Kitaifa
Mashirika mzigo kitanzani, Samia anoa panga lake
Dar es Salaam. Wakuu wa mashirika ya umma na taasisi ambazo Serikali inamiliki hisa kubwa, wanapaswa kukaa mguu sawa wakati Msajili wa Hazina akikamilisha tathimini ya pili ya ufanisi wake, ambayo Rais Samia Suluhu Hassan amesema ataitumia kufanya uamuzi.
Wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa benki ya NMB Plc yaliyofanyika jana katika ukumbi wa Mlimani City, Rais Samia na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu walieleza juu ya hatua wanazokusudia kuchukua kwa mashirika yanayosuasua kiutendaji.
“Serikali tumeamua kufanya tathimini ya mashirika yetu yote makubwa na yale ambayo tuna hisa nyingi, lengo ni kubaini yasiyo na faida, ambayo yanashindwa kujiendesha na ambayo yanaitia Serikali hasara,” alisema Samia na kuongeza:
“Msajili wa Hazina amefanya tathimini ya awali ameniletea ripoti. Nikamwambia nenda kafanye tathimini ya pili, kwa hiyo wale mnaoshika mashirika TFS (Wakala wa Misitu Tanzania) Dos Santos nakuona, kajitizame vizuri ndani ya shirika lako pamoja na kwamba misitu ni wewe peke yako, kajitizame vizuri”.
Rais alisema ujumbe huo ni kwa wakuu wote wa mashirika, na kwamba hatua hiyo haina kurudi nyuma kwa kuwa kuna yatakayofutwa, kusaidiwa na mengine yatapewa miongozo namna ya kujiendesha ili yote yapate faida.
Alisema Serikali ilianzisha mashirika hayo ili yasaidie kuzalisha mapato na kuisaidia Serikali kubeba mzigo, siyo yenyewe kula serikalini.
“Kwa hiyo msajili vaa njuga, nimekupa baraka zote, nasubiri taarifa ya mwisho ya mashirika gani yanabaki, yapi yanaondoka na yapi yasaidiwe nini kufanya biashara na siku tutakayoyatangaza, yale ambayo tutatoa fedha mfukoni kuyasaidia, nitawaambia hayo mashirika yakifa mfe nayo,” alisema.
Alisisitiza kuwa hatavumilia wala hataki kusikia shirika linazorota, ilhali meneja wake anapiga suti nzuri na kutamba mitaani.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliwataka wenyeviti na maofisa watendaji wa taasisi za Serikali kuhakikisha zinakuwa na matokeo chanya kwa uchumi.
“Siku zote mabadiliko ya uchumi yanakuwa na mtazamo tofauti na vikwazo vingi. NMB ni hadithi nzuri tunaishi leo ikituonyesha tulipotoka. Wakati NMB inaenda kwenye awamu ya pili ya ubinafsishaji wengi walipinga, ikiwamo bodi na ilibidi Rais amtoe mwenyekiti na bodi ivunjwe ili mchakato uendelee.
“Hadi sasa tuna benki ambazo zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, ukienda kwenye bajeti iliyosomwa juzi tumeweka lengo la kuzipa mtaji hizo benki na mimi katika ofisi ya Msajili wa Hazina sijapokea hata senti ya rejesho. Sasa tujiulize, jema ni lipi, tumiliki asilimia 100 halafu tuendelee kutoa kwenye chungu kuwapa hao au twende katika mfumo huu wa NMB?” alihoji na kuongeza kuwa lengo la Serikali ni kuziona taasisi zake zinakua.