Kitaifa
Mikopo wanafunzi vyuo vya kati na ufundi sasa kicheko
Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kufuta ada kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi wanaochaguliwa kutoka kidato cha nne na kuanza kwa utekelezaji wa programu ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati umepokewa kwa kicheko na wadau wa elimu.
Uamuzi huo wa Serikali umekuja ikiwa imepita miezi minne tangu Rais Samia Suluhu Hassan akutane viongozi wa Shirikisho la Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), ambao walimuomba kwa mwaka mpya wa fedha wa 2023/24, Serikali itoe mikopo kwa wanafunzi ngazi ya cheti na stashahada.
Jana, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 alisema kuanzia mwaka ujao wa masomo kutakuwa na programu ya mikopo kwa wanafunzi waliochaguliwa katika vyuo vya kati katika fani za kipaumbele ambazo ni sayansi, afya, ufundi na ualimu.
Alisema Serikali inalenga kutoa elimu ya amali kwa ngazi zote kuanzia shule za awali, ambayo itamwezesha kijana wa Kitanzania kujiajiri au kuajiriwa na hivyo, kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa.
“Napendekeza kuondoa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga na vyuo vya ufundi vya DIT (Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam), MUST (Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).
“Hatua hii inalenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi na elimu inayohitajika katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya viwanda. Bajeti hii inaonyesha namna Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) anavyotaka kuwasaidia watoto wa maskini. Pochi ya mama imefunguka. Mama yuko kazini,” alisema Mwigulu.
Akizungumzia hatua hiyo, mhadhiri wa Chuo cha St John’s, Shadidu Ndosa alisema ni uamuzi mzuri katika kufanikisha utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda.
“Ili ufanikiwe kwenye uchumi wa viwanda ni lazima uwe na Watanzania wenye ujuzi na wanaofanya kazi, si wa kusimamia. Hapa namaanisha mafundi mchundo na wengine ambao ndio wanahusika moja kwa moja kwenye uzalishaji.
Hatua ya Serikali kuwapa mikopo na kuwafutia ada itaongeza hamasa ya vijana wengi kwenda huko na tutatengeneza wataalamu wengi na matokeo yake itakuwa kuongeza uzalishaji,” alisema Ndosa.
Umeme nchi nzima
Kwa upande wa nishati, Waziri Mwigulu alisema kuwa Serikali imetenga Sh903.8 bilioni ili kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwaka 2025, akifafanua kuwa hadi sasa zaidi ya asilimia 81 ya vijiji vimefikiwa na nishati hiyo.
“Serikali ya CCM inaendelea na usambazaji wa umeme vijijini ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, vijiji vyote viwe vimefikiwa. Katika kufikia azma hiyo, hadi Aprili 2023 kiasi cha Sh903.8 bilioni kimetolewa,” alisema.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kutaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme kwenye maeneo yote nchini, ikiwemo maeneo ambayo hayakuwa yameunganishwa na gridi ya Taifa kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita kushika hatamu za uongozi.
“Kukamilika kwa miradi hiyo kutaiwezesha nchi yetu kuanza kuuza umeme nje ya nchi na kuliingizia Taifa letu fedha za kigeni,” alisema.
Akitaja mafanikio katika sekta ya nishati, Dk Mwigulu alitaja ujenzi miradi ya Julius Nyerere (MW 2,115) ambao alisema hadi Aprili 2023 umefikia asilimia 86.89 na Rusumo (MW 80) aliosema umefikia asilimia 99 pamoja na kukamilika kwa mradi wa uzalishaji wa umeme kwa gesi wa Kinyerezi I Extension (MW 185).
Pia alitaja uimarishaji wa miundombinu ya usambazaji wa umeme kwa kuunganisha katika gridi ya Taifa mkoa wa Kigoma (Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu na Buhigwe) pamoja na wilaya za Ngara na Biharamulo za mkoa wa Kagera.
“Katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme katika vijijini na baadhi ya ngazi za vitongoji. Hii ni ishara kwamba mama amedhamiria kufikisha umeme nchi nzima,” alisema.
Arekebisha tozo za utalii
Kwenye sekta ya utalii, Dk Mwigulu alipendekeza kufanyika kwa marekebisho ya ada na tozo mbalimbali kwenye sekta ya utalii.
Katika marekebisho hayo, alisema watafuta ada ya kupanga na kurudia kupanga (grading and regrading) huduma za malazi zilizo nje na ndani ya maeneo ya hifadhi.
Pia amependekeza kupunguzwa kwa viwango vya ada ya leseni ya biashara ya utalii katika huduma za malazi zinazomilikiwa na Watanzania kutoka Sh5.7 milioni hadi Sh3.4 milioni kwa hoteli za nyota tano.
Kwa upande wa hoteli za nyota nne, alisema ada zipungue kutoka Sh4.6 milioni hadi Sh2.3 milioni, huku nyota tatu zikipungua kutoka Sh3.4 milioni hadi Sh1.1 milioni na za nyota mbili kutoka Sh2.9 milioni hadi Sh690,000 wakati nyota zitatoka Sh2.3 milioni hadi Sh460,000.
Pia alisema kupunguzwa kwa ada ya leseni ya utalii kwa huduma za malazi ambazo hazijakaguliwa na kupangwa katika viwango vya ubora nje ya maeneo ya hifadhi kutoka Sh2.3 milioni hadi Sh690,000.
Hata huduma ya malazi yanayopatikana katika makazi ya mtoa huduma, zitapunguzwa kutoka Sh920,000 hadi Sh230,000.
Waziri Mwigulu alipendekeza kupunguza ada kwa upande wa hosteli kutoka Sh920,000 hadi Sh460,000.
Akitoa maoni yake katika punguzo hilo la ada, Meneja ushirikishwaji Mradi wa USAID, Tuhifadhi Maliasili, Dk Elikana Kalumanga, alisema hii itasaidia kuondoa vikwazo katika uendelezaji wa sekta ya utalii.
“Kuondolewa kwa ada kutapunguza migogoro ambayo inaendelea kwa kuwa itatoa fursa kwa wakazi wa maeneo ya jirani na hifadhi kwa kuwahamasisha kujenga sehemu za kufikia watalii.
“Royal Tour imezaa matunda, hivyo kupunguza baadhi ya ada zinakwenda kukaribisha zaidi watalii kwa kupata nafuu ya malazi pindi watakapokuwa katika utalii, maana si wote wana uwezo wa kulala katika hoteli zenye nyota,” alisema Dk Kalumanga.
Nywele bandia, nepi juu
Kwa watumiaji wa nywele bandia kutoka nje, inaweza kuwa bajeti mbaya kwao kutokana na kuongezeka kwa ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35.
Pia kuna ongezeko la ushuru wa forodha kwa nepi za watoto zinazoingizwa kutoka nje ya nchi, kutoka asilimia 25 hadi 35.
Hata hivyo, Waziri Mwiguli alipendekeza kuondoa ushuru wa forodha kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye malighafi za kutengeneza nepi hizo za watoto.
Alisema hatua hii inalenga kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji na kuongeza uzalishaji wa ndani na kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo nchini, kuongeza ajira na mapato ya Serikali.