Kimataifa
Polisi yafukua makaburi 12 waliofariki wakiaminishwa kwenda mbinguni
Kilifi. Jeshi la Polisi nchini Kenya limefukua mabaki ya watu kutoka kwenye yanayodhaniwa kuwa ni makaburi zaidi ya 12 mashariki mwa nchi katika uchunguzi dhidi ya wafuasi wa dhehebu moja la Kikristo ambao waliamini kuwa wangeenda mbinguni ikiwa wangejiua kwa njaa.
Polisi walianza kutoa miili Ijumaa iliyopita, alisema Charles Kamau, mpelelezi katika mji wa Malindi karibu na msitu wa Shakahola uliopo kaunti ya Kilifi, ambapo polisi waliwaokoa waumini 15 wa Kanisa la Good News International wiki iliyopita, kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Citizen TV.
Vyanzo kutoka ndani ya jeshi hilo viliiambia AFP iliyopita kwamba miili 21 imepatikana hadi sasa na kwamba mingine zaidi inaweza kugunduliwa.
“Kwa jumla tangu jana, tuna miili 21,” chanzo cha polisi kiliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina.
“Hatujakwangua sehemu ya juu ya ardhi ambayo inatoa dalili wazi kwamba tunaweza kupata miili zaidi ifikapo mwisho wa shughuli hii,” chanzo kiliongeza. Chanzo cha pili cha polisi kilithibitisha idadi hiyo hiyo, pia kwa sharti la kutotajwa jina, AFP iliripoti.
Kituo cha televisheni cha NTV cha nchini Kenya kiliripoti Jumamosi iliyopita kwamba miili saba ilitolewa kutoka kwenye makaburi mawili kati ya 32 yanayoshukiwa na kuwa yamewekwa alama na polisi.
Kiongozi wa kanisa hilo, Paul Mackenzie, ambaye pia alitambuliwa katika taarifa kama Paul Nthenge Mackenzie, alikamatwa, shirika la habari la Reuters liliripoti. Wakili wa Mackenzie hakuweza kupatikana mara moja ili kutoa maoni yake.
NTV iliripoti kwamba Mckenzie amefanya mgomo wa kula akiwa mahabusu tangu kukamatwa kwake wiki iliyopita.
Polisi walisema waumini 15 waliookolewa walikuwa wameambiwa wajiue kwa njaa ili waweze kukutana na muumba wao. Wanne kati yao walikufa kabla ya kufika hospitalini.
Titus Katana, mshiriki wa zamani wa kanisa hilo, aliisaidia polisi kutambua makaburi hayo.
“Tumewaonyesha polisi makaburi, na zaidi ya hayo, tumeokoa maisha ya mwanamke ambaye alikuwa amebakiwa na saa chache tu, vinginevyo angekufa,” Katana aliambia televisheni ya Citizen.
Matthew Shipeta kutoka Haki Africa, shirika linalotetea haki za binadamu, alisema aliona angalau makaburi 15 ya kina kifupi katika msitu huo.
Helen Mikali, meneja wa nyumba ya watoto ambaye pia alikuwa akisaidia wachunguzi, alisema alitembelea vijiji kadhaa vya karibu ambapo wazazi na watoto walitoweka.
“Binafsi nimetembelea takriban makaburi 18 ya watoto,” Mikali aliiambia Citizen TV. Hata hivyo, hakusema alijuaje makaburi hayo yalikuwa na mabaki ya watoto.
Mwezi uliopita polisi walimkamata na baadaye kumwachia Mackenzie kwa kuwahimiza wazazi wa wavulana wawili kufa njaa na kukosa hewa kwa watoto wao hadi kufa.