Kitaifa
THRDC yasaini mkataba wa Sh3.4 bilioni na Sweden
Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesaini mkataba wa miaka mitatu na Sweden wenye thamani ya Sh3.2 bilioni kwa ili kusaidia utekelezaji wa mipango mikakati wa taasisi hiyo.
Makubaliano hayo yamesainiwa rasmi leo Juni 2, 2023 na utekelezaji wake utaanza mapema mwezi huu na kumalizika Desemba 31, 2026.
THRDC na Sweden wamekuwa na ushirikiano kwa zaidi ya miaka 10 tangu mtandao huo uanzishwe ambapo Ubalozi wa Sweden hapa nchini ulivutiwa na kazi zake na kuamua kuwa mdau wake mkubwa.
Taarifa iliyotolewa na THRDC leo imesema lengo kuu la mipango hiyo ni kuboresha mazingira kwa watetezi wa haki za binadamu kuendelea kutoa msaada wa haraka ikiwemo msaada wa kisheria pale wanapopitia mazingira hatarishi.
“Kusaidia watetezi wakiwa katika shughuli zao za utetezi na kutafuta fursa za majadiliano na mashirikiano baina ya watetezi wa haki za binadamu na taasisi mbalimbali za ndani na nje zikiwemo za kiserikali na zisizo za kiserikali,” imesema taarifa hiyo.
Pia taarifa hiyo imesema, fedha hizo zitawezesha kuwajengea uwezo watetezi wa namna ya kutekeleza kazi zao za utetezi na kujilinda wanapopitia changamoto, lakini pia kuwajengea uwezo asasi za kiraia kuhusu haki na wajibu wao ikiwemo swala la kuzingatia sheria zinazowahusu.
“Pia zitawezesha kukuza ustawi na ujenzi wa taasisi kwa kuchangia moja kwa moja kwenye kutekeleza malengo ya Mpango mkakati mpya wa Mtandao huo.”