Kitaifa
Rais Samia: Tanzania inang’ara uwekezaji rasilimali watu
Dar es Salaam. Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya vizuri katika kuvutia uwekezeaji wa rasilimali watu kwenye sekta za afya, elimu na huduma nyingine za kijamii, kama sehemu ya kuchochea ukuaji wa uchumi.
Haya yamebainishwa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Mei 19 2023, ambapo amezindua maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu uwekezaji rasilimali watu na hivyo hivyo kujibu hitaji la nguvu kazi hiyo utakaofanyika baadaye mwezi.
Mkutano huo utawaleta pamoja wakuu wa nchi na Serikali za Afrika kubadilishana uzoefu na kutoka na azimio la pamoja juu ya namna ya kuboresha uwekezaji huo barani Afrika.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Samia amesema mkutano huo utakuwa jukwaa la kipekee kwa wakuu wa nchi za Afrika kubadilishana uzoefu juu ya namna ya kuwezesha nguvu kazi katika mataifa yao.
“Uwekezaji rasilimali watu ni muhimu, Tanzania tumejitahidi sana katika uwekezaji huo kuanzia sekta za afya, elimu na huduma nyingine za jamii,” amesema Rais Samia.
Taarifa kutoka Benki ya Dunia ambayo inaratibu mkutano huo zinasema kuwa, utaangazia jukumu la rasilimali watu katika ukuaji wa uchumi na pia utaibua mjadala juu ya umuhimu wa kuwekeza kwa watu.
Aidha, mkutano huo utahimiza majadiliano ya kiufundi, kushirikishana maarifa ya sasa kuhusu mitaji watu na baadaye kuhitimishwa na maazimio madhubuti yenye kuonyesha hatua zinazofuata kutoka kwa wakuu wa nchi wanaoshiriki.
Mada kuu katika mkutano huo ni ufungamanishwaji wa rasilimali watu na ukuaji wa uchumi, na kutumia mgao wa idadi ya watu, kushughulikia uduni wa maisha, lakini pia pengo la ujuzi kwa vijana na wanawake.
Umaskini wa kujifunza ni sehemu ya watoto umri chini ya miaka 10 wasioweza kusoma na kuelewa maandishi rahisi ambapo kwa Afrika, wanakadiliwa kufikia asilimia 89.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema nguvu kazi inaanzia kwenye afya ya mtoto anapokuwa tumboni hadi anapozaliwa na kukua.
Amesema baada ya hapo uwekezaji unahamia kwenye elimu pamoja na sekta nyingine zinazomwezesha kijana kufanya kazi.
“Tanzania tumeona ni jambo la msingi kuwa wenyeji wa mkutano huu wa viongozi wa Afrika na tunatarajia utakuwa na mafanikio makubwa hasa katika kutafuta majawabu ya namna ya kuwekeza zaidi kwenye rasilimali watu,” amesema Dk Mwigulu.