa

Uzembe, kamari vyatajwa chanzo ajali za barabarani

Dar/Mikoani. Wakati jinamizi la ajali likianza kurejea nchini, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema uchunguzi wa awali unaonyesha uzembe wa madereva ndiyo chanzo.

Ajali hizo zimetokea ikiwa imepita wiki moja tagu Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra), kuyafutia ratiba mabasi yaliyopanga kuanza safari zao usiku wa saa tisa, yakiwamo mabasi sita ya Ally’s Star na matatu ya Katarama Express, huku kampuni inayomiliki mabasi ya Isamilo ikipewa onyo.

Miongoni mwa ajali hizo ni iliyotokea Juni 21, ambapo watu saba walifariki dunia baada ya basi la New Force walilokuwa wakisafiria kupinduka katika Kijiji cha Igando kilichopo wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda Imori alisema chanzo chake kilikuwa dereva wa basi kulipita lori bila kuchukua tahadhari, hivyo likamshinda na kugonga daraja kisha kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi.

Alibainisha kuwa ajali hiyo ilitokea saa nane na nusu mchana likiwa linatokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Rukwa.
Ajali nyingine ilitokea jana katika Kijiji cha Kijomu, Kata ya Hedaru, Wilaya ya Same, ikihusisha basi la Kilimanjaro Express na gari dogo aina ya Toyota Corola na kusababisha vifo vya watu wawili, akiwamo Ofisa wa Jeshi la Uhamiaji Kurasini, Martin Mhagama (45).

Basi lingine la Kampuni ya New Force jana lilipata ajali mkoani Pwani ambapo abiria zaidi ya 40 walinusurika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Pwani, chanzo cha ajali hiyo ni gari dogo lililokuwa likitokea mkoani Morogoro kutaka kuyapita magari mengine eneo la mteremko.

Ajali nyingine za hivi karibuni ni pamoja na iliyotokea mkoani Morogoro Juni 8, na kusababisha vifo vya watu wawili baada ya gari dogo aina ya Toyota Harrier kugongana na lori aina ya Fuso eneo la Melela Mangae, wilayani Mvomero.

Ajali hiyo ilitokea ikiwa ni siku chache tangu kutokea kwa ajali nyingine Juni 5, ambapo basi dogo aina ya Coaster liligongana na lori katika eneo la Iyovi na kusababisha vifo vya watu watano.
Nyingine ilihusisha Noah na lori aina ya Fuso iliyotokea kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’anzi alisema ajali hizo zilizotokea mfululizo zimechangiwa na uzembe wa madereva, ikiwemo mwendo kasi na kupita magari mengine bila kuchukua tahadhari.

“Ukiangalia ajali nyingi zilizotokea zimesababishwa na uzembe wa madereva, mfano hii ya basi iliyotokea Njombe, dereva alikuwa analipita gari lingine kisha gari likamshinda, hivyo hivyo iliyotokea Kibaha, lakini hii ya Kilimanjaro dereva wa gari dogo alikuwa amelala,” alisema Ng’anzi.

Alibainisha kuwa pamoja na uzembe wa madereva, jeshi hilo linaendelea kufuatilia kwa karibu ili kubaini madereva wasiofuata sheria za barabarani na kuwachukulia hatua.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Abdalah Mohammed alisema madereva wao wanajitahidi, huku akitupia lawama magari mengine wanayopishana nayo.

“Sisi kama wamiliki tutaendelea kusisitiza madereva kufuata sheria za usalama barabarani, madereva wa mabasi wanajitahidi sana, ukiangalia hata ajali tatu za hivi karibuni chanzo chake ni magari mengine,” alisema Mohamed.

Wadau waomba kamari kudhibitiwa

Wakati Jeshi la Polisi likiwanyooshea kidole madereva kwa uzembe, imebainika kuwa baadhi ya madereva hushawishika kukimbiza magari na kukosa umakini ili wawahi zawadi za wapambe wanaosubiri maeneo yanakoelekea.

Imeelezwa kuwa, baadhi ya mawakala hucheza kamari kwa kuchangisha fedha ili kuwapa tuzo madereva wa mabasi ya safari ndefu yanayowahi kufika.

Wakizungumza katika stendi kuu ya mabasi ya Nyegezi jijini Mwanza, walisema tabia hiyo siyo tu ni ukiukwaji wa sheria kutokana na mabasi hayo kufika kabla ya muda wa ratiba za safari.

“Huwa wanafanya ubashiri kama ilivyofanyika kwenye michezo ya kubahatisha, huku wakishindana kati ya mawakala wa kampuni tofauti.

“Gari linalofika mwanzo siyo tu hushangiliwa, bali pia humwagiwa maji kama inavyofanyika wakati wa hafla ya kupokea ndege inapotua kwa mara ya kwanza,” alisema Mrisho Said, ambaye ni wakala.

Licha ya kudaiwa kwenda mwendokasi, mabasi yanayoshinda kuwahi kituo cha Nyegezi hupiga honi kwa sauti ya juu, huku wakishangiliwa na madereva bodaboda na wafanyabiashara ndogondogo walioko pembezoni mwa barabara kuanzia eneo la Buhongwa, umbali wa takribani kilomita tatu hadi wanapofika kituoni.

“Tena ushindani huu wa kuwahi kituo cha Nyegezi huwasababishia matatizo ya kujikuta wamepitishwa vituo abiria wanaoshukia njiani katika vituo vya Buhongwa na Mkolani, ambao mara nyingi hupitishwa hadi Nyegezi kwa sababu madereva wanahofia kupitwa wakisimama,” alisema John Madaraka, mmoja wa abiria aliyewahi kupitishwa kituo.

Amina Ally, mmoja wa abiria waliokutwa stendi ya Nyegezi aliiomba Serikali kudhibiti tabia ya madereva kushindana kwa mwendo kasi kuwahi kufika kituo cha mwisho wa safari, kwa sababu tabia hiyo inahatarisha usalama na maisha ya abiria.
“Makundi yanayochochea ushindani huo yadhibitiwe kwa sababu vitendo vyao vinafanyika hadharani,” alisema Amina.

Takwimu za ajali

Ripoti ya ‘Tanzania in figures 2021’ ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaonyesha mwenendo wa ajali za barabarani zimepungua kutoka 2,924 mwaka 2019 hadi 1,864 mwaka 2021, huku ajali 1,933 zikiripotiwa mwaka 2020.

Ajali zinazosababisha vifo zimeongezeka kutoka 1,031 mwaka 2020 hadi 1,038 mwaka 2021.
Vifo vilivyoripotiwa kusababishwa na ajali mwaka 2021 vilikuwa 1,368, sawa na wastani wa kila ajali ilisababisha kifo cha mtu mmoja.

Pia, majeruhi waliotokana na ajali za barabarani wameongezeka kutoka 2,362 mwaka 2020 hadi 2,452 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 3.8.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi