Connect with us

Kitaifa

‘Drones’ sasa kuchunguza visumbufu mimea shambani

Dar es Salaam. Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imesema wahitimu 20 wa kozi ya ndege zisizo na rubani ‘drones’ watakuwa msaada mkubwa katika kufanya uchunguzi ili kubaini visumbufu vya mimea katika maeneo mbalimbali.

Hayo yameelezwa  leo Mei 25 na  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Nduguru wakati wa mahafali ya wahitimu hao yaliyofanyika viwanja vya makao makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Amesema hatua hiyo italeta tija katika sekta ya kilimo kwa kuboresha uzalishaji na mavuno kwa wakulima nchini.

Amesema mwaka 2017 Umoja wa Ulaya (EU) ilifanya ukaguzi nchini kuhusu huduma za afya ya mimea nchini na kubaini upungufu ikiwemo ukosefu wa ufuatiliaji wa taarifa za visumbufu vya mazao.

“Kama mnavyojua wale wanaofanya utafiti kuhusu changamoto za mimea kuna maeneo mengine sio rahisi kuyafikia iwe kwa gari au miguu. Lakini kupitia drones hizi zitakazotumiwa na watalaamu maeneo hayo yatafikiwa na kupata taarifa zinazohitajika kufanyiwa uamuzi utakaoimarisha afya za mimea,” alisema Profesa Nduguru.

Hata hivyo, Profesa Ndunguru amesema utafiti wa kubaini visumbufu mimea ni moja kati ya kazi za mamlaka za afya ya dunia na matokeo yanayotokana na mchakato huo yanayotoa msingi wa ufahamu wa masharti ya vipaumbele vya kuzingatia kazi mbalimbali.

Amesema miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na kudhibiti visumbufu, usafirishaji na uingizwaji wa mazao ya kilimo, uanishwaji wa maeneo huru ya visumbufu na utokomezaji wa visumbufu sambamba na ufahamu wa hali hiyo nchini.

Mwakilishi Mkazi wa FAO nchini, Nyaberi Tippo amewapongeza wahitimu hao, akisema hatua hiyo ni muhimu na itakwenda kusaidia uchunguzi wa mimea hatarishi na magonjwa ya mimea.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kilimo na Usalama wa Chakula, Zanzibar, Hamad Masoud Ali amesema eneo hilo ni muhimu na litakwenda kuimarisha sekta hiyo na kwamba changamoto za mimea za Tanzania na visiwani zinashabiana.

Mafunzo hayo kwa watalaamu hao yameratibiwa na kuwezeshwa na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Chakula Duniani (FAO), kwa ushirikiano na Serikali.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi