Kitaifa
Profesa Kitila aeleza umuhimu wa kutoa mikopo kwa Astashahada, Stashahada
Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, ameishauri Serikali kuanza utekelezaji wa mpango wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya astashahada na stashahada nchini.
Hata hivyo, Profesa Mkumbo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, ametoa tahadhari akisema haitakuwa sahihi kupunguza mikopo ya elimu ya juu na kuelekeza katika elimu ya vyuo vya kati.
Kauli hiyo ameitoa leo Februari 15, 2023 wakati wa mjadala wa Jukwaa la Mwananchi Space, lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited(MCL) kwa mada inayohoji maoni kuhusu umuhimu wa Serikali wa kutoa mikopo kwa astashahada na atashahada.
Mjadala huo unafanyika ikiwa ni siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na viongozi wa Shirikisho la Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), akiridhia ombi la kutaka kuongezewa fedha za kujikimu kutoka Sh8, 500 kwa siku hadi Sh10, 000.
Kuhusu wanafunzi wa ngazi ya cheti na stashahada kupata mikopo hiyo, Rais Samia alisema jambo hilo halitawezekana kwa sasa, wanakwenda kujipanga na kuweka mipango ya kulitekeleza siku zijazo.
Katika ufafanuzi wake, Profesa Mkumbo amesema atashiriki kuisukuma Serikali kuja na mkakati wa kugharamia mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kati kutokana na unyeti wa kundi hilo.
“Tanzania tuna wahandisi wengi zaidi kuliko technicians (mafundi mchundo), matokeo yake wanaopitia mfumo wa kati ni asilimia 25 waliobaki wanapitia elimu ya juu.
“Kwa hiyo uamuzi wa Serikali kutoa mikopo katika wanafunzi hao ni muhimu sana,”amesema Profesa Mkumbo.
“Kwa kawaida, wanaotakiwa kumaliza vyuo vya kati ni wengi kuliko vyuo vikuu kuliko vya kati lakini Tanzania ni kinyume chake. Lakini mikopo hiyo itaakisi Dira ya 2025, mpango wa miaka mitano na Ilani ya CCM. Kwa hiyo hakuna namna tukitekeleza itaonekana kama wanapata ufadhili.”