Kitaifa
Luhemeja awatahadharisha Dawasa upatikanaji wa maji Dar

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mku Wizara ya Maji, Cyprian Luhemeja amewatahadharisha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (Dawasa) endapo hawata kuwa makini ifikapo 2025, kiwango cha maji kitapungua hadi asilimia 80.
Luhemeja ambaye alikuwa Mtendaji Mkuu wa Dawasa kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu alitoa tahadhari hiyo jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha siku 365 za mama awamu ya pili kilichorushwa na kituo cha Clouds media.
Alisema mkoa wa Dar es Salaam ni mji mkubwa wa kibiashara unaochangia kwa asilimia 75 ya mapato na kwa sasa maji yanapatikana kwa asilimia 95.
“Dawasa kuweni makini mwaka 2023 maji yanapatikana kwa asilimia 95, ukipiga hesabu 2025 kama hamna kazi mnayofanya tutakuwa asilimia 80,”alisema Luhemeja.
Alibainisha kuwa mkoa huo unakuwa kwa kasi sana, hivyo ni lazima wawe na kasi itakatyoendana na kukuwa kwa mji kama endapo watataka kuwa na viwango sawa.
“Kazi kubwa inafanyika yamebaki maeneo machache ikiwemo Mwanagati, Kitunda, Kivule na Chamanzi ambapo tayari 40 biioni zimetengwa kwaajili ya kufanya usambazaji kwenye maeneo hayo.
Akizungumzia miradi ya maji iliyokamilika vijijini Luhemeja alisema miradi 382 imekamilika na zaidi ya watu 2 milioni wanapata maji huku vituo 3,400 vikijengwa kwenye vijiji 684.
Kwa upande wake waziri wa wizara hiyo, Juma Awesso alisema kila mwaka mvua zimekuwa zikinyesha lakini maji yamekuwa yakipotelea baharini na wakati mwingine kusababisha changamoto.
“Kwanini tuyaruhusu maji yaingie baharini halafu tutumie garama nyingi kuyabadilisha kwanini tusuichimbe mabwawa makubwa ya kuhifadhia maji,”alihiji Waziri Awesso.
Alibainisha kuwa uzoefu tulioupata kupitia mabadiliko ya tabia ya nchi iwe funzo, nakuwataka wananchi kulinda na kutunza rasilimali za maji.
