Kitaifa
NHIF yasajili wanafunzi 342,933 bima ya afya
Dodoma. Serikali imesema hadi kufikia Machi 2023, imesajili jumla ya wanafunzi 342,933 ambao wanatoka shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati na kuwaingiza katika mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Juni 15, 2023 na Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Lucy Sabu.
Katika swali lake mbunge huyo ametaka kujua kuna mpango gani wa kuwasajili wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Kati kwenye utaratibu wa Bima ya Afya ya NHIF.
Mbunge huyo pia ameuliza ni utaratibu upi unatumika kuwasajili wanafunzi wengi ikiwa suala hilo haliko kisheria.
Naibu Waziri amesema zoezi la kusajili wanafunzi ni endelevu kupitia shule na vyuo na kwamba elimu zaidi inaendelea kutolea ili wengi wasajiliwe na kupatiwa vitambulisho.
“Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeanzisha mpango wa bima ya afya kwa wanafunzi wa ngazi zote kwa kuchangia Sh50,400 kwa mwaka ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu wakiwa masomoni, likizo na wakati wa mafunzo kwa vitendo,” amesema Dk Mollel.
Hata hivyo Waziri amesema kuwa kazi kubwa iliyo mbele ni kwa wabunge na Watanzania wote kuhakikisha wanaupigania muswada wa bima ya afya kwa wote uweze kurejeshwa tena bungeni kwani itajibu matatizo yote.