Connect with us

Kimataifa

40 wafariki dunia katika ajali ya treni Ugiriki

Watu 40 wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha treni ya abiria na treni ya mizigo kugongana uso kwa uso nchini Ugiriki usiku wa Jumanne.

Wengi wa waathiriwa wanadhaniwa kuwa wanafunzi wa chuo kikuu waliokuwa wakirejea kutoka likizo. Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka zaidi, maafisa wamesema.

Treni ya abiria iliyokua inasafiri kutoka Athens hadi mji wa kaskazini wa Thessaloniki, na treni ya mizigo iliyokuwa njiani kutoka Thessaloniki kuelekea Larissa ziligongana uso kwa uso nje ya mji wa Tempe muda mfupi kabla ya saa sita usiku jana Jumanne.

“Ni janga lisiloweza kuelezeka,” msemaji wa serikali, Yiannis Oikonomou, aliwaambia waandishi wa habari. “Mawazo yetu yako kwa jamaa za waathiriwa, waliopotea na waliojeruhiwa.”

Mkuu wa kituo cha eneo hilo, anayehusika na utoaji wa ishara katika kuongoza treni amekamatwa, afisa wa polisi amesema, wakati wapelelezi wakijaribu kujua ni kwa nini treni hizo mbili zilikuwa kwenye njia moja.

Saa chache baada ya ajali hiyo, kikosi cha zima moto cha Ugiriki kimesema watu 66 kati ya watu 85 waliojeruhiwa katika ajali hiyo wamepelekwa hospitalini karibu na Larissa. Sita wako katika uangalizi mahututi.

Wengi wa waathiriwa walielezewa kuwa wanafunzi ambao walikuwa wamekusanyika katika mabehewa mawili ya kwanza.

“Abiria wengi hawakuelewa ni nini hasa kilikuwa kimetokea kwa sababu walikuwa wamelala,” manusura mmoja amenukuliwa akiliambia shirika la habari la serikali, ANA-MPA.

“Nilikuwa nimelala pia, na mlio mkubwa ulinitikisa niliamka. Tulipogundua kilichotokea, tulijaribu kutoka nje ya mabehewa, na tulipofanikiwa, tuliona machafuko,” ameongeza manusura huyo.

Roubini Leontari, mchunguzi mkuu katika hospitali kuu ya Larissa, ameambia vyombo vya habari vya ndani kuwa miili 35 “hivi sasa iko katika chumba cha kuhifadhia maiti wakati uhamisho wa miili mingine ukiendelea”.

Amesema baadhi ya miili ilichomwa kiasi cha kutotambulika na mingi ilikuwa ya vijana.

“Tunajikuta mbele ya janga lisilo na maana,” rais wa Ugiriki, Katerina Sakellaropoulou, amesema katika taarifa. “Hasa tunaomboleza vijana.”

Katerina ametangaza kuwa atakatisha ziara rasmi nchini Moldova ili kurejea Ugiriki, ambako kipindi cha siku tatu cha maombolezo kilitangazwa rasmi.

Akitembelea eneo la mkasa huo, waziri mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, amesema jukumu kubwa zaidi sio tu kuwatibu waliojeruhiwa na kutambua miili bali kupata undani wa jinsi mkasa huo ulivyotokea.

“Kuna jambo moja tu ambalo ninaweza kuhakikisha: tutajua sababu ya mkasa huo na tutafanya lolote ili jambo kama hili lisitokee tena,” Mitsotakis amewaambia waandishi wa habari.

Uchunguzi wa polisi umeanzishwa kubaini chanzo cha ajali hiyo. Mwendesha mashtaka wa umma, Stamatis Daskopolopoulos, ambaye amepewa jukumu la kusimamia uchunguzi huo, alisema mashahidi wameanza kutoa ushahidi.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi