Kimataifa
Polisi yawadhibiti waandamanaji Kenya, maduka mitaani yafungwa
Nairobi. Wakenya wamefanya tena maandamano leo Jumatatu Machi 27, 2023 kwa mara nyingine dhidi ya serikali kupinga kupanda kwa gharama za maisha, baada ya upinzani kuapa kuwa maandamano hayo yatafanyika licha ya marufuku ya Jeshi la Polisi.
Usalama umeimarishwa huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwa katika maeneo ya kimkakati jijini Nairobi na kufanya doria mitaani, huku maduka mengi yakiwa yamefungwa na huduma za treni kutoka viunga vya mji mkuu hadi katikati ya jiji zimesitishwa.
Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga amewataka watu kujitokeza barabarani kila Jumatatu na Alhamisi, hata baada ya maandamano wiki moja iliyopita kuwa na vurugu na kuathiri shughuli baadhi ya sehemu za Nairobi.
Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Kenya (IGP), Japhet Koome aliwaambia waandishi wa habari Jumapili Machi 26, 2023 kwamba maandamano hayo ni “haramu” na yamepigwa marufuku.
Wakati wa mapigano ya Jumatatu iliyopita, mwanafunzi wa chuo kikuu aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi, huku maofisa 31 wakijeruhiwa wakati wa mapigano kati ya polisi wa kutuliza ghasia na waandamanaji mjini Nairobi na ngome za upinzani Magharibi mwa Kenya.
Zaidi ya watu 200 walikamatwa, wakiwemo wanasiasa kadhaa wakuu wa upinzani, huku waandamanaji pamoja na msafara wa Odinga mwenyewe wakipigwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kuzuka kwa machafuko ya kisiasa tangu Rais William Ruto aingie madarakani zaidi ya miezi sita iliyopita baada ya kumshinda Odinga katika uchaguzi ambao mpinzani wake anadai “ameibiwa”.
Licha ya marufuku ya polisi, Odinga alitoa wito jana Jumapili kwa Wakenya kujiunga na kile alichokitaja kuwa “mama wa maandamano yote”.
“Ninataka kumwambia Ruto na IGP Koome kwamba hatutatishika,” alisema. “Hatutaogopa mabomu ya machozi na polisi.”
Odinga pia alimshutumu Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua kwa kuandaa operesheni ya kusababisha “ghasia” katika maandamano ya leo.
Wakazi wa Nairobi walikuwa na wasiwasi baada ya ghasia za awali.
“Itabidi na mimi nifunge pia kwa sababu nimeona majirani zangu wengi wamefunga biashara zao,” amesema Mercy Wangare, mhudumu wa kibanda cha Mpesa katika duka la vifaa vya elektroniki.
“Ninapima tu hali itakavyokuwa kabla sijaamua kwa sababu kuwaona polisi hawa wakifanya doria ni ishara kwamba mambo hayatakwenda vizuri.”
Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya imejaribu kuzuia vituo vya televisheni kutangaza moja kwa moja maandamano hayo, lakini hatua hiyo ilizuiwa na Mahakama Kuu.
Ruto ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi kwa safari ya siku nne nchini Ujerumani na Ubelgiji, amemtaka mpinzani wake kusitisha hatua hiyo.
“Ninamwambia Raila Odinga kwamba ikiwa ana shida nami, anapaswa kunikabili na aache kutia hofu nchi,” alisema Ruto Alhamisi iliyopita.
“Acheni kudumaza biashara za mama mboga, matatu na Wakenya wengine,” alisema Ruto akimaanisha. wafanyabiashara wanawake na waendeshaji wa mabasi madogo ya binafsi.
Wakenya wengi wanashindwa kupata chakula, wakipambana na gharama kubwa za bidhaa za msingi pamoja na kuporomoka kwa sarafu ya nchi hiyo na ukame mkubwa uliowaacha mamilioni ya watu na njaa.
Wakati wa kampeni za uchaguzi, Ruto alijipambanua kama bingwa wa kupigania haki za wanyonge na kuapa kuboresha maisha ya Wakenya wa kawaida.
Hata hivyo, wakosoaji wanasema amekiuka ahadi zake kadhaa za kampeni na ameondoa ruzuku kwenye mafuta na unga wa mahindi ambao ndiyo chakula kikuu cha Wakenya.