Connect with us

Kitaifa

Sh157 milioni zawapa tabasamu wanafunzi Geita

Geita. Wanafunzi zaidi ya 200 wanaotoka Kijiji cha Nyakagwe Wilaya ya Geita wameondokana na adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 16 kwenda na kurudi shule ya Sekondari ya Butobela baada ya Serikali kujenga shule mpya ya Sekondari Nyakagwe.

Kutokana na mazingira, Serikali pia imejenga bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa shule hiyo iliyoko Kata ya Nyakagwe Wilaya ya Geita lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 80

Wanafunzi 194 walioanza kidato cha kwanza mwaka huu ni miongoni mwa wanufaika wa uamuzi wa Serikali kwa kushirikiana na wananchi wa kutekeleza mradi wa ujenzi wa shule mpya na bweni la wanafunzi wa kike kwa gharama ya zaidi ya Sh157 milioni kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzinduzi wa bweni la wasichana, Ofisa Mtendaji Kijiji cha Nyakagwe, Ruben Makala amesema kukamilika kwa mradi huo siyo tu umewaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, bali pia utapunguza tatizo la utoro na mimba zinazotokana na vishawishi wakati wa kwenda na kurudi shule.

Kwa mujibu wa takwimu za idara ya elimu Geita, zaidi ya wanafunzi 100 wa shule ya sekondari Butobela walibainika kuwa watotoro kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2021/22, huku umbali wa kutembea kwenda na kurudi shule, mito kujaa maji nyakati za masika na shughuli za kiuchumi zikitajwa kuwa miongoni mwa sababu.

Ofisa mtendaji huyo ameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kutatua changamoto ya kukosekana kwa huduma ya umeme na maji na kujenga uzio kulinda usalama wa mali na jumuiya ya shule hiyo.

Diwani wa Kata ya Nyakagwe, Charles Kazungu ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi wa vyumba 15 vya madarasa katika shule za kata hiyo ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari za umma.

‘’Kwa miezi 10 iliyopita, Serikali imetoa zaidi ya Sh11 bilioni kutekeleza miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na mabweni katika shule mbalimbali wilayani Sengerema,’’ amesema Magembe

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuzindua bweni la wasichana shule ya sekondari Nyakagwe ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Geita kutumia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) kutoka kampuni GGM kufunga umeme jua shuleni hapo ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi