Kitaifa
Rais Samia ‘kumfutia’ Lema kesi kwazua gumzo
Dar es Salaam. Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kumfutia kesi Godbless Lema imewaibua wanasheria wanaosema inashusha hadhi ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), wakitaka mfumo wa haki jinai ufumuliwe ili kuilinda.
Maoni ya wanasheria hao yanazingatia Ibara ya 59B hususan kifungu cha nne kinachosema: “Katika kutekeleza mamlaka yake, Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au na mamlaka yoyote na atazingatia, nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki, na maslahi ya umma.”
Akiwasalimia wakazi wa Usa River mkoani Arusha juzi, Rais Samia alisema Lema alipotaka kurudi nchini alimuuliza kuhusu kesi zake na akamwambia atazifuta.
“Kwa hiyo mdogo wangu amerudi, aliniambia mama nataka kurudi nikamwambia rudi, akasema mama nina kesi nikamwambia nazifuta, rudi. Amerudi tuimarishe siasa, si ndio?” alihoji Rais.
Lema aliyerudi nchini Machi mosi tangu alipokimbia Novemba 2020 kuelekea Canada, amekuwa akimshukuru Rais Samia kwa kubadilisha hali ya siasa nchini.
Akizungumza juzi wilayani Karatu mkoani Arusha, Lema alisema “nataka nitumie fursa hii kumshukuru, lakini afikirie jambo moja, mimi ni kiongozi wa kisiasa, viongozi wangu ama mimi mwenyewe nimepata fursa ya kupigania haki yangu lakini wapo masikini wengi magerezani ambao wamebambikiwa kesi, hawawezi kuwa na access ya kukufikia wewe, wala wazazi wao, hawa wanahitaji Katiba mpya na sheria bora.”
Katiba inavunjwa
Akiizungumzia kauli ya Rais Samia, Wakili Jebra Kambole alisema Ibara ya 59B(4) ya Katiba inaunda ofisi ya DPP na kutaka iwe huru, isiingiliwe na mtu wala mamlaka yoyote.
“DPP anafanya kazi kwa niaba ya Watanzania sio Serikali wala Rais na walalamikaji ni wananchi si Serikali. Ndiyo maana DPP anatakiwa kuwa huru, anashtaki, anaendesha mashitaka, anafuta kwa niaba ya wananchi, siyo kwa niaba yake, Rais wala Serikali,” alisema Kambole.
Kwa nafasi yake, alisema Rais anaweza kumteua DPP au kumwondoa wakati wowote hata kutumia madaraka yake kutoa maagizo kwa ofisi ya DPP.
Chanzo cha udhaifu huo alisema ni Katiba japo inatoa ulinzi kwa DPP na ofisi yake kuachwa huru. “Kwa sababu hii Katiba imempa Rais mamlaka ya kumteua na kumwondoa DPP, lakini Katiba hiyohiyo inamlinda DPP asiingiliwe na mtu yeyote. Kwa hiyo tuna tatizo la Katiba na la kiutendaji. Rais asingetoka hadharani na kusema amemfutia Lema kesi, hiyo haikuwa sawa,” alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu madaraka ya DPP, Kambole alisema masilahi ya kesi ni ya wananchi na yamekaimishwa kwa DPP.
“Ukisema mwanao amebakwa na unataka DPP afute kesi, haiwezi kufutwa kwa sababu ukibaka unaiathiri jamii sio mtu mmoja. Au mtu akifanya mauaji, mtu akasema hata kama ameua sisi hatuna shida naye, haiwezekani kwa sababu madhara yanakwenda kwa jamii,” alisema Kambole.
Kuhusu uhuru wa DPP, alisema utalindwa vizuri endapo nafasi hiyo itaombwa kwa ushindani.
“Kwa mfano Kenya, DPP anakaa miaka minane. Kwa kipindi chote hicho hawezi kuondolewa labda afanye makosa ya jinai na baada ya miaka minane, hatakiwi kupata kazi Serikalini,” alisema Kambole.
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Rugelemeza Nshala naye alisema Katiba iko wazi.
“Inawezekana ni kuteleza tu au kujipatia sifa kidogo na kuchangamsha watu. Kisheria anayefuta kesi ni DPP, Rais anaweza kuzungumza kisiasa au inaweza kuchukuliwa kuwa ameteleza ndiyo maana kwa sasa tunazungumzia mfumo wa haki jinai ufumuliwe. Wote umeoza kwa hiyo huwezi ukatibu uozo kwa kupachikapachika tu, unachotakiwa pengine ni kufukua wote unakwenda unazika,” alisema.
Juhudi za kumpata DPP, Slyvester Mwakitalu hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita bila kupokelewa huku wasaidizi wake wakisema yupo kwenye kikao cha kikazi.
Akizungumza katika jukwaa la Club House jana asubuhi, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema kauli ya Rais haikumaanisha kwamba taratibu hazikufuatwa.
“Si kesi za Lema pekee, huwa mnaona mahakama mara nyingi ama inatupilia mbali kesi au anakwenda DPP anaifuta kesi. Rais akisema nimemfutia Lema kesi haina maana kwamba alitoka mahali akaenda akafuta hiyo kesi, hapana, ile ni lugha ya mazungumzo. Pengine tulizitazama kesi zake tukauliza, ninyi mnao ushahidi wa jambo hili? Hapana, ondoeni hiyo kesi, sasa ile ondoeni hiyo kesi haina maana kwamba wanaamka asubuhi wanaiondoa. Lazima ule utaratibu iufuatwe,” alisema Dk Tulia.
Kesi za Lema
Lema alikuwa anakabiliwa na kesi namba 63/2020 iliyokuwa na mashtaka 15 likiwamo la kusababisha taharuki kwa jamii baada ya kusambaza taarifa zinazodaiwa kuwa za upotoshaji kuhusu mauaji ya watu 14 wilayani Manyoni mkoani Singida. Alidaiwa kutenda makosa hayo Februari 29 mwaka 2020 wilayani Manyoni kwenye mazishi ya kiongozi wa Chadema.
Aprili 27 mwaka 2018 Mahakama ya Wilaya ya Arusha ilimwachia huru Lema aliyekuwa akituhumiwa kwa uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli baada ya Jamhuri kushindwa kupeleka ushahidi.
Hata hivyo, baada ya kuachiwa, alikamatwa tena na kusomewa mashitaka ya kutoa lugha zenye kujenga hisia mbaya ambayo aliyakana.